• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Mswada wachanganya Wabunge upande wa UDA

Mswada wachanganya Wabunge upande wa UDA

NA WANDERI KAMAU

WABUNGE wa chama tawala cha United Democratic Movement (UDA) wako katika njiapanda ikiwa wapitishe Mswada wa Fedha 2023 au la, kutokana na pingamizi nyingi ambazo umepata kutoka kwa Wakenya.

Duru zinasema kuwa wabunge wengi wanahofia mustakabali wao kisiasa, kwa kuwa ikiwa wataupitisha, wataonekana kuwasaliti raia na ikiwa watakosa kuupitisha, basi wataonekana kumkaidi Rais William Ruto.

Bunge la Kitaifa limepangiwa kurejelea vikao vyake Juni 6, ambapo ripoti kuhusu mswada huo tata itawasilishwa ili kujadiliwa.

Ikiwa mswada huo utapitishwa, basi hilo litatoa nafasi kwa Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung’u, kusoma Bajeti ya Mwaka wa Kifedha 2023/2024 mnamo Juni 15.

Tayari, Rais Ruto amewarai wabunge hao kuupitisha mswada huo, kupitia Mkutano wa Wabunge alioongoza katika Ikulu mnamo Jumanne.

Kwenye mkutano huo, Rais aliwarai wabunge kuupitisha mswada huo ili kuiwezesha serikali yake kutimiza ahadi alizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni zake mwaka 2022.

Lakini licha ya Rais, Naibu Rais Rigathi Gachagua na maafisa wengine serikalini kuupigia debe mswada huo na kuwahimiza wabunge kuupitisha, wengi wameripotiwa kuingiwa na wasiwasi kuhusu maamuzi watakayofanya ili kujiokoa kisiasa.

Ingawa wengi wametoa hakikisho kuwa wataunga mkono mswada huo, duru zimeeleza ‘Taifa Jumapili’ kuwa, baadhi wanabuni njia za kukwepa kushiriki kwenye shughuli za upigaji kura, ili kutoonekana kuwasaliti raia.

“Wabunge wengi wanabuni kila mbinu kukwepa kushiriki katika upigaji kura bila kuonekana kumkasirisha Rais na bila kuonekana kuwasaliti raia. Wengine hata wameanza mipango ya kusafiri nje ya nchi kama njia ya kutoa kisingizio cha kutoshiriki kwenye zoezi hilo,” zikaeleza duru.

Bajeti ya mwaka huu itasomwa Juni 15, na itakuwa bajeti ya kwanza chini ya Rais Ruto tangu alipochukua uongozi Septemba mwaka uliopita.
Hayo yanajiri huku muungano wa Azimio la Umoja ukiwahimiza wabunge wake kuukataa mswada huo, kwa kuwa “utawadhulumu raia”.

Mnamo Jumatatu, kiongozi wa Azimio, Raila Odinga, aliwaomba wabunge wake kufanya kila wawezalo kuhakikisha mswada huo hautapitishwa na Bunge.

“Tunawataka Wakenya kufahamu kuwa, huu ni Mswada wa Kenya Kwanza. Ni bajeti ya Kenya Kwanza. Ni njia ya Kenya Kwanza kuwafinya Wakenya. Tutawaagiza wabunge wetu kuuangusha,” akasema Bw Odinga.

Baadhi ya masuala tata yaliyo kwenye mswada huo ni pendekezo la kuwatoza Wakenya walioajiriwa asilimia tatu ya mishahara yao, ambapo serikali inalenga kutumia fedha hizo kutekeleza mpango wa kitaifa wa ujenzi wa nyumba, kuwawezesha Wakenya kupata nyumba kwa bei nafuu.

Hata hivyo, pendekezo hilo limekosolewa vikali na maelfu ya waajiri na wafanyakazi, wengi wakieleza hofu ya kupoteza ajira zao ikiwa litaanza kutekelezwa.

Wiki iliyopita, Afisa Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Waajiri (FKE), Bi Jacqueline Mugo alionya kwamba, huenda mashirika mengi yakalazimika kuwafuta kazi maelfu ya wafanyakazi, kwa kuwa itakuwa vigumu kutoa ada hizo chini ya hali ya kiuchumi ya sasa.

“Ikiwa serikali itatekeleza mpango huo, basi waajiri wengi hawatakuwa na lingine ila kuwafuta baadhi ya wafanyakazi. Ni vizuri pawe na mashauriano ya kutosha kuhusu pendekezo hilo,” akasema Bi Mugo.

Walimu pia wametoa kauli kama hiyo, wakiihimiza serikali kuwaongezea mishahara kwanza kabla ya kuanza kutekeleza mpango huo.

Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) na Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo Anuwai (KUPPET) vimesema kuwa, viko kwenye mazungumzo na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) vikiitaka kuwaongeza mishahara kwa asilimia 60 na 42 mtawalia kabla ya serikali kuanza kuwatoza ada hiyo.

“Hali ilivyo, itailazimu serikali iwaongezee walimu mishahara kabla ya kuanza kuwatoza ada hiyo, kwani wengi wana ada na mikopo mingi sana wanayolipia,” akasema Katibu Mkuu wa KNUT, Bw Collins Oyuu.

Kulingana na wadadisi, mwelekeo ambao wabunge wamechukua unafaa kumfungua macho Rais Ruto kutathmini tena baadhi ya mapendekezo tata yaliyo katika mswada huo.

Kenya Kwanza ina jumla ya wabunge 181 katika Bunge la Kitaifa huku Azimio ikiwa na wabunge 159, baada ya baadhi yao kuhamia katika Kenya Kwanza.

Kwa mswada wa bajeti kupita katika Bunge, huwa unahitaji kuungwa mkono na angaa wabunge 50 ili kuwa sheria.

  • Tags

You can share this post!

Funga-kazi EPL vikosi vikipigana ya mwisho

Gaucho: Uhuru hajaninunulia gari

T L