• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Vigogo wanavyoviziana kuwania ubabe 2022

Vigogo wanavyoviziana kuwania ubabe 2022

Na BENSON MATHEKA

Vigogo wa kisiasa wanaomezea mate urais wanaendelea kuviziana kila moja akisubiri kuona hatua ambayo mwenzake atachukua katika juhudi za kubuni miungano ya kisiasa kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hakuna anayetaka kuanika wazi mipango yake kwa sasa japo mazungumzo ya kusuka miungano yanaendelea chini kwa chini hata kati ya wanaochukuliwa kuwa mahasimu wa kisiasa.

Hata Naibu Rais William Ruto ambaye amekuwa akitangaza wazi kwamba amejipanga kukabiliana na wapinzani anasemekana kuwa kwenye mazungumzo na baadhi ya wanasiasa wakuu wakiwemo vinara wa muungano unaoendelea kusukwa wa One Kenya Alliance.

Duru zinasema kwamba Dkt Ruto amekutana mara kadhaa na vinara wawili wa OKA katika juhudi za kuwashawishi wamuunge mkono.

Muungano wa OKA unaleta pamoja Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.

Ingawa wanne hao wanasisitiza kuwa wako pamoja na wanaendelea kujipanga kabla ya kuzindua rasmi muungano huo, inasemekana kuwa kuna tofauti zinazoweza kuwafanya watengane.

Tayari chama cha Kanu kimeashiria kuwa huenda kikajiondoa kwa kuwa kina mkataba wa muungano na chama cha Jubilee ambacho kinawania kuungana na ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wamesema kuwa hawawezi kumuunga Bw Odinga ambaye alikuwa mshirika wao katika uliokuwa muungano wa NASA kugombea urais.

Ingawa kufikia sasa Bw Odinga hajatangaza azima yake ya kugombea uais kwa mara ya tano kwenye uchaguzi mkuu ujao, hatua ambazo yeye na chama chake kimechukua zinaonyesha jina lake litakuwa kwenye debe.

Wadadisi wa siasa wanasema hii ndiyo sababu ODM kiliondoka NASA ili mkataba uliomfunga Bw Odinga usiwe kizingiti kwake kugombea na kusuka muungano mpya.

ODM na Jubilee zimetangaza kuwa zitaungana kwenye uchaguzi mkuu ujao, muungano ambao huenda ukahusisha vyama vingine vikubwa na vidogo.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, mviziano unaoendelea ni kwa sababu hakuna mwanasiasa anayetaka kujitokeza kujifunga katika muungano ambao utamtumbukiza kwenye baridi ya kisiasa.

“Baadhi ya vigogo wa kisiasa wanaomezea mate urais wamekuwa kwenye baridi ya kisiasa kwa miaka mingi na hawataki kufanya makosa kwa kujifunga kwenye miungano. Pia, kuna presha kutoka kwa wanaoshawishi hali ya siasa nchini kwamba wanafaa kufuata mkondo fulani,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Larry Ouko.

Inasemekana kuwa ingawa vinara wa OKA waliokuwa kwenye NASA wamesema hawatamuunga Bw Odinga, baadhi yao wamekuwa wakizungumza naye kwa lengo la kushirikiana kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa ingawa chama chake kinasuka muungano na Jubilee anapanga chombo kikubwa kitakachomshinda Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Vinara wa OKA nao wamekuwa wakisema kwamba wanapanua muungano wanaosuka kushirikisha vigogo wengine akiwemo Bw Odinga kama kinara mwenza na sio mgombea urais.

Kuna minong’ono kwamba lengo la vinara wa OKA ni kuunda chombo vya kuongeza thamani kwenye meza ya mazungumzo ya kubuni muungano mkubwa kabla au baada ya uchaguzi.

Inasemekana tayari Bw Odinga na Dkt Ruto wameanza kuvizia vinara wa muunagano huo kila mmoja akitaka kuwavuta upande wake.

Tayari, Bw Odinga amekutana na Bw Moi na kuna kila dalili kwamba watashirikiana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Duru za kuaminika zinasema kwamba Bw Odinga na Bw Musyoka wamekuwa wakizungumza bila kuhusisha washirika wao ambao inaaminika wana misimamo mikali.

Kulingana na mdadisi wa siasa Gabrel Kauma, kinachoendelea kwa sasa ni kupimana tu lakini miungano halisi itajitokeza mwaka ujao.

“Kitu kingine ambacho kitafanya vigogo wa kisiasa kutoka kwenye viota vyao ni uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusu Mswada wa kura ya maamuzi kuhusu BBI. Mswada huo una minofu kwa wanasiasa kwa kuwa unatoa nafasi za kugawana,” asema Kauma.

Mahakama ya Rufaa inatarajiwa kutoa uamuzi wake Agosti 20 na Bw Kauma anasema huu utakuwa ufunguo wa miungano ya kisiasa.

Bw Kauma anasema kwamba mviziano huu umejitokeza pia katika maeneo baada ya viongozi kukosa kuwapa mwelekeo uchaguzi mkuu ukikaribia.

“Kwa mfano, eneo la Mlima Kenya liko katika ulimbo wa kisiasa kwa kuwa Rais Kenyatta hajatangaza anayetaka kuwa mrithi wake. Kwa wakati huu ni dalili kwamba huenda hatatimiza ahadi yake ya kumunga Dkt Ruto ambaye ameunda chombo kujiandaa kugombea urais. Kuna dalili pia anaweza kumuunga Bw Odinga ambaye ni mshirika wake kwenye handisheki,” asema.

Mdadisi huyu anasema kwa kutopatia ngome yake mwelekeo wa siasa za urithi wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Rais Kenyatta amewaacha washirika wake njia panda.

You can share this post!

Kenya Lionesses yaimarisha mazoezi kwa mechi ya kufuzu...

Shambulizi la bomu 1998 lilivyomtosa kwa usanii