• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Uhuru apigia debe Raila kumrithi 2022

Uhuru apigia debe Raila kumrithi 2022

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta kwa mara nyingine alionyesha dalili za kuunga mkono azimio la kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kuwa mrithi wake 2022, huku akimsuta Naibu Rais William Ruto.

Akizungumza kwa mafumbo alipoongoza hafla ya kuupandisha hadhi mji wa Nakuru kuwa jiji, Rais Kenyatta alimpigia debe Bw Odinga kimafumbo, akiwarai wenyeji kuwa hawapaswi kuzingatia umri wanapowachagua viongozi.

“Uongozi ni kama mbio za masafa marefu. Hupaswi kuenda kwa kasi, kwani utachoka haraka na kuishiwa na pumzi. Mzee (Odinga) atakuja na kukupita na baadaye kuibuka mshindi,” akasema Rais Kenyatta, akionekana kumlenga Dkt Ruto.

Dkt Ruto amekuwa akifanya kampeni katika sehemu tofauti nchini kwa kauli ya “Hustler” (mfumo wa kuwainua watu maskini kiuchumi).

Kampeni zake zimekuwa zikiendeshwa na mrengo wa ‘Tangatanga’, unaowashirikisha wabunge vijana, ambapo wengi wao wanahudumu mihula ya kwanza.

Rais Kenyatta alisema kwamba uongozi bora hautokani na umri wa mtu, bali mawazo, sera na maamuzi anayofanya.

“Msiambiwe mtu fulani hafai kwa sababu ya umri wake, kwani uongozi si kama mchezo wa kandanda. Uongozi bora hutoka kwa akili ya kiongozi husika,” akasema Rais Kenyatta.

Dkt Ruto amekuwa akimpuuza Bw Odinga kuwa “mzee”, akisema hana uwezo wa kuendeleza miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na utawala wa Jubilee.

Katika dalili zilizoonyesha mikakati ya kumpigia debe Bw Odinga, washirika wa Dkt Ruto walinyimwa nafasi kuhutubu katika hafla hiyo.

Licha ya hafla hiyo kuwa na umuhimu wa kitaifa, Dkt Ruto hakuhudhuria, na badala yake alikuwa akifanya kampeni katika Kaunti ya Machakos.

Bw Odinga ndiye alihutubu, huku akimsifia Rais Kenyatta kwa juhudi alizoweka kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Baadaye, washiriki walihutubiwa na Gavana Lee Kinyanjui, aliye mshirika wa karibu wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Bw Kinyanjui amekuwa miongoni mwa magavana kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakiwarai wenyeji kumuunga mkono Bw Odinga 2022.

Gavana huyo vile vile alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa wakiupigia debe Mswada wa BBI.

Seneta Susan Kihika na Mwakilishi wa Wanawake, Liza Chelule hawakuhutubu.

Wawili hao ni washirika wa karibu wa Dkt Ruto, ambapo wamekuwa wakiungana naye katika sehemu tofauti nchini kupigia debe chama cha UDA.

Wadadisi wanasema ni wazi sasa nia ya Rais Kenyatta ni kumwachia usukani Bw Odinga, licha ya kutotangaza msimamo wake wazi.

“Ingawa hatajitokeza wazi, uchaguzi utakapokaribia msimamo wake hautakuwa siri tena,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta aliwarai wenyeji kukumbatia nafasi hiyo kuboresha biashara na sekta nyingine muhimu za kiuchumi.

You can share this post!

Kenya kunufaika kupitia mpango wa FAO kukabili athari za...

Amerika kushirikiana na utawala mpya 2022

T L