• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
MUUNGANO WA RAILA, RUTO WAINGIA DOA

MUUNGANO WA RAILA, RUTO WAINGIA DOA

JUSTICE OCHIENG’ na ONYANGO K’ONYANGO

WAFUASI wa Naibu Rais Dkt William Ruto na wale wa Kinara wa ODM Raila Odinga wamegawanyika kuhusu nani awanie Urais kati ya wawili hao huku madai kuwa muungano kati yao unanukia yakizidi kushika kasi.

Mrengo wa Dkt Ruto unamtaja kama anayefaa kuingia ikulu, ikizingatiwa kuwa amehudumu kama Naibu Rais kwa mihula miwili na katiba haimruhusu kuwa mgombea mwenza tena.

Vilevile, majemedari wa Dkt Ruto wanadai kwamba, hata endapo ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) itapitishwa na wadhifa wa Waziri Mkuu ubuniwe, nafasi hiyo si ya hadhi ya kushikiliwa na Naibu Rais ambaye yupo pua na mdomo kutua ikuluni.

Kwa upande mwingine, wandani wa Bw Odinga wanamtaja kama mwanasiasa mkongwe mwenye tajriba pana, ambaye anafaa kuhudumu kama Rais, angalau kwa muhula moja.

Aidha, wanasisitiza kuwa Bw Odinga hawezi kuhudumu kama Waziri Mkuu baada ya kushikilia wadhifa huo katika iliyokuwa serikali ya ‘nusu mkate’ kati ya 2008-2013. Pia wanadai kwamba, Bw Odinga ndiye mwanasiasa mwenye ushawishi zaidi nchini baada ya Rais Uhuru Kenyatta, na kuendea wadhifa mwingine kutakuwa kama kujishusha hadhi kisiasa.

Suala jingine ambalo linazua hofu katika kambi ya Dkt Ruto ni kuwa, amejizolea umaarufu mkubwa katika ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya, na yupo katika hatari ya kupoteza ushawishi huo iwapo ataridhiana na Bw Odinga.

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata japo anasisitiza kuwa muungano kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto utashinda uchaguzi wa 2022 kwa urahisi, mtihani mkubwa ni iwapo Mlima Kenya utaendelea kumuunga mkono Naibu Rais akiamua kushirikiana na Bw Odinga asiyeshabikiwa na jamii ya eneo hilo.

“Si siri kwamba Wakikuyu wamewekeza kisiasa katika kambi ya Naibu Rais na iwapo ataungana na Bw Odinga, basi lazima wahakikishe wanajumuisha mwanasiasa kutoka Mlima Kenya. Ushirikiano kati ya wawili hao ni tiketi ya moja kwa moja ya kuingia ikulu,” akasema Bw Kang’ata.

Mbunge wa Belgut Nelson Koech na Seneta wa Bomet Christopher Lagat nao wanadai kwamba urais wa Dkt Ruto si suala la kughairiwa na Bw Odinga anafaa kujiunga na vuguvugu la Hustler kuchukua wadhifa wa waziri mkuu.

“Yeyote anayetaka kujiunga nasi anafaa asahau kugombea kiti cha Urais. Kwa mtazamo wangu, ni mapema sana kuzungumzia muungano wa Naibu Rais na Bw Odinga,” akasema Bw Koech.

Hata hivyo, seneta maalum Rose Nyamunga, mwandani wa Bw Odinga anasema kuwa Dkt Ruto ni mwanafunzi wa kisiasa wa Bw Odinga na ushirikiano kati ya wanasiasa hao wawili ni jambo linalowezekana.

Mbunge wa Emurrua Dikir Johana Ngeno ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya Kanu na yupo mrengo wa Dkt Ruto naye anasisitiza kuwa muungano wa Ruto-Raila ndio unahitajika nchini.

“Kama Rais Kenyatta amefanya kazi na Raila hata Naibu Rais anaweza kufanya hivyo. Ikumbukwe walishirikiana vyema mnamo 2007 na wanafahamiana,” akasema Bw Ng’eno.

Mchanganuzi wa kisiasa Javas Bingambo hata hivyo anasema Bw Odinga na Dkt Ruto watashirikiana tu kuelekea 2022 si kwa sababu ya urafiki wao bali kulinda maslahi yao ya kisiasa.

You can share this post!

Ielewe teknolojia ya 5G iliyozinduliwa na Safaricom na...

Waliotia ‘mchele’ kwa pombe ya mteja wakamatwa