• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
ODM yamkubali Kingi kwa masharti

ODM yamkubali Kingi kwa masharti

Na MAUREEN ONGALA

CHAMA cha ODM kimesema Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, yuko huru kumuunga mkono Bw Raila Odinga kwa urais, ila kwa masharti kuwa hatatatiza shughuli za chama hicho.

Wiki iliyopita, Bw Kingi aliashiria kuwa ataungana na Bw Odinga chini ya muungano mpya wa Azimio la Umoja kuelekea kwa uchaguzi ujao wa urais kupitia kwa chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA).

Hata hivyo, Mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire, amemtaka gavana huyo adhihirishe uaminifu wake kwani hakuhudhuria mkutano wa hadhara wa Azimio la Umoja jijini Nairobi.

Wakati huo huo, Mbunge huyo wa Ganze alidai gavana huyo anayetumikia kipindi cha pili cha ugavana atakuwa hatarini kusahaulika kisiasa ikiwa ataendelea kukwamilia PAA.

Alimtaka azingatie kurudi katika ODM badala ya kumshabikia Bw Odinga kupitia kwa mlango wa nyuma.

“Huu mwelekeo anaochukua utamfanya apoteze umaarufu wake. Ajiunge nasi, na tutamkaribisha. Kile alichofanya (kukosa kuhudhuria mkutano wa Azimio la Umoja) kilikuwa ni unafiki. Lakini tunatumai ataambia wafuasi wake kwa nini hakuwa katika mkutano huo ilhali anatambuliwa kama kiongozi wa chama,” akasema.

Alitoa changamoto kwa Bw Kingi kuhudhuria mkutano ujao wa ODM ambapo Bw Odinga anatarajiwa kuzindua manifesto yake ili adhihirishe iwapo kweli anataka ushirikiano na chama hicho alichoasi.

Alikuwa akizungumza wakati alipokabidhi miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) katika shule za msingi za Bahati na Yembe, Kaunti Ndogo ya Bahati mnamo Jumanne.

Bw Mwambire alisema endapo Bw Kingi atasisitiza kukwamilia PAA, itabidi ajiandae kwa makabiliano makali kwani ODM haiko tayari kuachia vyama vingine viti vya kisiasa bila ushindani.

Viongozi wa PAA walikuwa wamekutana wiki chache zilizopita wakapitisha kauli kwamba chama kitasimamisha wagombeaji wa nyadhifa zote isipokuwa urais pekee.

“Yuko huru kumpigia kampeni Baba (Bw Odinga) lakini inafaa akumbuke kuwa Kilifi bado ni ngome ya ODM wala si PAA. Hata wale ambao wanajifanya kuegemea chama chake watamtoroka ifikapo Februari 2022,” akasema.

Bw Kingi alikuwa miongoni mwa wanasiasa ambao waliasi ODM punde baada ya Bw Odinga kutangaza ushirikiano na Rais Uhuru Kenyatta baada ya uchaguzi wa 2017 uliokumbwa na utata.

Huku baadhi ya wanasiasa waliokuwa ODM wakihamia upande wa Naibu Rais William Ruto, gavana huyo aliamua kuanzisha juhudi za kutafuta umoja wa Wapwani kisiasa.

Majaribio yake kuunganisha vyama vya Pwani ili kuwe na chama kimoja yaligonga mwamba kwani viongozi wa vyama hivyo walikataa pendekezo lake, huku wanasiasa ambao awali walikuwa wakishirikiana naye katika wito huo wakihepa.

Katika hotuba zake, Bw Kingi husisitiza kuwa hatua yake ya kuunda PAA ilinuiwa kuletea jamii za Wapwani chama ambacho wanaweza kutumia kutafuta nafasi katika meza ya uongozi wa kitaifa, akisema eneo hilo limekuwa likitengwa kwa muda mrefu kwa vile viongozi wamegawanyika.

Mnamo Agosti, ODM iliamua kumpokonya wadhifa wake wa uenyekiti, tawi la Kilifi ndipo Bw Mwambire akapewa wadhifa huo.

Bw Kingi aliondolewa pia katika wadhifa wake wa uenyekiti ODM, tawi la Kaunti Ndogo ya Magarini ambao alikuwa ameshikilia tangu mwaka wa 2010 alipokuwa mbunge wa eneo hilo.

You can share this post!

Ahimiza wazazi kulinda watoto wasibebwe na maji

Jamii ‘kutakasa’ mnara wa Ngala

T L