• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Raila hatarini kusalia pweke katika upinzani

Raila hatarini kusalia pweke katika upinzani

NA WANDISHI WETU

MADAI ya usaliti na mikakati ya Rais William Ruto kusaka umaarufu katika ngome za upinzani vinatishia kumwacha kinara wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga mpweke kisiasa.

Huku vyama tanzu vya Azimio vikilalamikia kufinywa na chama cha ODM chini ya uongozi wa Bw Odinga, Rais Ruto pia amekuwa akijaribu kuvuta baadhi ya vigogo wa muungano huo wa upinzani upande wake.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio, Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta amekuwa kimya tangu alipostaafu miezi miwili iliyopita – hali inayosababisha wadadisi wa masuala ya kisiasa kuamini kuwa amejitenga na upinzani.

Hatua ya baadhi ya viongozi wa Jubilee kutishia kujiondoa Azimio pia imeibua maswali kuhusu hatima ya muunganano wa Azimio unaojumuisha vyama 26.

Alhamisi, wabunge wanane wa Jubilee walishutumu washirika wao wa ODM wakiwataja kuwa ‘watapeli na walaghai wa kisiasa’.

Chama hicho kinachoongozwa na Rais Mstaafu Kenyatta, kinashutumu ODM kwa ‘kunyakua’ nyadhifa nyingi katika Bunge la Kitaifa na Seneti na kudhalilisha vyama vingine vya Azimio.

Wabunge wa Jubilee Adan Keynan (Eldas), Sabina Chege (Maalumu), Abdi Shurie (Balambala), Fatuma Dullo (Seneta wa Isiolo), Abdi Haji (Seneta wa Garissa), Amos Mwago (Starehe) na Sarah Korere (Laikipia Kaskazini) walitishia kujiondoa Azimio huku wakidai ODM waliwapokonya nafasi moja katika Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Wabunge hao walitishia kujiunga na muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu aliambia Taifa Jumapili kuwa, hajapokea barua kutoka kwa Jubilee ya kutaka kujiondoa Azimio.

“Kufikia sasa kuna vyama vinne pekee ambavyo vimewasilisha barua ya kujiondoa Azimio. Vyama hivyo ni Maendeleo Chap Chap, Pamoja African Alliance (PAA), Movement for Democracy and Growth (MDG) na United Democratic Movement (UDM),” akasema Bi Nderitu.

Siku chache kabla ya kustaafu, Kenyatta alionya viongozi wa upinzani kuwa watajuta iwapo hawataungana na kuunda upinzani thabiti wa kupambana na serikali ya Rais Ruto.

Kenyatta amekuwa akitekeleza majukumu yake kama mpatanishi wa pande zinazopigana nchini Ethiopia.

Mara baada ya kuapishwa, Rais Ruto aliteua Kenyatta kuwa balozi wa amani katika nchi za Upembe wa Afrika na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa jimbo la Tigray nchini humo walipokubali kutia saini mkataba wa amani nchini Ethiopia wiki iliyopita, Rais Ruto alikuwa wa kwanza kumpongeza Rais Mstaafu Kenyatta kwa kuongoza mazungumzo hayo ya amani.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanabashiri kuwa, uhusiano baina ya Rais Ruto na mtangulizi wake, Rais Mstaafu Kenyatta, unaonekana kurejea licha ya wawili hao kutofautiana vikali wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Iwapo chama cha Jubilee kitajiondoa Azimio, muungano huo huenda ukaishiwa na nguvu ya kukabili serikali ya Kenya Kwanza. Wandani wa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka wakiongozwa na magavana Wavinya Ndeti (Machakos) na Mutula Kilonzo Junior (Makueni) wamekuwa wakimshinikiza kugura Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza.

Bw Mutula ametishia kuongoza jamii ya Wakamba kuingia serikalini iwapo Bw Musyoka ataendelea kujikokota.
Rais Ruto tayari amesema yuko tayari kumpokea Bw Musyoka kwa mikono miwili endapo ataondoka Azimio.

Iwapo Bw Musyoka atagura Azimio, Bw Odinga atasalia mpweke na muungano huo utakuwa katika hatari ya kuvunjwa.
Rais Ruto amekuwa akilenga wanasiasa wa Azimio waliopoteza viti katika uchaguzi wa Agosti 9 na magavana walioondoka afisini baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.

Tayari Kenya Kwanza wamenasa aliyekwua gavana wa Kisii, James Ongwae.

Katika hatua ya kufifisha Azimio zaidi, Rais Ruto pia ameanza kulenga viongozi waliochaguliwa kupitia vyama vya Azimio.

Ijumaa, Rais Ruto alikutana na wabunge wa Azimio kutoka Magharibi; Bernard Shinali (Ikolomani), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Titus Khamala (Lurambi) katika Ikulu ya Nairobi.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa ambaye alichaguliwa kupitia tiketi ya ODM, pia alikutana na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi jijini Nairobi.

Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula tayari ameelezea azma yake ya kushirikiana na Rais Ruto.

Huku Bw Odinga akikabiliwa na hatari ya kusalia mpweke, Katibu Mkuu wa Azimio Junet Mohamed anashikilia kuwa mipango inaendelea ya kuunda kikosi imara cha upinzani kitakachopambana na serikali ya Kenya Kwanza. Kwa mujibu wa Bw Mohamed, muungano wa Azimio la Umoja utaanza rasmi mapambano dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza Januari 2023.

“Tunajiandaa kuunda upinzani wenye nguvu utakaobandua Rais Ruto mamlakani 2027,” anasema Bw Mohamed.

Kulingana na mpango huo, muungano wa Azimio utaweka mawaziri 22 wa ‘kivuli’ kukabili mawaziri wa Rais Ruto.

Baraza la Mawaziri wa Azimio lilifaa kutangazwa mwezi Oktoba lakini kufikia sasa halijatajwa.

Awali, Bw Musyoka alikuwa amedokeza kuwa kiongozi wa Azimio Raila Odinga angetangaza baraza la mawaziri wa upinzani mara baada ya kurejea kutoka ziarani nchini India mwezi Oktoba.

Kwa mujibu wa Bw Mohamed, mawaziri hao wa Azimio watatangazwa Januari, mwaka ujao. Vigogo wa Azimio pia wanalenga kutumia mamilioni kuajiri wataalamu watakaokuwa wakifanya utafiti na kisha kuwapa ripoti mawaziri wa kivuli.

Mawaziri hao wa kivuli watatumia ripoti hiyo kukosoa na kufichua maovu ndani ya serikali ya Kenya Kwanza. Wazo ni kuwa na kundi lenye nguvu na ufahamu ambalo litakuwa likijibu na kukosoa serikali kitaalamu na kwa hali ya kufahamu- kwa kutumia takwimu sahihi na taarifa husika za sera.

Mbinu hii inanuiwa kutia nguvu ofisi za mawaziri kivuli ili wasifanywe kuwa wasemaji tu wanaohusika na malumbano ya kisiasa. Tatizo la mbinu kama hii ni kwamba wafanyakazi zaidi watahitajika.

Kuajiriwa kwa watalaamu kama hao na pia ofisi ya kufanyia kazi na gharama nyingine za shughuli zao kutahitaji ufadhili.
Changamoto hiyo ndio imesababisha vigogo wa Azimio kuchelewa kuunda kikosi cha kukosoa serikali ya Ruto.

Utata kuhusu hatima ya kisiasa ya Bw Odinga pia umesababisha mpango wa kuunda kikosi cha kukosoa serikali kujikokota. Bw Odinga amefichua kuwa atatangaza hatima yake ya kisiasa baadaye hali ambayo imewaacha Bw Musyoka na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua katika njiapanda.

Bw Odinga amesisitiza kuwa kushiriki kwake katika siasa baada ya 2022 kunatokana na haja ya kulinda mafanikio ya demokrasia ambayo kufikia sasa yamepatikana.

Waziri mkuu huyo wa zamani anahofia kwamba akistaafu siasa, mafanikio ambayo yamepatikana kufikia sasa yanaweza kuporomoka chini ya utawala wa Rais Ruto. Bw Musyoka amekuwa akizunguka katika ngome ya Bw Odinga – haswa eneo la Nyanza – huku akijiandaa kuwania urais 2027.

Bw Mohammed anaeleza kwamba kila kitu kitakuwa sawa, ikiwemo uongozi wa muungano huo, kufikia wakati muundo wa upinzani utazinduliwa mapema mwaka ujao 2023.

Ripoti za LEONARD ONYANGO, OSCAR OBONYO na SHABAN MAKOKHA

You can share this post!

SHANGAZI SIZARINA: Mbona kila ninayemtongoza anikataa?

Wanafunzi wa chuo cha ufundi Thika kuhusika moja kwa moja...

T L