• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Raila njiapanda kuhusu muafaka akionekana ‘mateka’

Raila njiapanda kuhusu muafaka akionekana ‘mateka’

NA WANDERI KAMAU

KINARA wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, yuko kwenye njiapanda kuhusu mwelekeo atakaofuata katika kutatua mzozo kuhusu uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kati ya maswala mengine yenye utata, baada ya vigogo-wenza kumrai kufuata njia ambayo haitawaacha nje.

Jana Jumatano, duru katika mrengo huo ziliiambia ‘Taifa Leo’ kuwa, vigogo wenza wa Bw Odinga—Kalonzo Musyoka (Wiper), Bi Martha Karua (Narc-Kenya), Jeremiah Kioni (Jubilee), Eugene Wamalwa (DEP) kati ya wengine—wanamshinikiza afuate mkondo kama ule wa Maridhiano ya Kitaifa mnamo 2008, uliobuni Serikali ya Muungano wa Kitaifa kati yake akiwa Waziri Mkuu na Rais (marehemu) Mwai Kibaki.

Duru hizo zilisema kuwa vigogo hao wanahofia kuwa ikiwa Bw Odinga atafuata mchakato wa Bunge la Kitaifa –unaopendekezwa na mrengo wa Kenya Kwanza, wake Rais William Ruto—basi kuna uwezekano wengi wao wataachwa nje, hivyo kuendelea kuwa katika baridi ya kisiasa.

Pia, wanahofia huenda Kenya Kwanza ikatumia wingi wake katika Bunge kuhujumu baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Azimio. Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema huenda matakwa hayo mapya yakamweka Bw Odinga katika hali ngumu kisiasa, ikizingatiwa Rais Ruto na waandani wake wamesisitiza kuwa hawatakubali handisheki au makubaliano yoyote ya kisiasa na Bw Odinga au washirika wake.

Mnamo Jumapili, Rais Ruto alikutana na viongozi wa Bunge la Kitaifa na Seneti wa Kenya Kwanza, kwa mazungumzo yaliyoangazia kuanzishwa kwa mchakato wa kubuni kundi la wabunge litakalouwakilisha mrengo huo katika mchakato huo.

Jumatatu, Rais Ruto aliwahakikishia wafuasi wake kuwa hatua yake ya kukubali mazungumzo na Bw Odinga kujadili masuala tata aliyoibua si njia ya kubuni handisheki hata kidogo.

“Hakuna handisheki hata kidogo. Lazima tuheshimu Katiba. Hatutaki kujipata kwenye hali tuliyojipata kati ya 2018 na 2022, ambapo hakukuwa na Serikali wala Upinzani,” akasema Dkt Ruto.

Awali, kauli iyo hiyo ilikuwa imetolewa na washirika wake Naibu Rais Rigathi Gachagua na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa.

Kwenye mahojiano Jumatano, mdadisi wa siasa Prof Macharia Munene alisema ikiwa Bw Odinga atashinikiza mchakato wa Maridhiano ya Kitaifa, basi hilo litakuwa kama mwiba wa kujidunga, kwani Kenya Kwanza italitumia kujijenga kisiasa.

“Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa hana mipango yoyote ya kuingia katika serikali kupitia mlango wa nyuma, kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya wanasiasa wa Kenya Kwanza kama Bw Ichung’wa. Kenya Kwanza itatumia hilo kuanza kumponda Bw Odinga kama kiongozi mnafiki,” akasema Prof Munene.

Mdadisi huyo alisema mwelekeo huo pia utamsawiri vibaya Bw Odinga kimataifa, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya mataifa yaliyohusika katika kumrai kusitisha maandamano aliyokuwa akiyaongoza ni Amerika.

“Bw Odinga ataonekana kuwa mnafiki, anayetumia ushawishi wake kuihangaisha serikali bila sababu maalum. Ni hali inayoweza kumharibia sifa na mustakabali wake wa kisiasa,” akasema mdadisi huyo.

Bw Musyoka, imeibuka, anahofia kutelekezwa kwenye baridi ya kisiasa, kwani hilo litaathiri azima yake ya kuwania urais 2027. Bw Musyoka analenga kumrithi Bw Odinga kisiasa ielekeapo 2027, ikizingatiwa amemuunga mkono kuwania urais mara tatu—2013, 2017 na 2022.

Mwaka 2022, kiongozi huyo alikubali kumuunga mkono Bw Odinga licha ya kumteua Bi Karua kama mgombea-mwenza wake. Wadadisi wanaeleza Bw Musyoka anahofia kuachwa nje kisiasa kama ambavyo Bw Odinga aliwafanya waliokuwa washirika wake katika muungano wa National Super Alliance (NASA)-Bw Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula-alipofanya handisheki na Rais Mstaafu Uhuru Kenyata mnamo 2018.

Wakosoaji wa Bw Odinga wamekuwa wakisema alitumia handisheki baina yake na Bw Kenyatta pekee kujifaidi, huku akiwasahau washirika wake kama Bw Mudavadi, Bw Wetang’ula na vigogo wengine waliomsaidia katika kampeni za urais 2017.

Washirika wa Bw Musyoka katika Wiper na ngome yake ya kisiasa eneo la Ukambani wamekuwa wakisisitiza kuwa wakati umefika Bw Odinga kumrudishia mkono kwa kusimama naye mara tatu kuwania urais, hata baada yake kutomteua kuwa mgombea-mwenza wake mwaka uliopita.

Wasiwasi kama huo ndio wanaodaiwa kuwa nao Bi Karua na Bw Kioni, ikizingatiwa wameibukia kuwa washirika wakuu wa Bw Odinga, hasa kwenye maandamano aliyokuwa akiyaongoza kila Jumatatu na Alhamisi.

“Kwa kumshinikiza Bw Odinga kutozingatia mchakato wa Bunge, vigogo hao wanalenga kuhakikisha kuwa hata wao wamevuna, kwani wamekuwa pamoja na Bw Odinga katika harakati zote za kuishinikiza serikali ya Rais Ruto kuangazia masuala tata waliyoibua,” asema mdadisi wa siasa Javas Bigambo.

Vile vile, anasema kuwa ikiwa Bw Odinga ndiye atafaidika pekee, basi huenda vyama tanzu katika mrengo wa Azimio kama vile Wiper, Narc-Kenya, Jubilee kati ya vingine vikahisi kutengwa na ODM, kwani vilitoa mchango pia kwa kura alizopata Bw Odinga kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

  • Tags

You can share this post!

JURGEN NAMBEKA: Mafuriko ya Mwatate ishara hatujapangia...

Fungueni ‘server’ bila kuogopa – Madzayo

T L