• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
Msimu wa utapeli waanza

Msimu wa utapeli waanza

Na BENSON MATHEKA

WANANCHI wameombwa kuwa macho dhidi ya kutapeliwa na wanasiasa ambao wameanza kuwatembelea mashinani kwa nia ya kuwashawishi wawapigie kura mwaka ujao.

Kulingana na mdadisi wa siasa Peter Warui, Wakenya wanafaa kufahamu kwamba wanasiasa sio marafiki wao, mbali ndio maadui wakubwa wa maendeleo na wanawatumia tu kuafikia malengo yao ya kisiasa.

Mtindo huu huwa unashuhudiwa kila wakati uchaguzi mkuu unapokaribia, kisha wanasiasa hao hutoweka baada ya kushinda au kushindwa.

Lakini wakati huu msimu huo umekuja mapema kutokana na ushindani unaotarajiwa kwenye uchaguzi wa mwaka ujao.

“Kuanzia sasa hadi 2022 utakuwa msimu wa wanasiasa kutapeli raia mashinani kupitia makundi ya wanawake, vijana, makanisa na kwenye matanga,” asema mwanaharakati James Wariara.

“Ukiona wanasiasa wakila chakula katika vibanda kijijini mwako, ujue kwamba msimu wa kudaganywa umefika na ni wewe wanataka kutapeli,” mwanahabari John Kamau alionya majuzi.

Miongoni mwa mbinu wanazotumia ni kutembelea maeneo ya mashinani ambako hawajafika kwa miaka minne iliyopita kujumuika na wananchi wa kawaida, kuhudhuria ibada makanisani, matanga na kutawazwa na wazee.

“Katika kutangamana na wananchi mitaani na vijijini, wanasiasa huwa wananyenyekea na kuahidi makubwa. Lakini mara baada ya uchaguzi huwa wanatoweka hadi msimu ujao wa uchaguzi,” asema Bw Wariara.

Wiki iliyopita, Kiongozi wa ODM Raila Odinga alitembelea soko la Burma jijini Nairobi, ambako alijumuika na wananchi wa kawaida kwa chakula cha mchana katika kibanda.

Mara ya mwisho wafanyabiashara wa mtaa huo walipotembelewa na mgombeaji wa urais na pengine mwanasiasa ilikuwa 2017 baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Wakati huo Rais Kenyatta alihutubia wafuasi wake eneo hilo ambapo alikashifu mahakama kwa hatua hiyo.

Bw Odinga pia ameanza kuhudhuria ibada makanisani Jumapili, mazishi na makundi mbalimbali akiwa na nia ya kuonyesha kuwa anajitambulisha na wananchi wa kawaida. Jumapili iliyopita alihudhuria ibada katika kanisa la Soweto Catholic mtaani Kayole, Nairobi.

Naibu Rais William Ruto naye amekuwa mstari wa mbele kutembelea maeneo wanakoishi wananchi wa kawaida ama kufanyia biashara, makanisani na mazishi kujipendekeza kwao akidai kuwa yeye ni ‘hasla’ kama wao.

Pia amekuwa akialika makundi ya wananchi wa kawaida katika nyumbani kwake Karen jijini Nairobi, na nyumbani kwake Sugoi mjini Eldoret kama mbinu ya kujionyesha kuwa anajali maskini.

Akiwa na kundi lake la ‘hasla’, Dkt Ruto pia amekuwa akitembelea maeneo ya mashinani kujitambulisha na maskini kwa kula kwenye vibanda duni, kununua mahindi choma na ndizi na kujifanya kushiriki shughuli zao za kawaida.

Kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi pia ni miongoni mwa wanasiasa wanaotumia mbinu hii.

“Huu ni msimu mwingine wa wanasiasa kukita kambi mashinani wakiwapa vijana pesa za kununua pombe wazome wapinzani wao, badala ya kuweka mazingira bora kwao wapate kazi na kuimarisha maisha yao. Wanapotumia vijana kupigana, watoto wao huwa wanalindwa na maafisa wa polisi katika mitaa ya kifahari mijini,” asema Bw Wariara.

Anasema wanasiasa huwa wanadhani kwamba baada ya miaka mitano, raia huwa wamesahau ahadi walizowapa bila kutimiza.

“Kwa mfano, Ruto anafikiri Wakenya walisahau ahadi ambazo aliwapa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017 akijifanya anawajali. Bw Odinga naye anafikiri Wakenya wamesahau kuwa anashirikiana na serikali aliyokuwa akikosoa kama iliyoshindwa kuwahudumia,” asema Bw Wariara.

You can share this post!

Bensouda afurahia kuruhusiwa kukagua vifaa vilivyomilikiwa...

Trump aacha Amerika yenye aibu na ubaguzi