• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
Uhuru alivyozamisha merikebu ya Jubilee

Uhuru alivyozamisha merikebu ya Jubilee

NA WANDERI KAMAU

MVUTANO na mzozo unaoshuhudiwa katika Chama cha Jubilee (JP) umetajwa kuchangiwa na hatua ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuchelewa kuokoa jahazi la chama hicho.

Mnamo Jumatano, ilimlazimu Bw Kenyatta kufika katika makao ya chama yaliyo katika mtaa wa Kileleshwa, jijini Nairobi, baada ya makabiliano makali kuzuka baina ya makundi hasimu yanayowaunga mkono ‘makatibu wakuu’ tata Jeremiah Kioni na mbunge Kanini Kega wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Bw Kioni, ambaye alihudumu kama mbunge wa Ndaragwa, amekuwa akishikilia kuwa ndiye Katibu Mkuu halisi wa chama, huku Bw Kega akishikilia kuwa yeye ndiye Katibu Mkuu anayetambulika kisheria, kufutia mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na viongozi wake kwenye mkutano uliofanyika katika mkahawa mmoja jijini Nakuru mnamo Februari.

Misimamo hiyo mikali ndiyo imekuwa msingi wa mvutano wa kuchukua udhibiti wa chama baina ya viongozi hao wawili.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa kosa na lawama kuu kuhusu mzozo huo inapaswa kuelekezwa kwa Bw Kenyatta, kwani hajakuwa akionekana kushughulikia mizozo hiyo hapo nyuma, bali amekuwa akijitokeza katika dakika za mwisho mwisho.

Wanasema kuwa mtindo huo ulianza baada yake kuchaguliwa kama rais kwa muhula wa pili 2017, kwani alionekana kupuuza masuala ya chama na uongozi wake.

“Tangu 2017 alipochaguliwa kama rais, Bw Kenyatta aliitelekeza Jubilee na hapo ndipo matatizo yake yalipoanza. Aliacha kufanya mikutano ya mara kwa mara baina yake na wabunge waliochaguliwa kwa tiketi ya chama, na kuanza kukichukulia kama mali yake binafsi. Alianza kufanya maamuzi muhimu ya kisiasa bila kuwashirikisha viongozi, hali iliyoanza kubuni dhana za usaliti. Kwa mfano, wabunge wengi wamekuwa wakimlaumu kwamba hatua yake kubuni handisheki na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga 2018 haukuwa uamuzi wa chama bali uamuzi wake binafsi,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana naye, kosa jingine la Bw Kenyatta lilikuwa ni kuwaamini washirika wake wachache kuendesha na kusimamia masuala muhimu ya chama, badala ya kuwashirikisha wabunge na viongozi waliochaguliwa.

Baadhi ya washirika wanaolaumiwa kwa ‘kuangusha’ chama hicho ni aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wake, David Murathe.

“Wakati Bw Kenyatta alianza kusikiliza ushauri wa watu kama Bw Murathe na wengineyo, hapo ndipo meli ya Jubilee ilianza kuyumba. Hilo ndilo lilizaa uasi mkubwa kutoka kwa Rais William Ruto (wakati huo akiwa Naibu Rais) na viongozi waliomuunga mkono. Tangu wakati huo, nyota ya Jubilee imekuwa ikizama kila siku, dhihirisho kuu likiwa matokeo mabaya kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, ambapo chama kilipata viti vichache sana ikilinganishwa na uchaguzi wa 2017,” asema mdadisi wa siasa Oscar Plato.

Wadadisi wanasema kuwa mtindo wa Bw Kenyatta kutelekeza majukumu yake ya uongozi haukuanza leo au 2017, kwani alifanya hivyo tena wakati alikuwa Kiongozi Rasmi wa Upinzani nchini kati ya 2002 na 2007.

Wakati huo, aliacha chama cha Kanu—alichokuwa kiongozi wake – na kujiunga na Party of National Unity (PNU) chake Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki ambapo alimuunga mkono kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2007.

Katika hali hiyo, wadadisi wanasema Bw Kenyatta hapaswi kuwalaumu wabunge kama Bw Keega, Bi Sabina Chege kati ya wengine ambao wameiasi Jubilee na kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza, kwani yeye mwenyewe ndiye aliyechangia pakubwa masaibu yanayokiandama chama.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Ruto atarajie presha kali kutoka kwa Raila

Msaada kwa walioathirika na mafuriko Nakuru

T L