• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Raila na Ruto wararuana vikali Mlimani

Raila na Ruto wararuana vikali Mlimani

Na WAANDISHI WETU

NAIBU Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga jana walivamia eneo la Mlima Kenya kusaka kura za urais huku kila mmoja aking’ang’ania sehemu ya zaidi ya kura milioni sita za ukanda huo.

Dkt Ruto alikuwa kaunti za Embu na Kirinyaga akiandamana na washirika wake wapya, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula, ambapo aliendelea kuwasihi wakazi wasimchague Bw Odinga kwa sababu ni “mradi wa matajiri”.

Naye Bw Odinga alikita kambi katika Kaunti ya Murang’a ambako alinadi sera za vuguvugu la Azimio la Umoja katika mkutano ulifanyika katika uwanja wa Ihura, eneobunge la Kiharu.

Awali, Waziri huyo mkuu wa zamani aliwatembelea wakwe zake, Daniel Gachukia na Profesa Eddah Gachukia nyumbani kwao eneo bunge la Kandara.

Mkewe mwanawe Bw Odinga, Raila Junior, Wambui Odinga, ni mjukuu wa Bw na Profesa Gachukia.

Akiongea katika kituo cha kibiashara cha Kibugu, eneobunge la Manyatta, Kaunti ya Embu, Dkt Ruto alipigia debe muungano mpya wa Kenya Kwanza huku akimtaja Bw Odinga kama “mtu mwongo ambaye hupenda kuhadaa washirika wake kwa manufaa yake kibinafsi.”

Naibu Rais alisema ni kutokana na mwenendo wa Bw Odinga wa kuwahadaa washirika wake ambapo mswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya kisiasa ulipitishwa ili kuzima tabia hiyo.

“Rais Uhuru Kenyatta alitia saini mswada huo kuwa sheria ili kumzuia yule jamaa wa vitendawili asiwadanganye wenzake. Amewahaa watu wengi zaidi kiasi kwamba imelazimu sheria itengengezwe ili kuzuia uwongo huo. Ikiwa ni mwongo katika mahusiano yake na viongozi wengine, sembuse wananchi?” Dkt Ruto akauliza.

“Badala ya sheria kutungwa kwa ajili ya kuboresha uchumi, kubuni nafasi za ajira na kustawisha kilimo, bunge linalazimishwa kuketi hadi usiku ili kudhibiti uwongo wa mtu mmoja. Mbona tutunge sheria ili kuzuia mtu mmoja kuwadanganya wenzake?”

“Huyu mtu aende nyumbani. Tunamwambia akome kuitisha maandamano, akome kujiapisha,” Dkt Ruto akaongeza.

Naye Bw Odinga alimshambulia Dkt Ruto, Mudavadi na Wetang’ula akiwataja kama viongozi ambao walifeli katika utendakazi katika nyadhifa walizoshikilia awali na badala yake wakajihusisha na ufisadi.

“Hawa jamaa watatu ninawafahamu zaidi kwa sababu nimewahi kufanya kazi nao. Mmoja nilimteua kama Naibu Waziri Mkuu na akashindwa na kazi. Mwingine alihudumu kama Waziri wa Kilimo lakini akajigeuza mfanyabiashara wa mbolea badala ya kusaidia wakulima wapate pembejeo hiyo kwa bei nafuu. Mwingine aliuza nyumba ya ubalozi wa Kenya kule Japan akiwa waziri wa mashauri ya Kenya. Eti sasa wameungana kuwahadaa Wakenya kwamba wataboresha maisha yao,” akasema.

Ripoti ya MERCY MWENDE, DAVID MUCHUI na CHARLES WASONGA

 

You can share this post!

JUKWAA WAZI: Murkomen ‘amkaribisha’ rasmi...

Wandani wa Raila wapiga jeki kampeni za Natembeya

T L