• Nairobi
  • Last Updated May 30th, 2023 10:25 AM
Ruto aahidi atakubali matokeo akishindwa

Ruto aahidi atakubali matokeo akishindwa

NA LEONARD ONYANGO

NAIBU RAIS William Ruto jana aliahidi kuwa atakubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu ujao ikiwa atashindwa katika kinyang’anyiro cha urais.

‘Tutakubali matokeo ya uchaguzi ujao kwani atakayechaguliwa atakuwa ni kwa mapenzi ya Mungu,” akasema Dkt Ruto wakati wa maombi ya kitaifa katika hoteli ya Safari Park jijini Nairobi, Alhamisi.

Naibu Rais alisema hayo huku akiendelea kunung’unika kuwa mrengo wa Azimio unasaidiwa kwa raslimali za Serikali katika kampeni zake.

Pia amekuwa akidai kuna njama ya udanganyifu katika uchaguzi huo, kauli ambazo zinaonyesha huenda mrengo wake ukapinga matokeo iwapo wapinzani wao watatangazwa washindi.

Tayari muungano wa Kenya Kwanza umewasilisha malalamiko kwa IEBC ukitaka masuala kadhaa yashughulikiwe katika kuhakikisha kutakuwa na uwazi na haki kwenye uchaguzi huo.

Maombi hayo yalihudhuriwa pia na Rais Uhuru Kenyatta na Mwaniaji-Mwenza wa Azimio, Bi Martha Karua miongoni mwa viongozi wengine wa ngazi za juu serikalini.

Mwaniaji urais wa Azimio, Raila Odinga na mwenzake wa Wiper, Kalonzo Musyoka hawakuhudhuria maombi hayo ambayo huandaliwa kila mwaka.

Bi Karua alihimiza wanasiasa wenzake kufanya kampeni zinazohusu sera badala ya kudunishana: “Watu wanaomba hapa lakini wakitoka nje wanaendesha kampeni za matusi. Tushindane kwa sera wala si matusi. Maombi yetu yaandamane na matendo.”

Dkt Ruto pia alionekana kumlaumu Rais Kenyatta kwa matatizo yanayowakumba Wakenya akisema uhasama baina yao tangu 2018 ndio sababu ya serikali ya Jubilee kushindwa kutatua matatizo yanayowakumba Wakenya: “Najua hatukutimiza matarajio yenu, mimi binafsi nawaomba Wakenya msamaha. Ikiwa nilikosa kuafikia matarajio yako, naomba msamaha.”

Rais Kenyatta aliwataka wanasiasa wote wanaowania viti kukubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Uhuru ajitetea kuhusu njaa

Kiongozi wa nchi alijitetea kuhusu gharama ya juu ya maisha akidai kuwa inachangiwa na misukosuko ya vita nchini Ukraine.

Lakini wataalamu wa uchumi wanatofautiana na kauli ya Rais Kenyatta wakisema sera duni za serikali yake ndizo zimetumbukiza taifa kwenye matatizo ya kiuchumi ambayo yanakumba idadi kubwa ya Wakenya.

Katika utawala wake, Rais Kenyatta alikosa kuweka sera za kuinua uzalishaji wa bidhaa nchini na badala yake akafanikisha uagizaji hata wa bidhaa za kimsingi zinazoweza kuzalishwa nchini.

Wataalamu wanasema sera hizo ndizo zimefanya Kenya kutegemea kwa kiasi kikubwa karibu bidhaa zote ikiwemo chakula kutoka nje ya nchi.

Wanatoa mfano wa bidhaa kama vile mayai, vitunguu, mahindi, sukari, matunda, ngano na hata maziwa ambazo Kenya hununua kutoka mataifa jirani ya Uganda na Tanzania.

Hii ni licha ya Kenya kuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo kwa mahitaji yake na hata kuuza nje ya nchi kupitia kwa ustawishaji wa kilimo cha kunyunyizia mashamba maji, kupunguza bei ya pembejeo na kuweka sheria za kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu na mbolea ya ubora wa juu.

Kwa sasa Wakenya wapatao milioni tatu wanakumbwa na njaa huku mamilioni ya wengine wakishindwa kumudu gharama ya chakula.

Wachanganuzi wanasema kutegemea bidhaa za kigeni ndiko kiini cha mkurupuko wa bei unaoshuhudiwa kwa sasa kwani matatizo katika mataifa yanayouzia Kenya bidhaa huathiri Wakenya moja kwa moja.

Katika sekta ya viwanda, serikali imefanikisha uagizaji wa kila aina ya bidhaa kutoka mataifa kama vile China, Uturuki miongoni mwa mengine, badala ya kuinua viwanda vya hapa Kenya kwa kupunguza gharama ya stima pamona na ushuru.

Mzigo wa deni ambao Rais Kenyatta atawaachia Wakenya pia unalaumiwa na serikali yake kukosa uadilifu katika kusimamia uchumi.

  • Tags

You can share this post!

Wasafiri wataka ujenzi wa Uwanja wa Ndege Manda ukamilishwe

Wafuasi wa Ruto wahofia wimbi la Karua

T L