• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Raila alilia ngome yake isimwangushe uchaguzini Agosti

Raila alilia ngome yake isimwangushe uchaguzini Agosti

NA GEORGE ODIWUOR

MGOMBEA urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya amesihi wakazi katika ngome yake ya Nyanza wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili wamsaidie kushinda urais.

Bw Odinga aliwaambia wakazi hao kwamba wakimchagua kuwa rais watafurahia matunda ya uongozi wake kwa kupata huduma za serikali.

Akizungumza katika shule ya sekondari ya Agoro Sare Kaunti ya Homa Bay kwenye mkutano wa kampeni, Bw Odinga aliwarai wakazi wa kaunti za Migori, Kisumu, Siaya na Homa Bay kuimarisha hulka yao ya upigaji kura ili wamsaidie kushinda urais.

Ingawa Bw Odinga anafurahia umaarufu eneo la ziwani, tabia ya wakazi kutoka kaunti hizo kutojitokeza kwa wingi kupiga kura imekuwa kisiki kwake kushinda urais katika chaguzi za awali.

Huku uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ukikaribia, viongozi wameanza kutoa elimu ya upigaji kura kwa wakazi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kumsaidia Bw Odinga kushinda.

Kiongozi huyo wa ODM anataka wakazi kubadilisha mtazamo wao kuhusu uchaguzi kwa kulenga manufaa ya rais kutoka eneo lao.

Iwapo watadumisha desturi yao ya kutojitokeza kwa wingi kupiga kura, hawatakuwa na thamani kwa Azimio kwa kuwa hii inaweza kuwa mara ya mwisho ya waziri mkuu huyo wa zamani kugombea urais.

Bw Odinga alisema wakazi wanafaa kuonyesha mabadiliko katika uchaguzi mkuu ujao na akawataka wamakinike kwa kuhimizana ili wampigie kura kwa asilimia 100 ili wafurahie matunda ya serikali akiwa rais.

“Mumeona kwamba eneo hili limenufaika kwa muda mfupi ambao serikali imekuwa upande wetu( akimaanisha handisheki yake na Rais Kenyatta). Hebu fikirieni aina ya maendeleo mtakayopata nikiwa rais,” aliwaambia wakazi.

Alisema kwamba jamii zingine zimemweleza kwamba zinamuunga mkono na akahimiza wakazi wa ngome yake kuungana na wale wa maeneo mengine kumsaidia kuingia ikulu.

“Jamii zingine zimeniomba niwaambie kwamba ziko tayari kwa mabadiliko na zimewauliza pia kuyakumbatia. Ninawaomba muwe tayari kunipigia kura,” alirai Bw Odinga.

“Kenya imeamua inayotaka kuwa kiongozi wake. Kwa hivyo mnapaswa kuhakikisha ushindi hauponyoki,” aliongeza.

Wakati huo huo, Bw Odinga alimtaka mpinzani wake mkuu Naibu Rais William Ruto kujiandaa kukubali kushindwa.

“Nitamshinda. Huwa anashinda akiniita mganga na jamaa wa vitendawili. Anafaa kufahamu kuwa nchi imebadilika,” akasema Bw Odinga.

Gavana wa Kisii, Bw James Ongwae alidai kwamba wakazi wa Nyanza hawajawahi kuwa makini kutwaa urais katika chaguzi zilizopita na akawataka kubadilika katika uchaguzi mkuu ujao.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wabunge Gladys Wanga (Mwakilishi wa Kike) Peter Kaluma (Homa Bay Town), Lilian Gogo (Rangwe), Adipo Okuome (Karachuonyo), Ong’ondo Were (Kasipul), Eve Obara (Kabondo Kasipul), Millie Odhiambo (Suba Kaskazini) na seneta Moses Kajwang.

You can share this post!

PSG wamsajili kiungo Vitinha kutoka FC Porto ya Ureno

Kalonzo asisitiza lazima Sonko awe debeni Agosti 9

T L