• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Vita vya magavana, Kalonzo pigo kwa Raila Ukambani

Vita vya magavana, Kalonzo pigo kwa Raila Ukambani

Na PIUS MAUNDU

VITA vya ubabe vinavyoendelea kati ya magavana watatu wa eneo la Ukambani kwa upande mmoja na viongozi wa Wiper kwa upande mwingine, ni pigo kwa kampeni za kumvumisha kiongozi wa ODM Raila Odinga eneo hilo.

Huku magavana Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni), wakiendesha kampeni wiki jana, waliongeza uhasama kati yao na chama cha Wiper kwa kudai kuwa kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka aliitisha Sh3 bilioni ili ajiunge na Azimio la Umoja.

Uhasama kati ya kambi hizo mbili ulijitokeza Jumamosi katika hafla ya mazishi ambayo pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna na naibu kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya katika Kaunti ya Makueni.

Viongozi hao wa ODM walikuwa wametoka mjini Mutomo ambako waliungana na magavana hao watatu kumpigia debe Bw Odinga.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, alimkashifu waziri huyo mkuu wa zamani kwa kile alichodai ni kuwatumia magavana hao wa Ukambani kumhujumu Bw Musyoka katika ngome yake.

“Mbona mnamtusi Bw Musyoka ikiwa mnataka ajiunge na Azimio la Umoja. Ongeeni nasi vizuri,” Bw Kilonzo aliyeonekana mwenye hasira, akasema, huku akishangiliwa na waombolezaji.

Seneta huyo ambaye ni kiranja wa wachache katika Seneti, alisema Bw Musyoka hafai kulazimishwa kuunga mkono azma ya Bw Odinga kuwania urais.

Hata hivyo, Gavana Oparanya na Bw Sifuna walipuuzilia mbali madai ya Seneta Kilonzo Junior wakiyataja kama yasiyokuwa na msingi wowote.

Wawili hao walisema Bw Odinga anamheshimu Bw Musyoka zaidi na hawezi kumhujumu kwa njia yoyote.

Viongozi hao wa ODM walitumia nafasi hiyo kuwarai wafuasi wa Bw Musyoka wamuunge mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9, 2022.

Majibizano hayo yaliyotokea huku fununu zikienea kwamba Bw Musyoka anafanya mazungumzo na Bw Odinga kwa lengo la kufanya kazi pamoja kuelekea uchaguzi huo.

Duru zinasema kuwa Bw Musyoka anataka atambuliwe kama kiongozi mwenye ushawishi katika eneo la Ukambani, wazo ambalo magavana hao watatu hawataki kukumbatia.

Bi Ngilu, Prof Kibwana na Dkt Mutua, wanahisi kuwa Bw Musyoka anachelewa kutoa mwelekeo kwa jamii ya eneo hilo kwa kujivuta kujiunga na Azimio la Umoja.

“Hatuhitaji mtu mwingine kumfanyia kampeni Bw Odinga katika eneo la Ukambani. Tuna uwezo wa kumwezesha Bw Odinga kupata kura za urais katika eneo hili. Mtu yeyote kutoka jamii yetu ambaye anajivuta, akisubiri abembelezwe, anapoteza wakati wake,” alisema Bi Ngilu majuzi baada ya kukutana na baadhi ya wataalamu kutoka Ukambani, viongozi wa kidini na wafanyabiashara, katika hoteli moja mjini Machakos.

“Ikiwa ni pesa wanatafuta, warejee kwa jamii. Tutawachangia pesa hizo,” akaongeza.

You can share this post!

Himizo wafuasi wa ODM wajiandikishe kushiriki mchujo

Juhudi zilivyofanywa kupata wa kumkabili Nyong’o Agosti

T L