• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Raila na Ruto wachuuza asali chungu

Raila na Ruto wachuuza asali chungu

NA PAUL WAFULA

AHADI za kuimarisha uchumi zinazotolewa na Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga zitaongeza matatizo ya kiuchumi kwa wananchi.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya uchumi, mzigo wa kufadhili utimizaji wa ahadi hizo utabebeshwa wananchi ambao tayari wamelemewa na ugumu wa gharama ya maisha uliosababishwa na sera duni za kiuchumi za utawala wa Jubilee pamoja na janga la Covid-19.

Wanasema kuwa ahadi hizo hazina msingi, hivyo itawabidi Dkt Ruto na Bw Odinga wakichaguliwa kuongeza kodi ili kufadhili ahadi hizo, ama walazimike kuzipuuza ilivyofanyika kwa miradi ya awali ya Jubilee kama vile laptopu kwa wanafunzi, kubuniwa kwa nafasi zaidi za kazi na ujenzi wa viwanja vya michezo kote nchini.

Baada ya kukosa kutimiza ahadi hizo alizotoa kwa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, safari hii Dkt Ruto amebadilisha wimbo kwa kupigia debe kauli yake ya “Huslter Nation” anayodai itazingatia kuwainua kiuchumi watu wa tabaka la chini hasa vijana na akina mama.

Mwanasiasa huyo amekuwa akizunguka kila pembe ya nchi kwa ahadi kuwa atatenga Sh30 bilioni za kuwasaidia wafanyibiashara wadogo hasa vijana, mama mboga, bodaboda na walalahoi wengine.

Kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi anamkosoa Dkt Ruto akisema amekuwa sehemu ya matatizo ya kiuchumi yanayoumiza mamilioni ya Wakenya kwa sasa.

“Kabla ya kuanza kuwapa watu maskini pesa, lazima kwanza ujenge uchumi imara. Inasikitisha kuwa waliosababisha wananchi wengi kutumbukia katika umaskini sasa ndio wanaahidi kuwatoa kwenye mashimo hayo. Hauwezi ukategemea aliyekurusha shimoni akutoe humo kwa ahadi ya mapeni kidogo,” akasema Bw Mudavadi.

Bw Odinga naye anauza wazo kuwa atakuwa akipatia familia maskini zipatazo million mbili pesa taslimu Sh6,000 kila mwezi kwa kila moja. Hii ina maana serikali yake itahitaji Sh12 bilioni kila mwezi kwa ajili ya mradi huo.

Lakini mwanasiasa huyo anayejaribu kubisha hodi Ikulu kwa mara ya tano hajaeleza atakavyopata pesa hizo na jinsi atawatambua maskini hao milioni mbili ikizingatiwa kuna watu zaidi ya milioni 10 maskini hohehahe nchini.

Lakini akitetea ahadi hiyo, Bw Odinga anasema atapata pesa hizo kwa kulazimisha wizara na mashirika ya serikali kupunguza matumizi pamoja na kupiga vita ufisadi, ambapo pesa zitakazookolewa zitapewa maskini.

Lakini historia ya serikali za Kenya inaonyesha kuwa juhudi zote za kukata matumizi na kukabili ufisadi zimegonga mwamba.

Kwa mfano, Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiahidi kupunguza matumizi serikalini lakini hakuna juhudi zimefanyika kuafikia hilo.

Bw Odinga pia analenga kura za waendeshaji bodaboda wapatao milioni 2.4 kwa ahadi kuwa atabuni Hazina ya Kitaifa ya Boda Boda pamoja na kujenga kiwanda cha kutengeneza pikipiki hapa Kenya.

“Kiasi kikubwa cha pesa zinazokusanywa kama ushuru hapa Kenya zinatumika kulipa mishahara ya watumishi wa serikali na madeni. Watatoa wapi pesa za kufadhili ahadi zao?” ashangaa mwanauchumi Tony Watima kuhusu ahadi za Bw Odinga na Dkt Ruto.

Bw Watima anasema kuwa mbinu bora zaidi ya kuwakomboa maskini ni kuwasaidia kupata mikopo nafuu ili waweze kuwekeza kwenye biashara.

Mbinu hii ilitumiwa na serikali ya Mwai Kibaki, ambapo serikali ilipunguza ukopaji kutoka benki za humu nchini, hali iliyozilazimisha kukopesa wananchi wa kawaida kwa gharama nafuu.

Lakini Rais Kenyatta na Dkt Ruto walipochukua madaraka mnamo 2013 walitibua muundo huo wa kiuchumi kwa kukopa kila mara katika benki za nchini, hivyo kuwafungia nje wananchi wa kawaida.

“Tatizo kuu ni serikali kukopa kutoka kwa benki za hapa nchini. Hii imefungia nje wananchi kwani hawawezi kushindana na serikali kupata mikopo,” asema mwanauchumi huyo.

Bw Watima anasema hatua yoyote ya serikali kukopesha wananchi moja kwa moja haitafaulu kutokana na tatizo la wengi kushindwa kulipia mikopo hiyo, akishauri kuwa mbinu bora ya kuwasaidia maskini ni serikali kufadhili mikopo wanayopewa na benki.

Wataalamu wanasema kuwa ahadi za Dkt Ruto na Bw Odinga pia zinapuuza ukweli kuhusu hali mbovu ya uchumi wa Kenya hasa kutokana na deni kubwa linalodaiwa nchi. Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka huu Sh1.16 trilioni zitatumika kulipia madeni.

You can share this post!

Kunihusisha na ufisadi kutafeli kwani Wakenya si wajinga- ...

Agizo watumishi wakumbatie mavazi ya Kiafrika

T L