• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Raila arudi na joto la maandamano

Raila arudi na joto la maandamano

CECIL ODONGO Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa Azimio, Raila Odinga leo anatarajiwa kutoa mwelekeo mpya kuhusu mkondo wa maandamano pindi baada ya kuwasili nchini kutoka Dubai.

Bw Odinga atatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) leo Ijumaa mchana ambapo atapokelewa na viongozi na wafuasi wake kisha aelekee uwanja wa Kamkunji mtaani Kibera, Nairobi kwa mkutano wa hadhara.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Bw Odinga jana Alhamisi alisema ‘tunarejea kwa wananchi’ – ishara kwamba kinara huyo wa Azimio huenda akatangaza kurejewa kwa maandamano ya kila Jumatatu na Alhamisi.

Kulingana na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, Bw Odinga anatarajiwa kutoa tangazo muhimu kuhusiana na maandamano ambayo yalisitishwa kwa muda kupisha mashauriano na serikali.

“Mkutano wa Kibra kesho (leo Ijumaa) utakuwa maandalizi ya maandamano yatakayofanyika Jumanne, Mei 2, 2023. Viongozi wa Azimio watatangaza mipango yetu ya siku zijazo katika kikao chenyewe,” Bw Wandayi akaambia Taifa Leo.

Bw Wandayi aliwataka wafuasi wa Azimio kujitokeza kwa wingi kumlaki Bw Odinga uwanjani JKIA kisha msafara huo unaotarajiwa kuwa mkubwa uelekee uwanja wa Kamkunji.

Mkutano wa leo utakuwa wa tatu tangu Bw Odinga kukubali kufanya mazungumzo na serikali kwa lengo la kusitisha maandamano ya Azimio.

Vinara wa Azimio wanataka mitambo ya kuhifadhi matokeo ya kura za urais ifunguliwe ili kubaini ‘mshindi halali’ wa uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Upinzani pia unataka serikali ipunguze bei ya unga wa mahindi hadi chini ya Sh100 kwa kila kilo mbili na Rais Ruto akome ‘kununua’ wabunge wa Azimio kuhamia upande wa Kenya Kwanza kati ya matakwa mengineyo.

Mazungumzo tayari yamesambaratika baada ya upande wa Azimio kutaka mbunge wa Eldas Adan Keynan (Jubilee) asiwakilishe Kenya Kwanza.

Kambi ya Bw Odinga imeshikilia kuwa Bw Keynan ni mbunge wa chama cha Jubilee ambacho kimo ndani ya muungano wa Azimio.

Kabla ya kuondoka nchini wiki iliyopita, Bw Odinga alifanya mkutano katika Kaunti ya Murang’a na kisha kuhutubia wakazi katika maeneo mbalimbali.

Bw Odinga aliongoza mkutano mwingine wa Azimio katika uwanja wa Kamkunji mtaani Shauri Moyo, Nairobi.

Jana, mbunge wa Kibra Mwalimu Peter Orero alisema mipango yote ya kumkaribisha Bw Odinga katika eneobunge hilo imekamilika huku akisisitiza kuwa wakazi anaowawakilisha wanaunga mkondo kurejelewa kwa maandamano wiki ijayo.

“Inajulikana kuwa siasa za Raila zilianzia hapa Kibra na kauli yake inaheshimika sana hapa nyumbani. Tuko tayari,” akasema Bw Orero kwenye mahojiano na Taifa.

Aliendelea: “Wakazi wa Kibra ni wapenda amani na polisi hawafai kutumiwa kuvuruga mkutano wa leo au maandamano ambayo tutakuwa tukirejelea Jumanne.

Kaunti hazina pesa, watumishi wa umma wanacheleweshewa mishahara, gharama ya maisha imepanda.

Je, serikali inatarajia upinzani unyamaze tu mambo yakienda mrama? “akauliza. Bw Odinga alihudumu kama mbunge wa Lang’ata (enzi hizo ikijumuisha Kibera na Lang’ata) kuanzia 1992 hadi 2013.

Wanasiasa pia wanatarajiwa watatumia mkutano wa leo kumshambulia mbunge wa eneobunge jirani la Lang’ata Felix Oduor maarufu kama Jalang’o ambaye licha ya kuchaguliwa na ODM, ameanza ushirikiano na mrengo wa serikali akisema anatafutia wakazi wake miradi ya maendeleo.

Kulingana na mchanganuzi wa Masuala ya kisiasa Martin Andati, masuala ambayo yalifanya upinzani ukumbatie maandamano bado hayajatatuliwa ndiposa huenda yakashika kasi kuliko jinsi ilivyokuwa kabla ya kusitishwa.

Bw Andati anasema kuwa kujitokeza kwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuzuia kutwaliwa kwa makao ya Jubilee na wandani wake kama David Murathe ambao wamekuwa kimya kujitokeza, ni ishara tosha kuwa mara hii makabiliano yatachacha hasa iwapo Rais Mstaafu mwenyewe ataamua kujitosa kwenye maandamano

“Ile kamati iliyoundwa na upinzani na serikali haijafanya chochote, gharama ya maisha nayo bado yapo juu, watumishi wa umma wanacheleweshewa mishahara, watu wana njaa na huwezi kuwafungia nyumbani. Hizi ni ishara kuwa serikali ina kibarua kukabili maandamano ya upinzani,” akasema Bw Andati.

“Rais Kenyatta kuonekana kurejea kwa siasa kutaumiza serikali zaidi kwa sababu akiamua kuongoza maandamano na Bw Odinga, basi utawala wa sasa utasukumwa pembeni kabisa kuhusu kukabali changamoto za nchi,” akaongeza.

Bw Murathe, aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho ni kati ya viongozi ambao wameahidi kujitokeza na kupiga jeki maandamano yanayoanza Jumanne na wanatarajiwa kumlaki Bw Odinga leo Ijumaa.

  • Tags

You can share this post!

Uhifadhi wa Mto Thika walenga kuhakikisha viwango vya maji...

‘Pasta’ Ezekiel alipanga kuenda TZ aliponaswa...

T L