• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
Raila sasa atangaza maandamano upya

Raila sasa atangaza maandamano upya

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga jana Ijumaa alitangaza rasmi kwamba, maandamano yatarejea Jumanne baada ya mazungumzo kuporomoka.

Akiongea katika uwanja wa Kamukunji, eneo bunge la Kibra, Nairobi baada ya kurejea nchini kutoka ziara ya wiki moja Dubai, Bw Odinga alisema walisitisha maaandamano hayo kwa muda kutoa nafasi kwa sherehe za Pasaka na maadhimisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

“Viongozi wa madhehebu ya Kikristo walikuja kwetu na kuzungumza nasi kuhusu Pasaka. Kisha, wenzao wa Kiislamu wakaja na kutuomba tusimamishe maandamano kutoa nafasi kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Hii ndio sababu tulisimamisha maandamano bali sio kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa Ruto (Rais) na watu wake,” Bw Odinga.

“Kwa hivyo, kesho (leo) ni Jumamosi, kesho kutwa ni Jumapili, mtondo ni Jumatatu siku ya Leba Dei, kisha Jumanne tunarejea uwanjani,” akaongeza huku akishangiliwa na mamia ya wafuasi wake.

Bw Odinga aliisuta serikali kwa kuchelea kutimiza matakwa yao kuhusu kupunguzwa kwa ghrama ya maisha miongoni mwa maswala mengine.

Alikariri kuwa wanataka serikali ishukishe bei ya unga, umeme, mafuta na karo ya shule na Rais akome “kununua” wabunge wa mrengo wa Azimio ili kuupa nguzu upande wa Kenya Kwanza.

Aidha, Bw Odinga alisema wanataka mitambo ya kuhifadhi matokeo ya kura za urais ifunguliwe ili ifanyiwe ukaguzi huru kusudi “mshindi” huru wa uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022 ajulikane.

“Aidha, tunataka wale makamishna wanne waliotofautiana na matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati warejeshwe kazini kwa sababu hawakuwa na makosa yoyote,” akasema.

Mnamo Jumatatu wiki hii, mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Azimio Wycliffe Oparanya alitangaza kuwa maandamano hao yatafanyika jijini Nairobi pekee wala sio miji mingine ilivyofanyika Machi 2023.

“Tutafanya maandamano ya amani katika barabara kadha jijini Nairobi kuanzia asubuhi hadi jioni. Kwa hivyo, tunawataka polisi kutoa ulinzi kwa wafuasi wetu kwani tunarajia kuwasilisha barua ya malalamishi katika jumba la Harambee,” akasema Bw Oparanya ambaye ni gavana wa zamani Kakamega.

Kuhusu mazungumzo ambayo yaliporomoka Jumanne wiki hii, Bw Odinga alisema ni dharua kubwa kwa mrengo wa Kenya Kwanza kujumuisha Mbunge wa Eldas Adan Keynan katika kikosi chao.

“Ni utovu wa heshima kwetu kwa Kenya Kwanza kuchukua mwanachama wetu na kujumuisha katika kundi la wawasilishi wao ilhali ni mbunge wa Jubilee, iliyoko ndani ya Azimio,” Bw Odinga akasema.

“Sasa nasikia kwamba wamekubali kuondoa jina la Keynan. Lakini sisi pia tunasema kuwa Bw David Pkosing, ambaye ni Mbunge wa Pokot Kusini ataendelea kuwa upande wetu hata kama tumesikia kuwa chama cha Kenya Union Party (KUP) kimeomba talaka kutoka Azimio,” akaongeza.

Mnamo Alhamisi, kiongozi wa wawakilishi wa Kenya Kwanza katika mchakato huo wa mazungumzo George Murugara (Mbunge wa Tharaka) alisema mrengo huo umekubali kutomshirikisha Bw Keynan katika mazungumzo hayo “hivyo Azimio nao wamuondoe Bw Pkosing”.

Mnamo Jumatano, kiongozi wa chama cha KUP Profesa John Lonyangapuo alitia saini mkataba wa ushirikiano kati ya chama hicho na muungano wa Kenya Kwanza.

Hafla hiyo ilifanyika katika makao makuu ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu wa chama hicho Cleophas Malala.

Kuhusu mauaji ya halaiki ya Shakahola, Bw Odinga alipendekeza kuwa uchunguzi wa kina kuhusu uovu huo ufanywe na wataalamu kutoka nje.
Huku akisema serikali inafaa kuwajibikia mauaji hayo ya zaidi ya watu 100, Bw Odinga alilaani hatua ya Waziri wa Usalama Kithure Kindiki kuzima wanahabari wasiingie katika shamba hilo la mauti.

“Tunataka wanahabari waruhusiwe kupeperusha habari moja kwa moja kutoka eneo hilo. Wakifukua miili kutoka kaburi moja, wanahabari wanapiga picha na kusambazia walimwenguni. Operesheni ya kufukua miili katika shamba hilo haifai kuendeshwa kwa siri. Je, wanaficha nini?” Bw Odinga akauliza.

Wengine waliozungumza katika mkutano huo ni kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka miongoni mwa vinara wengine wa Azimio. Bi Karua alishikilia kuwa bei ya Unga sharti ipunguzwe hadi Sh100 kwa pakiti moja ya kilo mbili.

“Hii ndio maana tumesema kuwa Jumanne tutarejea uwanjani baada ya mapumziko ya muda mfupi. Hii ni kwa sababu tumegundua kuwa hii serikali inachezea shere Wakenya kuhusiana na suala hilo lenye uzito mkubwa zaidi,” akasema.

Naye Bw Kalonzo alimpongeza Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta katika juhudi zake za “kuokoa Jubilee dhidi ya wanyakuzi.”

“Rais Kenyatta alifanya jambo la busara na tunamuunga mkono. Ukigusa Jubilee umechokoza Azimio. Kwa hivyo, sote tunamuunga mkono Uhuru,” akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Shughuli ya ufukuaji makaburi Shakahola yatatizwa na mvua...

Huduma zakwama kaunti zikitatizika

T L