• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Uhuru amtolea Ruto kucha

Uhuru amtolea Ruto kucha

NA JUSTUS OCHIENG

RAIS (Mstaafu) Uhuru Kenyatta, jana Jumatano alilazimika kufika ghafla katika makao makuu ya chama cha Jubilee kuthibitisha ubabe wake katika chama hicho siku ambayo ghasia zilizuka kati ya wafuasi wa aliyekuwa Mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni na aliyekuwa mbunge was Kieni Kanini Kega, wanaopigania wadhifa wa katibu mkuu.

Mirengo hiyo miwili, mmoja unaounga Bw Kenyatta na mwingine unaounga Rais William Ruto, ilikabiliana vikali na kulazimisha polisi kutumia gesi ya kutoa machozi kutawanya wafuasi wao. Ghasia hizo zililazimisha Rais mstaafu huyo, ambaye ni kiongozi wa chama cha Jubilee, kutembelea makao makuu ya chama hicho mtaani Kileleshwa, Nairobi kumuunga mkono Bw Kioni, ambaye alimtambua kama katibu mkuu rasmi.

Bw Kenyatta aliitwa na Bw Kioni kufuatia kile alichotaja kama uvamizi wa makao makuu ya chama. “Niliitwa na Katibu Mkuu (Kioni) na akaniambia kinachotendeka. Nilisema lazima nifike kumuunga mkono na wanachama wa chama ili tulinde chama chetu,” Bw Kenyatta alisema katika makao makuu ya chama. Rais mstaafu, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, alisema kwamba, wanachama wa chama hicho ni lazima waheshimu sheria katika utatuzi wa mizozo.

“Tunataka haki zetu. Walipojaribu kutupokonya chama chetu, tulifuata sheria hadi tukapata haki. Kwa nini wavamie hapa na kuzua ghasia?” Bw Kenyatta alihoji akilenga mrengo wa Bw Kega.

Bw Kenyatta alihimiza Wakenya kuishi kwa amani, na kuwaonya wasichochewe kupigana.

“Tufuate sheria na kuishi kwa amani. Hakuna haja ya kuchochea kundi moja dhidi ya watu wengine,” alisema.

Bw Kenyatta ambaye pia alihutubia maafisa wa chama afisi za chama hicho akiandamana na Bw Kioni aliwataka wale wasioridhika na chama hicho kuhama badala ya kuzua ghasia za ndani.

“Yeyote anayetaka kuhama chama aondoke na kujiunga na kingine kwa amani. Ninawashukuru wote kwa kulinda chama chetu. Hatuna vita na yeyote na tunachowaambia wale wasiotaka kuwa katika chama hiki wako huru kuondoka na sio kuvuruga watu wenye amani hapa,” alisema Bw Kenyatta. Vile vile, alilaumu polisi, akiwaambia wazingatie kazi yao ya kulinda umma badala ya kutumiwa kisiasa na kuzua ghasia.

“Polisi wako na kazi nyingi na sio kuja hapa kuzua ghasia. Tunaonya wale wanaojaribu kutwaa chama kwa nguvu kwamba tutakilinda,” aliongeza Bw Kenyatta. Alisema kwamba, wanachama wa Jubilee wanaweza kutatua tofauti zao bila kusukumwa na polisi kuhusu wanachopaswa kufanya. “Ninaomba Wakenya waishi kwa amani. Tusikubali kuchochewa,” alisema.

Viongozi wengine wa Azimio wanaojumuisha Martha Karua, Kalonzo Musyoka, Wycliffe Oparanya na Eugene Wamalwa pia walitembelea afisi za Jubilee na wakamlaumu Rais Ruto kwa kutokuwa na nia njema, wakisema hatua yake inaonyesha kutojitolea kwa mazungumzo ya maridhiano.

“Tuko hapa kwa niaba yetu kama viongozi wa Azimio na pia kwa niaba ya kinara wetu Raila Odinga ambaye yuko nje ya nchi. Ni wazi kuwa agizo kutoka kwa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa inabatilisha barua ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa inayodaiwa kupatia mrengo fulani nguvu katika Afisi hizi.”

“Inaamanisha kuwa Kioni ndiye Katibu Mkuu na hao wengine, iwapo wako na tatizo lolote, wanafaa kutumia mfumo wa ndani wa Jubilee wa kutatua mizozo,” akasema Bi Karua.

Bw Musyoka alilaumu Kenya Kwanza kwa kutomheshimu Rais Mstaafu Kenyatta, ambaye ni kiongozi wa chama cha Jubilee. “Hauwezi hata kuonyesha heshima ndogo kwa Rais Mstaafu ambaye ni kiongozi wa Jubilee. Tunataka kuhimiza ukora kama huu ukome kwa kuwa Kenya ni nchi ya demokrasia,” alisema. Bw Musyoka alilaumu Kenya Kwanza kwa kutaka kunyakua Jubilee ili kuthibitisha mbunge wa Eldas Adan Keynan ni mwanachama wake.

“Hili ni jaribio la KK la kutuvuruga kabla ya maandamano yetu Mei 2 lakini hatutatishika. Tumejiandaa kukabiliana nao,” alisema Bw Wamalwa.

  • Tags

You can share this post!

Shakahola: Kontena kubwa Malindi kuhifadhi miili zaidi

Serikali yafunika uchi wake kwa kufungia nje wanahabari...

T L