• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Raila: Ni Krismasi ya mahangaiko

Raila: Ni Krismasi ya mahangaiko

NA EVANS JAOLA

HUKU Wakenya wanapojiandaa kusherehekea Krismasi, kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga, amesema  Wakenya wanapitia kipindi kigumu kwa sababu ya gharama ya juu ya maisha.

Bw Odinga amesema hayo Jumapili katika uwanja wa michezo wa Ndura ulioko Kitale katika Kaunti ya Trans Nzoia wakati wa fainali za kombe la Gavana George Natembeya.

Kiongozi huyo wa mrengo wa upinzani amesema Wakenya wana jukumu la kuhakikisha serikali iliyoko madarakani inawarahisishia maisha badala ya kuongeza ushuru kila kukicha.

“Krismasi mwaka huu 2023 imewadia wakati familia nyingi zinabambanya kupata chakula. Kila raia mzalendo ana haki ya kuitisha mabadiliko ili maisha yaimarike,” akasema Bw Odinga.

Kiongozi huyo wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) amesema hali hii inasababishwa na ushuru wa juu na pia bei za juu kwa bidhaa za msingi.

“Wakati mwafaka ukifika tutaitisha maandamano ya amani mwaka ujao wa 2024,” amesema kiongozi huyo.

Bw Odinga alikuwa ameandamana na kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa aliyeikemea serikali ya Kenya Kwanza kwa kushindwa kupunguza bei za bidhaa muhimu, akisisitiza kwamba Bw Odinga ndiye kiongozi bora anayeweza kulainishia Wakenya maisha.

Naye Gavana wa Siaya James Orengo amewataka Wakenya kutokezea kwa wingi Bw Odinga akiitisha maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.

Naye naibu kiongozi wa DAP-K Ayub Savula amewasuta wanaosema Bw Odinga ni mzee asiyeweza kuwania urais mwaka 2027.

Naye mwenyeji wao, Gavana Natembeya amechukua fursa hiyo kuwatakia Wakenya Krismasi njema.

  • Tags

You can share this post!

Historia ya kumfuatilia Baba Krismasi ilianzaje?

Polisi wachunguza kisa cha vijana 4 kuuawa Buruburu kwa...

T L