• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:41 PM
Uhuru matatani Sabina ‘akihepa’ na Jubilee Party

Uhuru matatani Sabina ‘akihepa’ na Jubilee Party

NA BENSON MATHEKA

MZOZO wa uongozi katika chama cha Jubilee umechukua mwelekeo mpya baada ya mrengo unaounga serikali ya Kenya Kwanza, kumtimua Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kama kinara wake na kumtangaza Mbunge Maalum Sabina Chege kuwa kaimu kiongozi.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Bw Kanini Kega ambaye amekuwa akiongoza mapinduzi katika chama hicho, alikosoa hatua ya Bw Kenyatta ya kuita mkutano wa wajumbe wa Jubilee akimtaja kama kiongozi wa zamani ambaye hana mamlaka ya kufanya hivyo.

Wiki jana, Bw Kenyatta aliongoza mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee ulioidinisha kuandaliwa kwa mkutano wa wajumbe kujadili sera za chama. Miongoni mwa yaliyotarajiwa katika mkutano huo ilikuwa ni kupitisha kuondolewa chamani kwa mrengo unaoongozwa na Bw Kega ambao unajumuisha Bi Chege miongoni mwa wengine.

Jana Jumanne, Bw Kega ambaye amekuwa akizozania wadhifa wa katibu mkuu na aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa, Bw Jeremiah Kioni, anayeungwa na Bw Kenyatta, alisisitiza ndiye msemaji wa chama hicho na akatangaza kuwa kikatiba na kisheria, rais huyo mstaafu hawezi kuwa kiongozi wa chama.

Bw Kega alisema mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la chama cha Jubilee ulioongozwa na Bw Kenyatta haukuwa wa kikatiba kwa kuwa alikoma kuwa kiongozi wa chama miezi sita baada ya kustaafu.

“Uhuru alikoma kuwa kiongozi wa chama cha Jubilee na hivyo basi hawezi kuendesha masuala ya chama. Taarifa kwamba aliita mkutano wa wajumbe wa kitaifa haitambuliwi. Kulingana na katiba ya chama, mimi, kama waziri mkuu ninafaa kuitisha mkutano kama huo,” alisema Bw Kega.

Akaongeza Bw Kega; “Kulingana na katiba, rais mstaafu hafai kuhusika na siasa, miezi sita baada ya kuondoka ofisini. Kutoka wakati alioondoka ofisini, muda wake (kama kiongozi wa chama) uliisha Machi 2023.”

Mbunge huyo wa zamani wa Kieni, alisema kwamba angali Katibu Mkuu wa Jubilee, kulingana na maazimio ya mrengo ambao ulimtimua Bw Kioni kabla ya kumuondoa Bw Kenyatta jana Jumanne, alipoingilia kati mzozo wa uongozi katika chama hicho.

“Baraza Kuu la Kitaifa limeamua kuwa Sabina atahudumu kama kaimu kiongozi wa chama hadi Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe utakapofanyika ambapo tutachagua kiongozi ambaye atapeleka chama mbele,” akasema Bw Kega.

Mrengo wa chama cha Jubilee unaoongozwa na Bw Kega unaunga serikali ya Kenya Kwanza huku unaoongozwa na Bw Kioni ukisisitiza kuwa chama hicho kingali mwanachama wa Azimio la Umoja One Kenya na unaunga maandamano.

Wiki jana, Bw Uhuru alifika katika ofisi za chama hicho na kumuunga Bw Kioni huku akiapa kukilinda dhidi ya wanaotaka kukinyakua.

Siku mbili baadaye, aliita mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee ambao mrengo wa Bw Kega ulikataa kutambua na badala yake ukamtimua kama kiongozi wa chama alichoanzisha na kutumia kutawala wa mihula miwili.

  • Tags

You can share this post!

Azimio: Bado tutaandamana Alhamisi

Ombi la Mackenzie kuonja uhuru lilivyogonga mwamba

T L