• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Raila atua Uingereza kuosha tope la Ruto

Raila atua Uingereza kuosha tope la Ruto

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM na mgombea urais wa muungano wa Azimio La Umoja Raila Odinga, anazuru Uingereza katika ziara inayochukuliwa kama ya kujiosha tope aliyopakwa na mpinzani wake Naibu Rais William Ruto.

Dkt Ruto alizuru Uingereza wiki jana kutoka Amerika alikotangulia katika ziara iliyochukua siku 10.

Akizungumza katika Chatham House Uingereza, Dkt Ruto alimlaumu Bw Odinga kwa kuvuruga ajenda za serikali ya Jubilee aliporidhiana na Rais Uhuru Kenyatta Machi 9, 2018.

Alisema kwamba Bw Odinga aliporomosha Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee na badala yake akaanzisha Mpango wa Maridhiano (BBI ) ili kuunda nyadhifa za uongozi.

“Handisheki ilibadilika kuwa njama, haikuwa na nia nzuri. Hakukuwa na umoja, hakukuwa na maridhiano. Handisheki iliporomosha chama tawala cha Jubilee na muungano wa upinzani wa NASA, iliharibu ajenda ya serikali. Umoja tunaotaja ni umoja wa viongozi,” Dkt Ruto alidai.

Bw Odinga anayeandamana na aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, Seneta wa Siaya James Orengo, Magavana Hassan Joho (Mombasa), Charity Ngilu (Kitui), Lee Kinyanjui (Nakuru) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed pia anatarajiwa kuhutubu katika Chatham House na kukutana na Wakenya wanaoishi Uingereza alivyofanya Dkt Ruto.

Katibu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli na baadhi ya wana mikakati wa Azimio La Umoja pia wako katika ziara hiyo inayojiri siku moja baada ya Odinga kutangazwa rasmu mgombea urais wa muungano huo.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na afisa yake, Bw Odinga leo Jumanne atakutana na Waziri wa Majeshi wa Uingereza James Heappey kisha kesho akutane na waziri wa masuala ya Asia Kusini, Afrika Kaskazini na Jumuiya ya Madola Lord Tarif Ahmad kabla ya kuhutubu katika Chattam House. Kenya ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola.

“Katika hafla hii, Raila Odinga ataeleza maono yake kuhusu Kenya na Afrika katika ulimwengu usiotabirika, na atafafanua lengo la kisiasa la umoja linalowakilishwa na muungano wake wa Azimio La Umoja,” Chatham House ilisema kwenye taarifa.

Mnamo Alhamisi, Bw Odinga atakutana na Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby katika Lambeth Palace kabla ya kukutana na Wakenya wanaoishi Uingereza katika hoteli ya Kessington Inn.

Katika ziara yake Uingereza wiki jana, Dkt Ruto pia alikutana na Askofu Mkuu Welby kwa mazungumzo kuhusu hali ya siasa za Kenya kabla na baada ya uchaguzi na haja ya kudumisha amani na umoja.

Dkt Ruto aliyetolewa jasho kwa maswali makali na Wakenya wanaoishi nchini humo alilimbikizia lawama Bw Odinga akisema alimpotosha Rais Kenyatta katika muhula wa pili wa utawala wa Jubilee.

Alidai kwamba ni Bw Odinga aliyefanya atengwe serikalini na majukumu yake kukabidhiwa watu walioshindwa kuyatekeleza.

Katika ziara yake ya siku nne, Bw Odinga anatazamiwa kujibu madai hayo.

Kiongozi huyo wa ODM, pia atakutana na waziri wa biashara wa Uingereza Theo Clerk.

You can share this post!

Walimu 200,000 wapewa mafunzo ya kutekeleza CBC

Yafichuka Sonko alilindwa na polisi 33 ziarani

T L