• Nairobi
  • Last Updated May 29th, 2023 9:37 PM
Punda amechoka, Raila aambia Ruto

Punda amechoka, Raila aambia Ruto

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, jana Jumamosi alimwambia Rais William Ruto peupe kuwa Wakenya wengi wamelemewa na gharama ya juu ya maisha hivi kwamba, hawawezi kuvumia tena.

Akihutubu Jumamosi wakati wa mazishi ya mkewe Shujaa Dedan Kimathi, Bi Mukami Kimathi, katika eneo la Njabini, Kaunti ya Nyandarua, Bw Odinga alimwambia Rais Ruto kuwa washirika wake hawamwambii ukweli kuwa Wakenya wengi wanaumia kutokana na gharama ya juu ya maisha kufuatia baadhi ya sera za kiuchumi ambazo zimeanza kutekelezwa na serikali yake.

“Tungetaka Wakenya kuendelea kuieleza serikali ukweli. Sisi kama Azimio si wendawazimu, tunaweza tu kuelewana. Gharama ya maisha imepanda. Usiwaletee Wakenya ushuru mwingi sana. Watu hawakwambii ukweli kuwa punda amechoka,” akasema Bw Odinga.

Jana Jumamosi ilikuwa mara ya kwanza viongozi hao wawili kukutana hadharani tangu uchaguzi mkuu wa Agosti 2022 na Bw Odinga kuanza kuongoza maandamano dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Azimio imekuwa ikishikilia kuwa serikali ya Rais Ruto imeshindwa kupunguza gharama ya maisha licha ya kutangaza mikakati mingi ya kuwasaidia Wakenya kuhimii makali ya gharama hiyo ya juu.

Hata hivyo, Rais Ruto alijitetea dhidi ya lawama za Bw Odinga na badala yake akalaumu handisheki kati ya kiongozi huyo na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwa kuchangia kupanda kwa gharama ya maisha nchini.

“Ni kweli kuwa gharama ya maisha iko juu. Lakini, si hata nikichaguliwa gharama ya maisha ilikuwa juu? Unga ulikuwa ukiuzwa kwa Sh230. Saa hii hali imeimarika, kwani angaa bei yake imeshuka hadi Sh170. Nimetafuta mahindi na kuleta. Angaa kuna matumaini itaendelea kupungua kwa kuwa wakulima wamerejea mashambani,” akasema Rais Ruto.

Akaendelea: “Kosa mlilofanya (Uhuru na Raila) ni kuelekeza pesa kwa wasagaji badala ya kuwasaidia wakulima kuimarisha uzalishaji. Hiyo ndiyo sababu nimeelekeza juhudi zangu katika kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji. Hiyo ndiyo njia ya kupunguza gharama ya maisha.”

Rais Ruto pia alijitetea dhidi ya madai ya kuwaongezea ushuru Wakenya, badala yake akisema amepunguza ushuru kwa karibu sehemu 20 kwenye bajeti ya sasa.

“Pengine kuna watu hawakwambii ukweli (Raila). Nimeondoa karibu Sh500 bilioni za madeni katika bajeti ya mwaka wa kifedha 2023/2024 ili kupunguza mzigo kwa Wakenya. Huwezi kunishinda kuendeleza masuala ya uchumi,” akasema Rais Ruto.

Kauli ya viongozi hao wawili inajiri huku serikali ikiendelea kuelekezewa lawama na Wakenya wengi kutokana na mpango wake wa kuwatoza watumishi wa umma asilimia tatu ya mishahara yao kama ada maalumu ya ujenzi wa nyumba.

Wiki iliyopita, Askofu Jackson Ole Sapit wa Kanisa la Kianglikana Kenya (ACK) alikosoa mipango ya kuongeza ushuru iliyopendekezwa katika Mswada wa Fedha 2023 na serikali, akiitaja kama njia ya kuwaongezea Wakenya mzigo wa ushuru.

  • Tags

You can share this post!

Manchester City kunusia taji leo Jumapili ikikomoa Everton

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuoka keki aina ya Red Velvet

T L