• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 AM
NDC ya Jubilee kuandaliwa uwanjani Ngong Racecourse

NDC ya Jubilee kuandaliwa uwanjani Ngong Racecourse

NA CHARLES WASONGA

KONGAMANO tata la Wajumbe wa Kitaifa (NDC) lililoitishwa na mrengo wa Jubilee unaoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta sasa litafanyika Mei 22, 2023 katika uwanja wa Ngong Racecourse, Nairobi baada ya kuzimwa Bomas of Kenya.

Katika tangazo la kulipiwa lililochapishwa katika gazeti la Saturday Nation, toleo la Mei 20, 2023, Bw Kenyatta ameeleza kuwa ajenda na maelezo mengine kuhusu kongamano hilo yanasalia yalivyo katika tangazo la Aprili 29, 2023 la kujulisha wajumbe kuhusu kikao hicho.

“Notisi inatolewa hapa kwamba mahala pa kufanyika kwa NDC pamehamishwa hadi uwanja wa Ngong Racecourse, Nairobi. Maelezo mengine yote yanasalia kulingana na notisi iliyochapishwa mnamo Aprili 29, 2023,” Bw Kenyatta akasema kupitia tangazo hilo.

Hatua hii inajiri baada ya usimamamizi wa Bomas of Kenya, ambako awali kongamano hilo liliratibiwa kufanyika, kutangaza kuwa ukumbi uliokodiwa na Jubilee unafanyika ukarabati kwa muda wa majuma manane.

Meneja wa Uvumishaji na Uhusiano Mwema wa Bomas of Kenya Glady Kangethe, katika barua kwa kaimu mkurugenzi mkuu wa Jubilee, Polycarp Hinga akaongeza hivi:

“Jinsi mnavyofahamu, wakati huu kumbi zetu zingine zinatumiwa na Kamati na Jopokazi mbalimbali zinazoshughulikia masuala nyeti zenye umuhimu wa kitaifa. Mteja mwingine pia amekodi ukumbi mwingine mkubwa. Kwa hivyo, hatutaweza kuwapa nafasi ya kufanya kongamano lenu la kitaifa la wajumbe, Bi Kang’ethe akasema kwenye barua kwa Hinga aliyoiandika Mei 12, 2023.

Lakini maafisa wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa Bw Kenyatta walipuuzilia mbali hatua hiyo wakishikilia kuwa NDC hiyo itaendelea katika uwanja mwingine.

Naibu Mwenyekiti David Murathe alisema mkutano huo utaendelea Jumatatu ulivyopangwa licha ya kile alichokitajia kama njama ya serikali kuwazuia kutumia kumbi za umma.

“Mkutano wetu ungalipo. Tutatangaza mahala pengine pa kufanyia mkutano na kualika wajumbe wetu kupitia jumbe fupi kupitia simu. Watajulishwa mapema,” akasema Bw Murathe.

Afisa huyo ambaye alitimuliwa afisini na kundi linaloongozwa na Mbunge wa Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega na Mbunge Maalum Sabina Chege mnamo Februari 13, 2023, alisema kuwa Bw Kenyatta ndiye ataongoza NDC hiyo katika wadhifa wake kama Kiongozi wa Kitaifa wa Jubilee.

Vinara wakuu wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Martha Karua na wanachama wa vyama vingine tanzu katika muungano huo pia wanatajiwa kuhudhuria kongamano hilo.

  • Tags

You can share this post!

Simbas yalenga kurarua Zimbabwe Currie Cup

Rais atelekeza ahadi baada ya kutua ikulu

T L