• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
‘Plan B’ ya Raila

‘Plan B’ ya Raila

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, anaonekana kusuka mikakati chini ya maji kurejea katika maandamano iwapo mazungumzo ya maridhiano kati ya muungano huo wa upinzani na ule unaotawala wa Kenya Kwanza yatagonga ukuta.

Tayari, kila upande umeteua wabunge saba kwenye meza ya mazungumzo, huku Kenya Kwanza ikikataa kuzungumzia masuala ambayo Azimio inasisitiza ni sharti yashughulikiwe ikiwemo kufunguliwa kwa sava ambazo IEBC ilitumia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, na kurudishwa kazini kwa makamishna waliokataa matokeo ya urais.

Ingawa imeteua wanachama saba kushiriki mchakato wa bunge alioitisha Rais William Ruto, Azimio pia inataka mazungumzo hayo yapanuliwe kuhusisha wadau wengine nje ya bunge, ombi ambalo Kenya Kwanza imekataa na kutangaza kuwa mazungumzo yatajikita katika suala la mchakato wa kuajiri makamishna wapya wa IEBC.

Hii inaonekana kumfanya Bw Odinga kushuku Kenya Kwanza haina nia njema na ameanza kuandaa mikakati ya kurudia maandamano kwa kuitisha vikao na mikutano ya mashauriano na wafuasi.

“Huku majadiliano yakiendelea (ndani ya Bunge), tutaanza msusuru wa mashauriano ya moja kwa moja na umma kupitia vikao na mikutano ya mashauriano,” akasema mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio, Wycliffe Oparanya katika taarifa punde baada ya Kenya Kwanza kuteua kikosi cha wabunge kitakachouwakilisha katika mazungumzo.

Bw Oparanya amesema wanasubiri mchakato wa bunge kuanza kabla ya kuamua hatua ya kuchukua lakini akasema vikao vya mashauriano vitaanza leo Nairobi vitakavyohusisha viongozi wa kidini, mashirika ya kijamii na yale yasiyo ya kiserikali pamoja na viongozi wengine watakaochaguliwa kupata maoni yao.

Hata hivyo alionya kwamba; “ Maandamani yangali chaguo letu iwapo watakosa kuonyesha nia njema katika mazungumzo. Tutarudi kwa watu waamue jinsi tutasonga mbele.”

Alipokubali ombi la Rais Ruto la kusitisha maandamano na kupatia nafasi mazungumzo ya maridhiano, Bw Odinga alisisitiza kuwa Azimio itaudi mitaani iwapo matakwa yao hayatazingatiwa.

Muungano huo wa upinzani sasa unapanga kuandaa mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi Jumapili ijayo, katika kile unachotaja kama kuelezea wafuasi wake hali ilivyo na hatua utakaochukua kufuatia kusitishwa kwa maandamano.

“Kusudi la vikao na mikutano ya umma ni kutuwezesha kuelezea watu hali ilivyo na hatua tutakazochukua kufuatia kusitishwa kwa maandamano,” alisema Bw Oparanya.

Mkutano wa Jumapili utafanyika katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji ambako Azimio ilianzisha mabaraza ya umma yaliyotangulia maandamano.

Bw Oparanya alisema kwamba, Azimio haitabadilisha nia kuhusu masuala inayotaka yashughulikiwe ikiwemo kupunguzwa kwa gharama ya maisha kupitia kurudishwa kwa ruzuku za mafuta, mahindi na stima.

Kenya Kwanza imekataa pendekezo hili huku Rais Ruto akisema ruzuku hizo zilitumiwa na utawala wa Jubilee kupora pesa.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, mmoja wa wawakilishi wa Azimio katika mazungumzo bungeni alisema, msimamo wa Rais Ruto na Kenya Kwanza unaashiria mchakato huo hautafaulu.

“Kusisitiza mchakato wa bunge ni hatari, kuhusishwa kwa Mheshimiwa Keynan (Adan) katika kikosi chake (Ruto) ni nia mbaya kabisa na dharau, kukataa kuzungumzia chochote kupunguza bei ya unga ni kuvunja mazungumzo,” Bw Sifuna, mmoja wa wandani wa Bw Odinga alisema.

  • Tags

You can share this post!

Kiambu yatenga Sh5.7 bilioni kwa usambazaji wa maji safi

Ndindi Nyoro aahidi bajeti ya 2023/24 itaweka zingatio kwa...

T L