• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
OKA hatarini kuporomoka, Moi adaiwa kumuunga mkono Raila

OKA hatarini kuporomoka, Moi adaiwa kumuunga mkono Raila

Na JUSTUS OCHIENG’

MGAWANYIKO umeibuka katika Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) baada ya viongozi wake kulaumiana kuhusu uhusiano na baadhi ya wapinzani wao, pamoja na kuanza kuchukua misimamo mikali kuhusu anayepasa kuwa mwaniaji wao wa urais 2022.

Kuzimwa kwa BBI pia kumeweka muungano huo unaoshirikisha Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi na Moses Wetang’ula (Ford Kenya) katika hali ya mshikemshike. BBI ilikuwa moja ya sababu za kubuniwa kwa muungano huo ili kuipigia debe, viongozi wake wakitegea kunufaika kutokana na kubuniwa kwa nafasi zaidi za uongozi wa juu.

Katibu Mkuu wa Kanu, Nick Salat aliambia Taifa Leo kuwa mshikamano mkuu wa OKA ulikuwa ni BBI, na vile hatima yake inaning’inia huenda ukasambaratika.

“Kwa njia moja au nyingine, sisi sote tunaunga mkono BBI. Hii ni kwa sababu bila BBI basi hata huu muungano wa OKA hautakwepo,” akasema Bw Salat.

Duru zinasema baadhi ya viongozi wanahisi kuwa Mwenyekiti wa Kanu, Seneta Gideon Moi wa Baringo ana njama ya kumuunga mkono Kinara wa ODM, Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022 badala ya mmoja kutoka muungano huo.

Bw Salat alimtetea Bw Moi akisema ushirika wake na Bw Odinga ni wa kipekee kwa kuwa wao ni marafiki: “Raila na Moi ni marafiki na tunaweza kumtembelea ‘baba’ wakati wowote tunapopata nafasi.” ?Alitaja wanaomkashifu Bw Moi kama wanasiasa ambao wanajipenda, akiashiria kwamba shutuma zao ndio utakuwa mwanzo wa kusambaratika kwa OKA.

Urafiki wa Mabw Odinga na Moi unaonekana kushamiri huku seneta huyo akiwa amemtembelea Bw Odinga mara mbili nyumbani kwake katika muda wa miezi miwili.

Bw Moi alimjulia hali waziri huyo mkuu wa zamani nyumbani kwake mtaani Karen mnamo Aprili 13, na pia siku ya Madaraka Dei katika makazi yake jijini Kisumu, kisha wawili hao wakaandamana moja kwa moja hadi uwanja wa Jomo Kenyatta ambapo sherehe hizo zilikuwa zikiendelea.

Kudhihirisha kwamba hali si nzuri katika OKA, Mbunge wa Lugari Ayub Savula, ambaye ni mshirika wa Bw Muidavadi, alisema kuwa ushirikiano wa Mabw Odinga na Moi hauwashtui, akisisitiza kuwa liwalo liwe, mwaniaji wa urais wa OKA atakuwa Bw Mudavadi.

Bw Savula alidai kwamba kinara wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula tayari amekubali kumuunga mkono Bw Mudavadi 2022, na hilo linamweka makamu huyo wa rais wa zamani pazuri zaidi kupeperusha bendera ya muungano huo kuliko Bw Musyoka na Bw Moi.

“Sisi tunafahamu kwamba mwaniaji wa OKA ni Mudavadi. Moi hana ushawishi Bonde la Ufa na hata BBI iliangushwa katika kaunti anayowakilisha ya Baringo. Kalonzo naye si mwaniaji imara na kwa kuwa Wetang’ula anaunga Mudavadi mkono, basi Wiper haiwezi kupeperusha bendera ya muungano,” akasema Bw Savula.

“Gideon alijiunga na siasa baada ya Mudavadi, kwa hivyo hana nafasi kabisa kutwaa tiketi ya OKA. Hatuna mwaniaji mwingine ila Mudavadi, hata tukiitwa watu wenye msimamo mgumu,” akaongeza mbunge huyo.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Wiper, Victor Swanya na Katibu Mtendaji wa Ford Kenya, Chris Mandu Mandu walimtetea Bw Moi wakisema vinara wa OKA wapo huru kutangamana na kushirikiana na wanasiasa wengine kwa ajili ya umoja wa taifa.

You can share this post!

Safari Rally itakuwa ‘mnyama’ tofauti na yule tumezoea...

Makahaba sasa wapeleka ‘huduma’ kwa nyumba za...