• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Mwisho wa maandamano ni Jumatatu – Gachagua

Mwisho wa maandamano ni Jumatatu – Gachagua

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameonya kuwa Jumatatu, Aprili 3, 2023 ndio itakuwa siku ya mwisho kwa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kufanya maandamano kwani serikali haitasita kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya waandamanaji waharibifu.

Akiongea Jumamosi katika ibada ya maombi ya kutoa shukrani katika eneobunge la Malava, Kaunti ya Kakamega, Bw Gachagua amewaonya vijana watakaothubutu kuharibu mali kwamba mkono wa sheria utawaandama.

“Nawaonya vijana ambao wamekuwa wakitumia fujo za maandamano kuiba mali, kuwapora watu na kutenda aina nyingine za uhayawani. Jumatatu ni siku yenu ya mwisho kufanya hivyo,” Bw Gachagua akasema.

Naibu Rais amesema kuwa imebainika kuwa maandamano hayo sio ya amani na yamegeuka kuwa ghasia za baada ya uchaguzi.

“Haya sio maandamano bali ni ghasia za baada ya uchaguzi kwani raia wasio na hatia wanaporwa na kushambuliwa kiholela. Huo ni uhalifu mkubwa kulingana na sheria ya uhalifu,” Bw Gachagua akasema.

Naibu Rais amesema Jumatatu, serikali itatekeleza kikamilifu wajibu wake wa kulinda maisha, mali na kudumisha utawala wa kisheria.

Onyo la Bw Gachagua linajiri siku moja baada ya kiongozi wa Azimio Raila Odinga kushikilia kuwa maandamano ya Jumatatu “yatakuwa mama ya maandamano yote.”

Bw Odinga amekuwa akiongoza maandamano akiishinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha, kushirikisha wadau wengine katika mchakato wa uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kufungua kwa mitambo ya tume hiyo ya kupokea matokeo ya uchaguzi wa urais, almaarufu, sava.

Mwanasiasa huyo mkongwe anashikilia kuwa maandamano hayo yatakuwa yakifanyika kila Jumatatu na Alhamisi kila wiki hadi serikali itakapokubali kutimiza matakwa yao.

  • Tags

You can share this post!

Man-City watandika Liverpool 4-1 katika EPL

Mradi wa majumba Kijani Ridge watunukiwa sifa

T L