• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Ruto, Raila wararuana Mombasa

Ruto, Raila wararuana Mombasa

BRIAN OCHARO na VALENTINE OBARA

UBABE wa kisiasa kati ya Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na Naibu Rais William Ruto katika Kaunti ya Mombasa ulionekana jana wakati wawili hao walipoongoza mikutano sambamba katika kaunti hiyo.

Bw Odinga alifichua kuwa, hakuwa na mpango wa kuandaa mkutano wa kisiasa Mombasa ila alialikwa na Gavana Hassan Joho.Mkutano huo ulileta pamoja wazee wa kijamii katika ukumbi wa Sheikh Khalifa, huku Dkt Ruto akiandaa mkutano wake na wazee katika uwanja wa Burhani kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Waziri huyo mkuu wa zamani alikuwa amewasili Pwani wiki iliyopita ikisemekana alikuwa mapumzikoni, lakini akaandamana na Rais Uhuru Kenyatta kuzindua karakana kubwa ya meli Mombasa Ijumaa kabla kuelekea maeneo ya magharibi Jumamosi.

Katika mkutano wa jana, Bw Odinga alipuuzilia mbali mfumo wa kiuchumi unaopendekezwa na Dkt Ruto, akisema hautasaidia kutatua changamoto zinazokumba Pwani na nchi kwa jumla.Wakati huo huo, aliidhinisha azimio la Bw Joho kuingilia siasa za kitaifa atakapokamilisha kipindi chake cha mwisho cha ugavana mwaka ujao.

Alisisitiza kuwa, njia bora ya kuleta mabadiliko nchini ni kwa kuongeza uwezo wa kifedha kwa serikali za kaunti jinsi ilivyokuwa katika pendekezo la kurekebisha Katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI), na kusawazisha uwakilishi wa maeneobunge.

“Tutahakikisha kuwa haki inafanyika katika taifa letu. Kenya inataka ukombozi wa tatu. Wa kwanza ulileta uhuru, wa pili ukaleta Katiba mpya na wa tatu utakuwa wa kukomboa uchumi wetu,” akasema.Alikubaliana na Bw Joho kuhusu hitaji la kuangalia upya mahitaji ya Wapwani hasa malalamiko kuhusu Bandari ya Mombasa, ajira, uwekezaji kwa uchumi wa baharini na mengine.

“Haya yote tunaweza kufanya lakini lazima tubadilishe mtindo. Mtindo sio kusema ‘chini-juu’ bali kuwekeza mashinani ili ajira ipatikane kwa watu wetu,” akasema.

Kwa upande wake, Dkt Ruto alisisitiza mchango wake katika serikali ya Jubilee ulifanikisha miradi katika sekta kama vile barabara, maji, na maeneo ya viwanda.

“Ndio sababu mimi nasimama hapa leo kuwaambia tuko na mpango na mpango wenyewe waanza kwa kuunganisha Wakenya wote. Tumepanga ajenda ya kupeleka taifa letu mbele,” akasema.Alisisitiza kuwa mfumo aliopendekeza ndio utaleta mabadiliko.

“Tutafanya bidii ili tusishindwe kutekeleza yale matarajio ambayo mko nayo kwetu,” akasema.Wandani wake wakiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, walisema wanaamini watatatua tatizo kubwa la umiliki wa ardhi katika eneo la Pwani.

Bi Jumwa alidai kuwa Bw Odinga alikuwa na ushawishi wa kutosha kuishinikiza serikali kutekeleza mapendekezo ya ripoti ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) kuhusu dhuluma za umiliki wa mashamba.

“Akisimama anasema hayuko serikalini lakini tunaambiwa yeye humshauri Rais Uhuru Kenyatta. Kama wewe ni mshauri wa rais mbona usimwambie afungue zile ripoti za TJRC ili suala la shamba litatuliwe? Ripoti iko pale pale na mapendekezo yako pale pale. Sisi Wapwani tutafuata mtu ambaye atatekeleza mapendekezo yaliyotolewa,” akasema.

Wandani wa Dkt Ruto walimkashifu Rais Kenyatta wakidai kuwa msimamo wake wa kuunga mkono Bw Odinga unasababisha watumishi wa umma kuhisi wanalazimishwa kufuata msimamo wake kwa lazima.Ziara ya Naibu Rais mjini Mombasa inatarajiwa kuwa ya mwisho ya kisiasa mwaka huu, kwa mujibu wa wandani wake katika eneo hilo.

Alianza mikutano yake na viongozi wa kijamii Jumamosi usiku na alipangiwa kutamatisha kwa mkutano wa hadhara eneobunge la Kisauni.

You can share this post!

Hofu Omicron ikienea katika nchi 89 duniani

TAHARIRI: Umakinifu wahitajika sherehe zikinukia

T L