• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Sakaja aponyoka, Sonko akihema

Sakaja aponyoka, Sonko akihema

NA RICHARD MUNGUTI

SENETA wa Nairobi Johnson Sakaja atapumua kwa muda kwa kuruhusiwa kuwania ugavana wa Nairobi.

Uamuzi huo umetolewa hata baada ya pingamizi za muda mrefu kuhusiana na madai kuwa Bw Sakaja hana cheti cha digrii.

Jana, Jopo Maalum ninalosikiza malalamishi kuhusu uteuzi chini ya George Mburugu, lilisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haina mamlaka ya kuchunguza na kubaini uhalali wa cheti cha digrii cha mwaniaji ugavana au urais.

“Hili jopo na IEBC halina uwezo wa kutathmini uhalali wa cheti cha digrii cha mwaniaji kiti yeyote. Afisa msimamizi wa uchaguzi wa Nairobi hapaswi kumchukulia mtu kuwa mshukiwa anapowasilisha vyeti vyake vya kuhitimu,” akasema Bw Mburugu.

Alikataa malalamishi ya wapigakura watatu wa Nairobi kwamba Bw Sakaja hajahitimu kuwa na digrii.

“Ni wajibu wa walalamishi kuwasilisha ushahidi mbele ya hili jopo kuthibitisha kuwa Bw Sakaja hajahitimu. Si kazi ya Sakaja kuthibitisha kwa sababu vyeti alivyowasilisha kwa IEBC ni halali,” akasema.

Walalamishi walidai kuwa Bw Sakaja hajahitimu kwa sababu hakuwasilisha cheti halali kilichothibitishwa na Tume ya Kudhibiti Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE), kuwa alisoma na kuhitimu katika chuo kikuu cha Team, Uganda. Pia hakuwasilisha cheti cha digrii kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, kwamba alisoma na kuhitimu, kama alivyokuwa amedai awali.

Bw Sakala jana aliwasilisha mbele ya jopo picha za kuhitimu, cheti cha digrii kutoka Team na kitabu kilicho na majina ya mahafala Oktoba 2016.

Alipohutubia wanahabari nje ya Mahakama ya Milimani, Bw Sakaja alikana madai kuwa hajahitimu na akadai watu wenye ushawishi serikali wanataka kumzuia kwa kuwa anampa ushindani mkali mpinzani wake Polycarp Igathe.

Bw Igathe ndiye mwaniaji wa chama cha Jubilee na mrengo wa Azimio la Umoja, unaoungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

Punde tu baada ya uamuzi huo, Naibu rais Dkt William Ruto alishangilia hatua hiyo na kuwataka wapinzani wajiandae kuona chama cha United Democratic Alliance (UDA) kikitwaa ugavana Nairobi.

Akiwa katika uwanja wa Jacaranda, eneo la Embakasi Nairobi, Dkt Ruto alisema jopo la IEBC lilithibitisha kuwa Bw Sakaja alikuwa akipigwa kisiasa.

“Mimi sasa nataka niwambie watu wa Deep State na System. Mlichokuwa mmempangia sakaja, mtajua majui. Hatutakubali kibaraka wa mtu yeyote achaguliwe hapa Nairobi… Watu wa kuzimia (Azimio) wanajua chuma chao ki motoni sasa,” akasema Dkt Ruto.

Afueni hiyo ya Bw Sakaja ni ya muda, kwa kuwa leo Jumatatu anatarajiwa kuwasilisha ushahidi mbele ya CUE kwamba kweli alisoma na kuhitimu digrii Uganda kama alivyodai.

Mnamo Ijumaa, mwenyekiti wa CUE, Prof Chacha Nyaigotti-Chacha alimtaka Bw Sakaja awasilishe kati ya nyaraka nyingine, risiti za kulipia karo, barua pepe za mawasiliano na chuo kuhusu kazi za darasani, na awataje wahadhiri waliomfunza.

Pia, Idara ya upelelezi wa Jinai (DCI) inashubiri ushahidi sawa na huo, huku afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ikitaka ripoti iwasilishwe kabla ya Julai mosi.

Wakati huo huo, Wakenya leo Jumatatu wanatazama kwa makini uamuzi wa iwapo Mike Mbuvi Sonko atakubaliwa kuwania ugavana wa Mombasa au la.

IEBC ilikataa kumwidhinisha ikisema alitimuliwa mamlakani kwa ukiukaji wa sheria kuhusu maadili ya afisa wa umma. Ilisema Bw Sonko alipoteza rufaa za kupinga uamuzi wa Bunge la Seneti na hakuenda katika Mahakama ya Juu.

  • Tags

You can share this post!

Kazi kwa Vijana: Kibicho achemkia Ruto, Gachagua

Lugogo afurahia kurudi Bandari akitokea Sofapaka

T L