• Nairobi
  • Last Updated May 29th, 2023 9:37 PM
Mzozo waendelea kuchacha Jubilee

Mzozo waendelea kuchacha Jubilee

BENSON MATHEKA Na RICHARD MUNGUTI

MZOZO wa uongozi wa uongozi katika chama cha Jubilee unaendelea kuchacha licha ya Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta kuandaa mkutano maalumu wa wajumbe wa kitaifa (NDC) uliowatimua wanachama waasi wanaoungwa mkono na serikali.

Waasi hao wanaoongozwa na mbunge maalumu Sabina Chege na mwenzake wa Bunge la Afrika Mashariki Kanini Kega, bado wanashikilia kuwa ndio wanatambuliwa rasmi kama viongozi wa chama hicho licha ya kutimuliwa na mrengo unaoongozwa na Uhuru na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni.

Bi Chege na Bw Kega wanasisitiza kuwa, msajili wa vyama vya kisiasa Ann Nderitu aliidhinisha uamuzi wa Baraza Kuu la Kitaifa la chama mnamo Februari 10, 2023 na uliotimua Bw Kenyatta, Bw Kioni, Naibu mwenyekiti David Murathe na Bw Kagwe Gichohi chamani mnamo Mei 10.

“Kufuatia ukaguzi wa stakabadhi zilizowasilishwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya kisiasa na katiba ya chama, ofisi hii imeridhika kwamba, chama kilifuata mchakato unaohitajika. Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya kisiasa, ofisi hii imebadilisha rekodi zake na sajili ya wanachama wa chama,” Bi Nderitu alisema katika barua aliyomwandikia Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee, Joshua Kutuny mnamo Mei 19, 2023.

Bw Kutuny ni mmoja wa waliotimuliwa na NDC iliyoitishwa na mrengo wa Uhuru na Bw Kioni pamoja na Bi Chege, Bw Kega na wengine wanaoshirikiana na muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Ni kwa nguvu za barua hii ambapo Bw Kega alipuuza kongamano la Jumatatu lililomtimua pamoja na washirika wake akilitaja kama mkutano wa kawaida wa kisiasa akisema haukuwa halali.

Akihutubia wanahabari muda mfupi baada ya kutimuliwa Jubilee, Bw Kega alipuuza NDC aliyoitisha Uhuru akisisitiza rais huyo mstaafu hana mamlaka ya kufanya maamuzi ya chama.

Bw Kega alisisitiza kuwa, mrengo wake utamchukulia Uhuru hatua za kinidhamu kwa kufuata mchakato wa kutatua mizozo ndani ya chama.

Hata hivyo, iliibuka kuwa mrengo wa Bw Kenyatta, kupitia Bw Kioni ulikuwa umepata agizo la Mahakama la kusimamisha kwa muda uamuzi wa mrengo hasimu wa Bi Chege na Bw Kega wa kuwatimua chamani.

Agizo lililotolewa na Mahakama ya Kutatua mizozo ya kisiasa Jumatatu Mei 22 2023 lilizuia mrengo wa Bw Kega na msajili wa vyama vya kisiasa kutekeleza uamuzi wa jopo la nidhamu la chama cha Jubilee wa kutimua Bw Kioni na wenzake.

“Agizo la muda linatolewa kusimamisha uamuzi wa jopo la nidhamu la mshtakiwa wa kwanza (chama cha Jubilee) wa kumtumia mlalamishi.”

“Agizo la muda linatolewa kuzuia mshtakiwa wa pili (msajili wa vyama vya kisiasa) kutekeleza mawasiliano ya mshtakiwa wa kwanza (chama cha Jubilee) yanayodai kutimua mlalamishi kutoka uanachama,” linasema agizo lililotolewa na mwenyekiti wa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa, Desma Nungo.

Haya yanajiri huku Bw Kenyatta akisisitiza kuwa hataachilia uongozi wa chama hicho na muungano wa Azimio ukitisha kujiondoa katika mazungumzo ya kamati teule ya bunge yaliyoufanya kusitisha maandamano iwapo serikali itaendelea kuvuruga Jubilee.

“Kuna wakati ambao nilifikiria nitastaafu kutoka siasa. Nilifikiria ningekuja kwa NDC kukabidhi uongozi hadi pale baadhi ya watu walipoanza vitisho. Ninataka kuwaambia kwamba, watishe mtu mwingine lakini sio mimi,” alisema Bw Kenyatta.

Jana Jumanne, mrengo wa Bw Kenyatta ulitarajiwa kuwasilisha kwa msajili wa vyama vya kisiasa, uamuzi wa NDC Jumatatu wa kuwatimua chamani Bi Chege, Bw Kega na washirika wao.

Akizungumza akiwa Siaya jana Jumanne, kiongozi wa Azimio Raila Odinga alishambulia serikali kwa kushawishi msajili wa vyama vya kisiasa kutoidhinisha kutimuliwa kwa waasi wa chama cha Jubilee na mkutano mkuu wa wajumbee (NDC) uliofanyika Jumatatu.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge Alice Ng’ang’a atoa basari, aahidi...

Mke wa King Kaka akumbuka alivyolipa bili ya deti ya kwanza...

T L