• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:20 AM
Sibanduki katika siasa ng’o – Uhuru

Sibanduki katika siasa ng’o – Uhuru

NA BENSON MATHEKA

RAIS (Mstaafu) Uhuru Kenyatta, jana Jumatatu aliapa kuwa hatabanduka katika siasa huku akiwaambia wanaomsukuma aachilie uongozi wa chama cha Jubilee kwamba hawaogopi.

Baadhi ya viongozi wa chama hicho wameungana na serikali kumshinikiza Bw Kenyatta kujiuzulu kama kiongozi wa chama hicho, uasi ambao ulimfanya kuitisha kongamano la kitaifa la wajumbe wa Jubilee lililofanyika Jumatatu.

Katika kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Ngong Racecourse, Nairobi, Bw Kenyatta alitangaza kuwa alibadili nia na kuamua kutostaafu siasa kutokana na vitisho vya baadhi ya wanasiasa kutwaa chama cha Jubilee.

Muungano unaotawala wa Kenya Kwanza umeunga waasi katika chama cha Jubilee kumshinikiza Bw Kenyatta kustaafu kwa mujibu wa Sheria ya Pensheni ya Kenya ili aweze kupokea marupurupu yake kama rais mstaafu.

“Niliwakabidhi mamlaka kwa amani mchana peupe lakini wanachofanya ni kunitusi na kuharibu chama chetu. Ninataka kuwaambia kuwa sisi tunapenda amani na kunyamaza kwetu sio uoga,” alisema.

Hata hivyo, rais huyo wa nne wa Kenya aliwaambia wazi kuwa vitisho na matusi ya mahasimu wake havitamfanya aache uongozi wa chama alichotumia kutawala.

“Sisi ni watu tunaopenda amani. Kukumbatia amani hakumaanishi sisi ni waoga. Hautatusikia tukitusi mtu. Wanaenda kanisani lakini badala ya kusali ni matusi tu. Wako hivyo na ni haki yao, lakini sisi kama Jubilee hatutafanya hivyo,” alisema.

“Kuna wakati ambao nilifikiria nitastaafu kutoka siasa. Nilifikiria ningekuja kwa NDC kukabidhi uongozi hadi pale baadhi ya watu walipoanza vitisho. Ninataka kuwaambia kwamba watishe mtu mwingine lakini sio mimi,” aliongeza Bw Kenyatta.

Akiapa kwamba hataogopa kutetea chama hicho, Bw Kenyatta aliwataka wasioridishwa nacho waondoke akisema wanaweza kumfanyia mambo mengine mengi lakini hatakubali wavuruge chama cha Jubilee.

“Nilinyamaza walipoiba mbuzi (kondoo) wangu na kuchoma mashamba. Wanaweza kuendelea kufanya hivyo lakini wasivuruge chama kwa sababu sio mali ya Uhuru Kenyatta,” alisema.

Alikuwa akirejelea uvamizi katika shamba lake na vijana waliokodishwa kuiba kondoo na kuchoma miti siku chache baada ya Kiongozi wa Wengi bungeni, Kimani Ichung’wah na Naibu Rais Rigathi Gachagua kuonya kuwa masikini wangevamia mali yake kwa kile walichodai kuwa anafadhili maandamano ya upinzani.

Katika kongamano la jana, wajumbe walipitisha kutimuliwa kwa waasi walioshirikiana na serikali kumtimua Bw Kenyatta kama kiongozi wa Jubilee wakiwemo Mbunge Maalumu Sabina Chege, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Kanini Kega na mwenyekiti wake Nelson Ndzuya.

Chama hicho pia kiliwatimua wabunge wa zamani Jimmy Angwenyi, mbunge wa Buuri Boniface Kinoti Gatobu), Naomi Shaban,Joshua Kutuny, Mutava Musyimi na Rachael Nyamai, Mkurugenzi wake mkuu Wambui Gichuru na Joel Kibe miongoni mwa wengine.

Viongozi wapya wa chama hicho ni Saitoti Torome (mwenyekiti), manaibu viongozi wa vyama Beatrice Gambo (mikakati) na Maoka Maore (operesheni), Joseph Manje (mipango), na Kados Muiruri.

Naibu katibu mkuu ni Yasir Noor, naibu katibu mratibu ni Pauline Njoroge. Aliyekuwa mbunge wa Kiharu Jamleck Kamau ndiye mkurugenzi mpya wa uchaguzi akichukua nafasi ya Bw Kega.

Kiongozi wa Azimio, Raila Odinga, aliyeongoza vinara wenzake kuhutubia kongamano hilo alisema hatua ya serikali ya kuvuruga chama cha Jubilee inalenga kuhujumu demokrasia ya vyama vingi.

Bw Odinga alisema iwapo serikali itaendelea kuvuruga chama hicho kwa kuunga waasi waliotimuliwa kuandaa kongamano la wajumbe, Azimio itajiondoa katika mchakato wa mazungumzo kupitia kamati teule ya bunge, uliosaidia kusitishwa kwa maandamano ya kila wiki.

“Wanataka kuharibu Jubilee sio kwa sababu ni dhaifu, ni kwa sababu wanatambua ina nguvu sasa na inaweza kuwa na nguvu zaidi na tishio miaka ijayo,” akasema Bw Odinga na kusisitiza kuwa Azimio itaunga Jubilee katika juhudi za kutetea demokrasia ya vyama vingi.

Akihutubia wanahabari muda mfupi baada ya kutimuliwa Jubilee, Bw Kega alipuuza NDC ya jana aliyoitisha Uhuru akisisitiza rais huyo mstaafu hana mamlaka ya kufanya maamuzi ya chama.

Bw Kega alisisitiza kuwa mrengo wake utamchukulia Uhuru hatua za kinidhamu kwa kutofuata mchakato wa kutatua mizozo ya chama.

“Tutaanda NDC halali baada ya Baraza Kuu la Kitaifa la chama kukutana,” alisema.

Bw Kega ambaye anadai kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Jubilee alisema NDC hiyo itafanyika kabla ya Julai 15, 2023 baada ya mchakato wa kutatua mizozo ya chama hicho kukamilika.

  • Tags

You can share this post!

Masaibu ya mhubiri Ezekiel yasikitisha wakazi Ngodhe

Omanyala kutetemesha kwenye riadha za Diamond League

T L