• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Uhuru kujua hatma yake kama kinara wa Jubilee Jumatatu

Uhuru kujua hatma yake kama kinara wa Jubilee Jumatatu

NA MOSES NYAMORI

HUENDA Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akabwagwa kama kiongozi wa chama cha Jubilee huku Msajili wa Vyama Anne Nderitu akianza mchakato huo.

Bi Nderitu amempa Bw Kenyatta hadi Jumatatu kujibu maazimio ya mkutano wa Baraza la Kitaifa la Chama (NEC) na kambi pinzani inayoongozwa na Kanini Kega iliyomwondoa katika uongozi wa chama na kumteua Sabina Chage kuchukua nafasi yake.

Mrengo unaoongozwa na Bw Kega jana Ijumaa ulitoa wito kwa Bw Kenyatta kufika mbele ya kamati ya nidhamu kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Kambi hiyo ilimpa Bw Kenyatta siku mbili kujibu baadhi ya shutuma zilizotolewa dhidi yake kabla ya kubwagwa.

“Fahamu kuwa mzozo umewasilishwa dhidi yako na kupokelewa na Kamati ya Kusuluhisha Migogoro ya Ndani. Kwa hivyo mnatakiwa kuwasilisha majibu yenu, pamoja na nyaraka zozote kwa kamati ndani ya siku mbili,” ilisoma barua hiyo ya Ijumaa.

“Utaarifiwa kuhusu tarehe ya kusikilizwa utakapopewa fursa ya kusikilizwa kabla ya kamati kutoa uamuzi wake wa mwisho kuhusu suala hilo.”

Kadhalika, Bi Nderitu katika barua nyingine alimwambia Bw Kenyatta kuwasilisha utetezi wake kabla ya ofisi yake kufanya uamuzi kuhusu mizozo ya uongozi katika chama tawala cha zamani.

Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) inatazamiwa kufanya uamuzi iwapo Bw Kenyatta alitimuliwa kihalali katika chama alichoanzisha kabla ya kuchaguliwa tena 2017.

Kadhalika, ORPP inatarajiwa kutoa uamuzi iwapo atachukuliwa hatua za kinidhamu na chama kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

  • Tags

You can share this post!

Makanisa, wafanyikazi wakataa ushuru mpya

Shujaa Mukami Kimathi anazikwa leo

T L