• Nairobi
  • Last Updated December 6th, 2023 9:00 PM
Raila akanusha kuna handisheki na Ruto

Raila akanusha kuna handisheki na Ruto

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga, amepuuzilia mbali uvumi kwamba, anapanga kufanya handisheki na Rais William Ruto, akisema kukutana kwake mara tatu na kiongozi wa taifa ndani ya wiki moja ‘kulikuwa sadfa tu’.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana Jumanne, Bw Odinga alikariri kuwa muungano wa upinzani katu hauna sababu ya kuridhiana kisiasa na serikali ya Kenya Kwanza aliyoisuta kuwa dhalimu.

“Ni kweli kwamba, nilikutana na William Ruto katika mazishi ya mpiganiaji uhuru shujaa Mama Mukami Kimathi kule Njambini, Nyandarua na tukasalimiana kwa mikono. Nilihudhuria mazishi hayo kutokana na uhusiano wangu wa karibu na Mama Mukami licha ya viongozi wengine wa Kenya Kwanza kututisha kwamba tusifike huko,” akasema.

“Baadaye kutoka Njambini, nilifululiza hadi katika uwanja wa michezo wa kimataifa wa Kasarani kwa sababu nilikuwa nimealikwa katika mashindano ya riadha ya Kipkeino Classic. Nilipofika huko, nilimpata Bw Ruto na tukaketi pamoja kufuatilia mashindano hayo. Sikupanga kukutana naye,” Bw Odinga akaongeza.

Aidha, kiongozi huyo wa Azimio alielezea kuwa, mnamo Jumamosi aliamua kwenda kutizama mchuano wa kandanda kati ya klabu za Gor Mahia na AFC Leopards, almaarufu “Mashemeji Derby” katika uwanja wa michezo wa Nyayo, Nairobi.

“Nilienda huku kama mdhamini wa klabu ya Gor Mahia. Lakini nilipokaribia mzunguko wa barabara kuelekea uwanja wa Nyayo, niliona msongamano wa magari. Nilipouliza, nikaambiwa Ruto ndiye alikuwa akielekea uwanjani Nyayo,” Bw Odinga.

Waziri huyo Mkuu wa zamani alisema, kwa mara nyingine alikutana na Rais Ruto na wakaketi wakikaribiana.

“Wakati wa mapumziko, tulikwenda pamoja katika chumba cha kubadilisha mavazi na picha nyingi zikapigwa. Hata hivyo, hatukusalimiana,” Bw Odinga akasema.

Alikariri Bw Odinga: “Ningetaka kurudia kwamba hatutaki handisheki na serikali hii ambayo kulingana na sisi si halali. Ningependa Gachagua aelewe msimamo huu.”

Kwa mara si moja, Naibu Rais Bw Rigathi Gachagua amekuwa akidai kuwa Bw Odinga amekuwa akitoa vitisho kwa serikali ya Kenya Kwanza kupitia maandamano yenye fujo kusudi aalikwe kujiunga na serikali kupitia handisheki.

Hata hivyo, Bw Odinga amekuwa akishikilia kuwa amekuwa akiitisha maandamano kuishinikiza serikali ishughulikie changamoto zinazowakabili wa Wakenya wala sio kwa lengo la kujiunga nayo.

“Kenya Kwanza imeendelea kudai kuwa kile ambacho tunasaka ni handisheki. Tunapinga kabisa uvumi huo usio na msingi kwamba, maandamano yetu yanayolenga kuimarisha maisha ya Wakenya ni kisingizio tu cha kutaka handisheki. Hii ni matusi kwa wafuasi wetu na Wakenya kwa ujumla. Hatuwezi kushiriki katika handisheki na serikali isiyo halali,” Bw Odinga akasema jijini Nairobi mwezi Aprili.

Lakini hatua ya Bw Odinga kukutana kwa mara ya kwanza hadharani, Jumamosi na Jumapili wiki jana ilipelekea Wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii kubashiri kuwa huenda wawili hao wanapanga kushirikiana kisiasa.

Wakiongea katika mazishi ya Mama Mukami, Rais Ruto na Bw Odinga walisema wanajuana vizuri zaidi kwani wamewahi kufanyakazi pamoja katika serikali za Hayati Daniel Moi na Mwai Kibaki.

“Naona handisheki nyingine ikinukia hapa. Bila shaka atakayepoteza hapa kisiasa ni Riggy Gi (Rigathi Gachagua),” Abel Mainye akasema kupitia Twitter.

Hata hivyo, jana Jumanne Bw Odinga aliahidi kuitisha maandamano mengine ikiwa serikali ya Rais Ruto italazimisha kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2023.

“Tunawaita Wakenya kujitokeza wapiganie haki yao ikiwa serikali itafanikisha mswada wa Fedha kupita Bungeni. Kabla ya hapo, natoa wito kwa Wakenya watoe maoni ya kupinga mswada huo utakapowasilishwa mbele yao. Aidha, tumewaamuru wabunge wetu kuupinga mswada huu unawaongezea Wakenya mzigo wa ushuru. Punda amechoka!” akafoka.

  • Tags

You can share this post!

UEFA: Manchester City na Real Madrid kumaliza udhia leo...

Ishara na dalili za upungufu wa vitamini C mwilini

T L