• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 2:18 PM
Raila na Ruto bega kwa bega

Raila na Ruto bega kwa bega

Na WINNIE ONYANDO

KINARA wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto kufikia sasa wako bega kwa bega kwenye kinyang’anyiro cha Urais mwaka ujao 2022.

Kura ya maoni ya kampuni ya Infotrak iliyotolewa Jumatatu inaonyesha kuwa, kama uchaguzi mkuu ungeandaliwa leo, hakuna ambaye angeingia ikulu.

Katiba inasema anayeshinda uchaguzi ni lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zitakazopigwa.

Ingawa Dkt Ruto alianza kampeni punde tu Bw Odinga aliposalimiana na Rais Uhuru Kenyatta, Machi 2018, kwa sasa yuko nyuma ya Kinara huyo wa ODM kwa asilimia moja.

Utafiti huo unaonyesha Bw Odinga akiwa na asilimia 33 ya kura, huku Dkt Ruto akipata asilimia 32.

Utafiti huo uliofanywa kati ya Disemba 17 na 21, uliwashirikisha watu 1,600 kutoka maeneo yote manane ya nchi, na kuwakilisha idadi ya wapigakura 19.6 milioni.

“Kulingana na utafiti uliofanywa katika maeneo manane ya wapiga kura, kuna farasi wawili katika kinyang’anyiro cha urais. Kuna ushindani mkubwa kati ya wawili hao,” inasema ripoti hiyo iliyosomwa na Mkurugenzi wa Infotrak, Bi Angela Ambitho.

Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakikosoana kwenye majukwaa ya kisiasa kuhusu sera za kiuchumi kati ya maswala mengine.

Wadadisi wa maswala ya siasa wanasema, huenda mambo yakabadilika, pale Rais Uhuru Kenyatta atakapoanza kumpigia debe mwaniaji anayemuunga mkono.

Rais Kenyatta amenukuliwa zaidi ya mara moja, akisema wakati wa siasa bado, na kwamba utakapofika, ataonyesha mwelekeo wa kule angetaka Wakenya wapige kura.

Bw Odinga tayari ametangaza kuwania urais kupitia Azimio la Umoja, baada ya kuungwa mkono na wafuasi wake katika maeneo yote ya nchi, likiwemo kundi la Wakfu wa Mlima Kenya.

Kwa upande wake, Dkt Ruto anaendelea kujipendekeza kwa makundi ya kina mama, vijana na wafanyibiashara wadogo.

Ngome ya Dkt Ruto kulingana na ripoti hiyo ni maeneo ya Bonde la Ufa, Nairobi, Mashariki na Kati mwa Kenya.

Naye Bw Odinga anadhibiti kikamilifu maeneo ya Nyanza, Pwani, Magharibi na Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Utafiti huo unaonyesha kuwa, asilimia tatu ya wapigakura wangependa viongozi kama vile Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Martha Karua, William Kabogo, Mwangi wa Iria, Reuben Kigame na Abduba Dida wawe wagombea urais.

Hata hivyo, asilimia nne walisema hawatapiga kura, huku asilimia 7 wakikataa kutoa majibu na asilimia 21 wakisema hawana uamuzi kwa sasa.

Kutokana na kuwa farasi ni wawili, asilimia 52 ya waliohojiwa wanataka muungano wa One Kenya Alliance (OKA) uvunjwe, na viongozi wake waunge mkono mmoja kati ya wagombea wawili wakuu wa urais.

Asilimia 28 wanasema kuwa, muungano huo wa OKA haujulikani.

Kaskazini Mashariki inaongoza kwa asilimia 60 ya idadi ya watu wanaotaka muungano huo uvunjwe, ili viongozi hao wamuunge mmoja kati ya wagonbea hao wawili.

Wakazi wa maeneo ya Pwani wanapinga kuvunjwa kwa muungano huo, huku asilimia 37 ya wakazi wa Kati mwa Kenya, wakisema hawana ufahamu wa muungano huo.

“Asilimia 55 ya watu wanaotoka katika maeneo ya miji wanataka muungano huo wa OKA uvunjwe huku asilimia 31 ya maeneo ya mashambani wakiwa na msimamo huo,” inasema ripoti hiyo.

Kura hiyo ya maoni inasema nafasi pekee ya viongozi wa OKA kwa sasa ni ugombea mwenza.

Wapigakura wa Nairobi wanaongoza kwa idadi ya watu wanaompendelea Musalia Mudavadi kuwa mgombea mwenza wa mmoja kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga.

Asilimia 19 ya waliohojiwa wanamtaka Bw Musyoka kuwa mgombea mwenza, huku asilimia 11 wakimchagua Gideon Moi.

Ni asilimia 7 pekee waliotaja jina la Moses Wetang’ula.

Lakini karibu robo ya waliohojiwa, wanasema watatu hao hawafai kuwa wagombea wenza katika uchaguzi mkuu mwaka 2022.

You can share this post!

Huzuni mkazi wa Witeithie akiuawa na fisi

Wahamiaji 27 wafa maji Pwani ya Libya

T L