• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Waliosaidiwa na Uhuru wamgeuka

Waliosaidiwa na Uhuru wamgeuka

NA WANDERI KAMAU

RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta amegeukwa na baadhi ya viongozi aliolea, kuwajenga na kuwatetea kisiasa kwa miaka kumi ambayo alikuwa uongozini.

Katika siku za hivi karibuni baadhi ya wanasiasa aliolea wamemgeuka na kutaka kutwaa chama alichotumia kuwaingiza katika siasa cha Jubilee. Ni mwelekeo unaozua taswira ya ‘asante ya punda ni teke’, ikizingatiwa baadhi ya wanasiasa hao ndio wanaoongoza juhudi za kumpiga vita Bw Kenyatta, hasa kwenye udhibiti wa Jubilee na kumpokonya wadhifa wa msemaji wa Mlima Kenya.

Baadhi ya wanasiasa aliowalea ni Mbunge Maalum Sabina Chege, Waziri Moses Kuria (Biashara na Viwanda), Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa, Gavana Anne Waiguru (Kirinyaga), wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Kanini Kega (EALA), Ngunjiri Wambugu (mbunge wa zamani, Nyeri Mjini), mwenyekiti wa Jubilee Nelson Dzuya kati ya wengine wengi.

Idadi kubwa ya wanasiasa hao waliingia katika Bunge la Kitaifa kupitia chama cha The National Alliance (TNA) na Jubilee katika miaka ya 2013 na 2017 mtawalia, wakati vilikuwa maarufu katika ukanda wa Mlima Kenya.

Bi Chege alichaguliwa kama Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Murang’a kupitia chama cha TNA mnamo 2013, alichoongoza Bw Kenyatta, alipowania urais kupitia Muungano wa Jubilee.

Alishinda tena nafasi hiyo 2017 kupitia Jubilee, aliyoongoza Bw Kenyatta.

Kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022 alihudumu kama mmoja wa wanachama wakuu wa Baraza la Azimio la Umoja, aliotumia Bw Raila Odinga kuwania urais.

Hata hivyo, Bi Chege sasa amemgeuka Bw Kenyatta, kwani ni miongoni mwa wanasiasa wanaolenga kumpindua kama kiongozi wa Jubilee. Tayari, Bi Chege ameteuliwa kama kiongozi wa Jubilee kuchukua nafasi ya Uhuru katika hali tatanishi.

Mbunge Maalum Sabina Chege ambaye ni wa Jubilee Party. PICHA | MAKTABA

Bw Kuria pia ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamegeuka kuwa wakosoaji sugu wa Bw Kenyatta. Hii ni licha ya kuwa Bw Kenyatta ndiye aliyemsaidia Bw Kuria kuingia bungeni kama mbunge wa Gatundu Kusini 2014 bila kupingwa kupitia TNA.

Bw Kuria aliingia bungeni kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Jossy Ngugi. Mnamo 2017, Bw Kuria alichaguliwa tena kwa miaka mitano kama mbunge wa eneo hilo kupitia Jubilee.

Licha ya ‘msaada’ huo wa kisiasa, Bw Kuria amegeuka kuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa Bw Kenyatta, kwa kumrushia cheche kali za maneno, hasa baada yake kutangaza kumuunga mkono Bw Odinga kuwania urais 2022.

Hali ni kama hiyo kwa Gavana Waiguru, kwani kama wanasiasa wengine, Bw Kenyatta alimtetea pakubwa kati ya 2014 na 2015, alipokabiliwa na tuhuma za ufisadi, alipohudumu kama Waziri wa Ugatuzi.

Akiwa Waziri wa Ugatuzi, Bi Waiguru alikabiliwa na shinikizo nyingi kutoka kwa mrengo wa Cord (ukiongozwa na Bw Odinga), ambapo ulimtaka kujiuzulu kutokana na kashfa ya uporaji wa zaidi ya Sh790 milioni katika Shirika la Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS). Bw Ichung’wa alichaguliwa kama mbunge wa Kikuyu kwa mara ya kwanza mnamo 2013 kupitia tiketi ya TNA.

Mnamo 2017, alishinda bila kupingwa kama mbunge kwa tiketi ya Jubilee. Naibu Rais Rigathi Gachagua alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge wa Mathira kwa tiketi ya Jubilee mnamo 2017. Kabla ya hapo, alihudumu kama afisa wa utawala wa mkoa na Msaidizi wa Kibinafsi wa Bw Kenyatta kati ya 2001 na 2006. Licha ya kutumia Jubilee kuingia bungeni kwa mara ya kwanza, Bw Gachagua amegeuka kuwa mkosoaji mkuu wa Bw Kenyatta, akimlaumu kwa “kulisaliti” eneo la Mlima Kenya licha ya kumuunga mkono 2013 na 2017 alipowania urais.

Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi pia amemgeuka Bw Kenyatta, licha ya kuwa miongoni mwa viongozi ambao Bw Kenyatta alishirikiana nao kuanzisha chama cha TNA. Bw Sakaja alihudumu kama mwenyekiti wa TNA kati ya 2013 na 2016. Pia, alihudumu kama Mbunge Maalum kati ya 2013 na 2017 baada ya kuteuliwa na chama hicho. Mnamo 2017, aliwania Useneta katika Kaunti ya Nairobi kwa tiketi ya Jubilee na kuibuka mshindi. Hata hivyo, aliiasi Jubilee 2022 na kuchaguliwa kama gavana kwa tiketi ya UDA, chake Rais Ruto.

Mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) alichaguliwa 2017 kwa mara ya kwanza kwa kutumia picha ya Bw Kenyatta kujipigia debe. Bw Kanini Kega, sawa na wengine, alichaguliwa kama mbunge kwa mara ya kwanza 2013 kwa tiketi ya TNA. Kwa sasa, Bw Kega anahudumu kama mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kupitia chama Jubilee, anachoongoza Bw Kenyatta. Kutokana na hilo, wadadisi wanasema kuwa mwelekeo huo ni hali ya kawaida ya kisiasa inayoshuhudiwa wakati wanasiasa wachanga wanahisi “kukomaa kisiasa”.

“Ingawa huenda wengi wakawalaumu wanasiasa hao kwa ‘kumdharau’ Bw Kenyatta, ukweli ni kuwa, wengi wanahisi wamepata mabawa na hawamtegemei tena Bw Kenyatta kujiendeleza na kujisimamia kisiasa,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Mchanganuzi wa siasa Martin Andati naye anasema kuwa umuhimu wa kisiasa wa Bw Kenyatta ulipungua tu wakati alipong’atuka kutoka uongozini baada ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

“Wanasiasa wengi wanamwasi Bw Kenyatta na kumfuata Rais William Ruto kwani Bw Kenyatta hana ushawishi wa kisiasa aliokuwa nao kabla ya kuondoka uongozini. Mielekeo ya wanasiasa wengi inasukumwa na maslahi na mustakabali wao wa kisiasa,” akasema Bw Andati.

  • Tags

You can share this post!

Kindiki awasili Malindi kuelekea Shakahola kufungua rasmi...

Wataalamu: Ushuru mpya utaumiza raia

T L