• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Wafuasi wa Ruto wahofia wimbi la Karua

Wafuasi wa Ruto wahofia wimbi la Karua

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya mwanasiasa Mwangi Kiunjuri kuwarai wenyeji wa Mlima Kenya kuwapigia kura viongozi bila kujali vyama vyao, imeibua hofu kuhusu mustakabali wa kisiasa wa muungano wa Kenya Kwanza katika eneo hilo.

Bw Kiunjuri, aliyehudumu kama waziri wa Kilimo na Ugatuzi mtawalia, ndiye kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP), ambacho kiko katika mrengo huo.

Mrengo huo unavishirikisha vyama vya UDA, ANC, Ford-Kenya kati ya vingine, ambapo vinamuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti.

Ijapokuwa Bw Kiunjuri amekuwa akimpigia debe Dkt Ruto, alionekana kubadilisha msimamo wake Jumatano, baada ya kuwarai wenyeji “kuwachagua viongozi wawatakao bila kuzingatia vyama vyao.”

“Chagueni viongozi watakaowasaidia. Msidanyanyike na mawimbi ya kisiasa yanayoletwa na vyama,” akasema Bw Kiunjuri, kwenye mahojiano na runinga moja.

Kulingana na wadadisi wa siasa, kauli ya Bw Kiunjuri inaashiria “mwelekeo mpya wa kisiasa katika ukanda huo.”

Vile vile, wanasema kauli yake inaashiria tashwishi kuhusu baadhi ya ahadi ambazo Dkt Ruto amekuwa akitoa kwa wenyeji wa eneo hilo.“Bw Kiunjuri ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa ambao wana tajriba pana ya kisiasa katika Mlima Kenya. Tashwishi yake inaashiria hali ya kutoridhika miongoni mwa wanasiasa walio katika kambi ya Dkt Ruto. Ni kauli inayoashiria kwamba huenda tukaanza kushuhudia mwelekeo mpya wa kisiasa katika ukanda huo,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Matamshi ya Bw Kiunjuri yanatokea siku chache tu, baada ya aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo, kueleza wasiwasi wake kuhusu nafasi ya Mlima Kenya katika mrengo wa Kenya Kwanza, kufuatia mkataba uliowasilishwa kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Bw Kabogo alimtaka Dkt Ruto kuweka wazi “mgao” wa Mlima Kenya katika serikali yake, kama ilivyo kwa vyama kama ANC, Ford-Kenya, Pamoja African Alliance (PAA) na Maendeleo Chap Chap (MCC) chake Gavana Alfred Mutua (Machakos).

“Tunataka kujua nafasi ya Mlima Kenya ni ipi ndipo tujue mgao wetu katika serikali ya Dkt Ruto,” akasema Bw Kabogo.

Kutokana na tashwishi hizo, Prof Njoroge anaonya huenda mwelekeo huo ukaashiria mwanzo wa kupungua kwa umaarufu wa Dkt Ruto.

“Kabla ya uteuzi wa Bi Martha Karua kama mgombea-mwenza wa Bw Raila Odinga, Mlima Kenya ilionekana kutokuwa na mwelekeo mwingine wa kisiasa. Hilo ni miongoni mwa sababu zilizomfanya Ruto kupata uungwaji mkono kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, ujio wa Bi Karua na tashwishi kuhusu nafasi ya eneo hilo katika muungano huo ni sababu ambazo huenda zikaufanya umaarufu wake kushuka ikiwa hatachukua tahadhari za mapema,” akasema Alhamisi.

You can share this post!

Ruto aahidi atakubali matokeo akishindwa

Rift Valley Prisons yalenga kubeba taji la voliboli nchini...

T L