• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 2:56 PM
Sabina asema Uhuru alilaza damu chamani

Sabina asema Uhuru alilaza damu chamani

NA MWANGI MUIRURI

JUBILEE, Sabina Chege jana Alhamisi alitangaza kuwa atamtimua Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta kutoka uongozi wa chama hicho kukinusuru kisisambaratike zaidi.

Alisema ukosefu wa uaminifu kwa Bw Kenyatta unatokana na msururu wa matukio ya usaliti na kukosekana kwa juhudi zozote kwa upande wa rais mstaafu huyo kutoa uongozi thabiti. Kuhusu kushirikiana kwake na serikali ya Kenya Kwanza licha ya Jubilee kuwa chama tanzu cha Azimio la Umoja One Kenya, Bi Chege alisema kwa wakati huu hakuna sheria inayowafunga katika mkataba wa kabla ya uchaguzi.

Bi Chege alisema vinara wa muungano huo hawajaitisha mkutano wowote kutoa mwelekeo na hivyo basi kuacha kila chama kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wake wa kisiasa.

“Kuhusu chama cha Jubilee, kama tungebaki katika Azimio, tungekufa. Kama tungewinda peke yetu, tungekufa. Tuliona ni bora kuwa na mkakati huru tukiungwa na marafiki wetu ili tuweze kujiondoa tukiwa na afya njema na matumbo yaliyojaa,” alisema.

Vile vile, alisema Bw Kenyatta hana usemi wowote kuhusiana na siasa za eneo la Mlima Kenya kwa kuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amempokonya wadhifa huo.

“Hakuna sherehe inayohitajika kufanywa kujua kwamba Bw Gachagua ndiye msemaji wa Mlima Kenya kutokana na wadhifa anaoshikilia,” alisema.

Bi Chege alisema Bw Kenyatta kama kiongozi wa chama alikuwa akikiporomosha chama cha Jubilee hadi kikawa na wabunge 28 pekee licha ya kuwa kilikuwa kikitawala. Alisema hata sheria inamtaka Bw Kenyatta kuacha kushiriki siasa za chama baada ya kustaafu kama rais.

“Sheria haiko upande wake kwa kuwa miezi sita baada ya kuondoka Ikulu, inamzuia kuwa kiongozi wa chama chetu. Bado hajaandika barua kueleza kwamba angali anashiriki siasa,” alisema.

Alimlaumu Bw Kenyatta kwa kuacha majukumu ya kiongozi wa chama kwa kushindwa kufanya uamuzi na kutotetea nafasi ya chama hicho Bungeni huku akionekana kuegemea ODM kinachoongozwa na Raila Odinga. Akizungumza katika runinga ya Inooro, Bi Chege alisema Kenyatta alipuuza ukweli kwamba Sheria ya Vyama vya Kisiasa inatambua UDA, ODM, Jubilee na Wiper kila kimoja kikiwa na zaidi ya viongozi 18 waliochaguliwa.

“Alituhepa katika meza ya mazungumzo ya kugawana uongozi wa bunge. Jubilee haikuhusishwa katika uundaji wa kamati za bunge, Tume ya Bunge, tulijaribu kuwasiliana naye kwa simu na arafa. Hakujibu,” alidai.

Aliongeza kuwa Bw Kenyatta alikabidhi Jubilee kwa viongozi wa ODM. “Tulipoenda kurudisha chama chetu kwa kufuata sheria, ni wanasiasa wa ODM tuliopata wakilinda lango.

Bw Kenyatta alivamia ofisi zetu akiandamana na wahuni wanaofahamika barabarani. Jeremiah Kioni (Katibu Mkuu anayepigwa vita) alikuwa hapo kama mzee wa kanisa na wakili akishika chuma kikubwa tayari kwa vita,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

TANZIA: Mukami Kimathi aaga dunia

Wang’ara na teknolojia ya kutafsiri lugha kurahisisha...

T L