• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
Seneta Madzayo ajutia uamuzi wake wa kuacha kazi ya ‘utulivu’ mahakamani

Seneta Madzayo ajutia uamuzi wake wa kuacha kazi ya ‘utulivu’ mahakamani

NA MARY WANGARI

SENETA wa Kilifi Stewart Madzayo amefunguka kuhusu masaibu anayokumbana nayo tangu alipoacha kazi ya jaji wa mahakama kuu na kujitosa kwenye siasa alipoteuliwa kama Kiongozi wa Wachache katika Seneti.

Akizungumza Ijumaa katika warsha ya siku tatu ya wanahabari inayoendelea jijini Mombasa, seneta huyo wa ODM amesema wadhifa wake kama Kiongozi wa Wachache katika Seneti una pandashuka nyingi na aghalabu ni hatari.

Kulingana na seneta huyo wa upinzani, kazi yake humlazimu kuwa mstari wa mbele kila mara katika juhudi za kuwezesha sauti ya waundasheria kutoka kambi ya walio wachache kusikika.

Aidha, amefichua jinsi alivyokumbana na vitoa machozi kwa mara ya kwanza alipochukua usukani katika wadhifa wake.

“Si rahisi kuwa mahali nilipo. Nilikuwa na maisha yenye amani tele wakati nilikuwa wakili na jaji wa mahakama,” amesimulia Kiongozi wa Wachache.

Akaongeza, “Kuwa kwenye upinzani kunamaanisha kupinga kila wakati. Wakisema ni samawati unasema ni nyekundu. Nilikuwa naona watu wakikimbizwa na vitoa machozi hadi nilipogeuka mhasiriwa. Sikuwa nimewahi kuzabwa na vitoa machozi lakini sasa kama Kiongozi wa Wachache, ninaweza kuhesabu karibu mara 50 ambapo nimekumbana na vitoa machozi kwa kuwa kazi yangu inanilazimu kuwa mstari wa mbele kila mara.”

Kuhusu Mswada wa Fedha 2023, Bw Madzayo amekosoa Upande wa Wengi wa muungano tawala wa Kenya Kwanza kwa kuwashinikiza wabunge wake kufuata msimamo wa serikali na kuwatishia wanaokaidi.

Ameonya kwamba kuwashinikiza wabunge kutaingilia wajibu wao kikatiba wa kuwakilisha maslahi ya wapigakura waliowachagua akisisitiza kuwa ni sharti wabunge wawe huru kufanya kazi yao.

“Kwa upande wetu, hatuna tatizo kwa sababu si lazima uunge mkono msimamo fulani. Ni sharti wabunge waruhusiwe kufanya kazi yao bila kupatiwa vitisho. Enzi ya kutishiwa imepitwa na wakati. Haifai kabisa kutishia Bunge.”

Isitoshe, ameelezea wasiwasi wake kuhusu mtindo wa serikali wa kusisitiza kwamba wenyeviti wa karibu kamati zote za Bunge la Kitaifa na Bunge la Seneti ni sharti watoke upande wa Walio Wengi bila kujali tajriba yao kitaaluma.

Jaji huyo wa zamani aliyegeuka mwanasiasa ameonya kuwa, kando na kuathiri utoaji huduma wa wenyeviti wa kamati mbalimbali, huwa pia inalemaza utendakazi wao kwa sababu wengi wao wanahudumu vilevile kama manaibu wenyeviti.

“Kambi ya walio wengi ilisisitiza kuwa wenyeviti wote ni sharti watoke kwao pekee. Wengi wao hata hawana wakati wa kuhudhuria vikao vya kamati kwa sababu tuseme ni mwenyekiti hapa na naibu mwenyekiti katika kamati nyingine. Huwezi kuwa mwenyekiti, naibu mwenyekiti na mwanakamati kwa pamoja. Huna muda wote huo. Sio kama katika serikali zilizotangulia tangu 2013 hadi 2022.”

  • Tags

You can share this post!

Waogeleaji 200 kutafuta ufanisi Kiambu kesho Jumamosi

Alia warembo humkwepa wakidai hawakumbatii

T L