• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Raila alaani fujo huku wafuasi wa wagombeaji ugavana wakikabiliana

Raila alaani fujo huku wafuasi wa wagombeaji ugavana wakikabiliana

NA PIUS MAUNDU

KINARA wa ODM, Raila Odinga amelaani vurugu iliyotokea Kaunti ya Machakos.

Akizungumza Ijumaa katika hafla ya kampeni, Bw Odinga alisema kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka hakumjulisha ajenda ya mkutano huo.

“Tukio lilitokea Machakos ni la aibu. Kulizuka vurugu tulipofika kwenye mkutano huo. Kwanza hatukujua ikiwa tulikuwa kanisani au kwenye kampeni. Bw Kalonzo hakunieleza ajenda ya mkutano huo,” akasema Bw Odinga.

Kadhalika, mwaniaji huyo wa kiti cha urais alisema alijulishwa kuwa wangekutana na viongozi wa kidini ila walipofika katika eneo hilo, kukatokea vita.

“Sikujua tunahudhuria maombi ya wawaniaji wa kiti cha ugavana Machakos,” akasema Bw Odinga.

Kiongozi huyo alisema kuwa anapeperusha bendera ya muungano wa Azimio na hafai kuonekana kuwa anaunga mkono chama kimoja katika muungano huo.

“Mimi na Bi Martha tunapeperusha bendera ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya. Azimio una vyama 26. Muungano huo una wawaniaji mbalimbali. Kwa hivyo, sifai kuonekana kuegemea chama fulani,” akasema Bw Odinga.

Wafuasi wa waaniaji wawili wa kiti cha ugavana Machakos walianza kushambuliana huku Bw Odinga na wandani wake wakijaribu kuwatuliza.

Hata hivyo, Bw Odinga aliyeandamana na mwaniaji mwenza wake, Martha Karua, mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi, Bw Musyoka, bosi wa Cotu, Fransis Atwoli, Charity Ngilu na Kivutha Kibwana walishindwa kuwatuliza wafuasi hao.

Wafuasi wa mwaniaji wa kiti cha ugavana kwa tikiti ya Wiper walianza kushambuliana na wafuasi wa Bw Waita kutoka jukwaa kuu la hafla ya maombi.

Bw Waita anagombea kiti hicho kwa tikiti ya Chama Cha Uzalendo.

Wafuasi wa Wavinya Ndeti walimtimua Bw Waita kwenye hafla hiyo ya maombi ambayo iliandaliwa na baadhi ya wachungaji katika eneo hilo kwa nia ya kumbariki Bi Ndeti.

You can share this post!

Karua aahidi ‘kuwakomboa’ wakazi Mlimani

Naomba unikome, Ruto afokea Uhuru mkutanoni

T L