• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Ruto, Raila wang’ang’ania IEBC

Ruto, Raila wang’ang’ania IEBC

NA MOSES NYAMORI

VUTA nikuvute imezuka kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio Raila Odinga kuhusiana na mswada unaopendekeza kubadilisha utaratibu wa uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wabunge wanaoegemea mrengo wa Azimio jana aliapa kuangusha Mswada huo wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC, 2022 uliodhaminiwa na kiongozi wengi Kimani Ichung’wa (Kikuyu).

Wandani hao wa Odinga wamedai nia ya mabadiliko yaliyopendekezwa katika mswada huo, unaolenga kubadilisha muundo wa jopo la uteuzi wa makamishna, ni kumwezesha Rais Ruto “kudhibiti” tume hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Lakini wabunge wa muungano wa Kenya Kwanza (KKA) wanashikilia kuwa wataharakisha mabadiliko yaliyopendekezwa kuondoa makossa yaliyoko katika sheria ya sasa.

Wanasema mabadiliko hayo yatawezesha shughuli ya uteuzi wa makamishna wapya “inajumuisha wadau wote”.

Mswada huo unajiri wakati huu ambapo shughuli ya uteuzi wa mwenyekiti mpya na makamishna wawili itarajiwa kuanza.

Mwenyekiti wa sasa Wafula Chebukati na makamishna Profesa Abdi Guliye na Boya Molu wanatarajia kustaafu mnamo Januari 17, muhula wao wa kuhudumu utakapoisha rasmi.

Wabunge wa KKA wanadai kuwa Sheria ya IEBC ya sasa ililazimishwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kwa nia ya kuwaacha nje wadau wengine wakati wa uteuzi wa Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna Irene Masit, Francis Wanderi na Justus Nyang’aya kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mswada huo, ambao unasubiri kuwasilishwa bungeni ili usomwe kwa Awamu ya Kwanza, unalenga kupunguza nafasi zilizotengewa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) kuteua wanachama wa jopo hilo la uteuzi.

Wakati huu, PSC imepewa nafasi ya kuteua wanachama wanne kati ya wanachama saba wa jopo hilo.

WANACHAMA WAWILI

Mswada huo sasa unapendekeza kuwa PSC iteue wanachama wawili badala ya wanne. Nafasi mbili zilizosalia zimetengewa Kamati Shirikisho ya Vyama vya Kisiasa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC).

Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) imedumisha nafasi yake moja sawa na Baraza Madhehebu Nchini (IRC) ambalo limesalia na nafasi mbili ilizotengewa katika sheria ya sasa.

“Lengo kuu na Mswada huu ni kuifanyia mabadiliko sehemu ya kwanza ya Sheria ya IEBC, Nambari 9 ya 2011 ili kubadilisha muundo wa jopo la uteuzi litakalojaza nafasi zilizoko wazi katika tume,” inasema mswada huo.

“Jopo hilo la uteuzi litajumuisha mwanamume na mwanamke, waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Bunge, mtu mmoja aliyependekezwa Kamashiri Shirikishi ya Vyama vya Kisiasa, mtu mmoja aliyependekezwa na Chama cha Wanasheria Nchini na watu wawili waliopendekezwa na baraza la madhehebu nchini (IRC),” mswada huo unapendekeza.

Bw Ichung’wa aliambia Taifa Leo kwamba kujumuishwa kwa Kamati Shirikishi ya Vyama vya Kisiasa kutahakikisha wadau wote wa kisiasa wanashirika katika mchakato wa uteuzi wa makamishna wa IEBC.

Alisema Sheria ya sasa imegeuzi mchakato huo kudhibitiwa na vyama vya kisiasa vyenye wanachama katika PSC.

Hii, alisema, inavifungia nje wadau wengine wengi katika mpango wa uteuzi wa makamishna wapya.

“Tunataka kuondoa uenevu ulioletwa na sheria ya sasa ambapo ni vyama vya kisiasa vinavyowakilishwa bungeni pekee ndivyo vyenye nafasi ya kushiriki katika shughuli hiyo muhimu.

“Ukitazama uteuzi uliopita, utagundua kuwa ulifanywa na Jubilee na ODM pekee huku vyama vingine vikiachwa nje. Kwa kuilete Kamati Shirikishi ya Vyama vya Kisiasa, tutahakikisha vyama vyote vinahusishwa,” Bw Ichung’wa akasema.

“Kuna haja ya kuharakishwa kwa Mswada huo kwa sababu Chebukati na makamishna wawili wanaondoka Januari. Hatutakubali kuwa na tume isiyoweza kutekeleza wajibu wake ipasavyo, kwa sababu makamisha wanne waliosalia hawajahitimu kuhudumu kama mwenyekiti,” akaongeza Mbunge huyo wa Kikuyu.

Lakini wabunge wa Azimio wanadai hatua ni sehemu ya njama fiche inayolenga kumpendelea Dkt Ruto kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Kiranja wa wachache Junet Mohamed alisema mswada huo unalenga kumwezesha Rais Ruto “kuteka uchaguzi mkuu wa 2027 kupitia IEBC”.

“Tutakataa mswada huu ndani na nje ya Bunge. Sasa hii ndio kielelezo cha hatua ya serikali kuteka IEBC na uchaguzi wa 2027. Mbona wanataka kubadilisha muundo wa jopo la uteuzi? Muundo wa sasa ulifikiwa kufuatia mashauriano mapana,” akasema Bw Mohamed, ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki.

You can share this post!

Namwamba ahofia mabadiliko ya tabianchi yatavuruga michezo

Jezi za Ingwe zanunuliwa kama njugu

T L