• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Mzozo wazidi Jubilee Kega akifutilia mbali mkutano alioitisha kinara wake Uhuru

Mzozo wazidi Jubilee Kega akifutilia mbali mkutano alioitisha kinara wake Uhuru

NA WANDERI KAMAU

WAASI katika Chama cha Jubilee (JP) jana Jumanne waliendelea kumwelekezea vita vya kisiasa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, baada ya Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Kanini Kega, kufutilia mbali mkutano uliokuwa umeitishwa na Bw Kenyatta.

Bw Kenyatta alikuwa ameitisha Mkutano Maalum wa Wajumbe wa chama Mei 22, ili kujadili mizozo ambayo imekuwa ikikikumba chama hicho.

Kikao hicho kilikuwa kimepangiwa kufanyika katika Ukumbi wa Bomas, jijini Nairobi, kulingana na tangazo lililochapishwa na rais huyo mstaafu mnamo Aprili 23.

Lakini Jumanne, Bw Kega alifutilia mbali mkutano huo, akisema kuwa chama kitatangaza tarehe mpya ya mkutano mwingine.

“Tafadhali fahamu kuwa Baraza la Kitaifa la Chama (NEC) limesimamisha tangazo la Kikao Maalum cha Kitaifa cha Wajumbe (SNDC) lililochapishwa katika vyombo tofauti vya habari Aprili 29, 2023. Chama kitatoa tangazo jipya kuhusu kikao kingine cha kitaifa cha wajumbe kulingana na maamuzi ya NEC mnamo Februari 10, 2023,” akasema Bw Kega kwenye taarifa.

Tangazo hilo linaonekana kuongeza mzozo ambao umekuwepo baina ya Bw Kenyatta na wanasiasa waasi katika chama hicho kuhusu umiliki wake.

Mzozo wa udhibiti wa chama hicho unahusisha makundi mawili makuu—moja linalomuunga mkono Bw Kenyatta na linaloongozwa na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni na jingine linalomuunga mkono Rais William Ruto, linaloongozwa na Bw Kega.

Kufuatia tangazo la jana, wadadisi wa siasa wanasema kuwa mzozo wa udhibiti wa chama hicho umemsukuma Bw Kenyatta kwenye kona, na lazima kuwe na juhudi za pamoja kusuluhisha mvutano huo kabla yake kutokota.

“Mahali mzozo huu unaelekea si pazuri. Lazima pawe na juhudi za kuusuluhisha haraka iwezekanavyo kwani kuna uwezekano utampaka tope Bw Kenyatta na kumshusha hadhi yake kama rais mstaafu,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mhadhiri na mdadisi wa siasa.

Kundi la Bw Kioni limekuwa likidai kuwa kundi la Bw Kega linafadhiliwa na serikali ya Kenya Kwanza, madai ambayo kundi hilo limekuwa likikana.

Mrengo wa Bw Kega unajumuisha Mbunge Maalum Sabina Chege, mwenyekiti Nelson Dzuya, wabunge Adan Keynan (Eldas), Kwenya Thuku (Kinangop) kati ya wengine.

Mzozo huo ulitokota kuanzia wiki iliyopita, baada ya mrengo wa Bw Kega kumtangaza Bi Chege kama Kaimu Kiongozi wa chama, kabla ya kuandaliwa kwa kikao kipya cha chama kuwachagua viongozi wapya.

Hatua hiyo ilifasiriwa kama ‘jibu’ kwa Bw Kenyatta, baada ya yeye kuripotiwa kumfurusha Bw Kega na wenzake chamani kupitia barua za siri zilizotiwa saini na zilizoeleza kujiuzulu kwao.

  • Tags

You can share this post!

Masaibu ya wazazi shule zikifunguliwa

Maaskofu wa kanisa la Anglikana wasema ukabila, mivutano ya...

T L