• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
WANDERI KAMAU: Changamoto tele Mlima ukijaribu kuja pamoja

WANDERI KAMAU: Changamoto tele Mlima ukijaribu kuja pamoja

Na WANDERI KAMAU

JUHUDI za kuliunganisha eneo la Mlima Kenya ielekeapo 2022 zinaonekana kukumbwa na changamoto tele, wadadisi wakisema huenda mikakati inayoendelea ikakosa kuzaa matunda.

Miongoni mwa juhudi zinazoendelea kwa sasa ni harakati za kuandaa kikao cha Limuru III, kinachotajwa kuwa cha mwisho kujaribu kuwaunganisha viongozi, wenyeji na mabwanyenye wenye ushawishi katika ukanda huo.

Tayari, imebainika kwamba kikao hicho kitaandaliwa Januari 22, 2022, kulingana na taarifa iliyotolewa na mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini).Bw Kuria ni miongoni mwa viongozi watatu wanaoendesha juhudi za kuliunganisha eneo hilo chini ya vuguvugu la Mt Kenya Unity Forum (MUF).

Washiriki wengine ni kiongozi wa Narc-Kenya, Martha Karua na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, ambaye pia ndiye kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP).“Msimamo wetu ni kuwa lazima wenyeji wa Mlima Kenya wawe na sauti moja.

Hilo ndilo lengo kuu la kuandaa kikao hicho,” akasema Bw Kuria.Licha ya juhudi hizo, wachanganuzi wanasema kuna uwezekano mkubwa kikao hicho kikakosa kubuni umoja wa kisiasa, ikizingatiwa harakati sawia hapo awali zilikosa kupata mafanikio.

Sauti moja

Miongoni mwa vikao hivyo ni kile kilichopangiwa kufanyika mjini Embu mnamo Septemba, ambapo viongozi wa vyama zaidi ya 20 vya kisiasa walitarajiwa kuhudhuria.Kulingana na wale waliokuwa wakishiriki katika maandalizi yake, lengo kuu lilikuwa kubuni “sauti moja ili kuondoa migawanyiko ya kisiasa ambayo imekuwepo.

”Hata hivyo, kikao hicho kiliahirishwa katika dakika za mwisho mwisho, baada ya baadhi ya wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ unaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto kudai “kutengwa.”“Hicho ni kikao kilichopangiwa na mrengo mmoja wa kisiasa unaodai kuwakilisha maslahi ya wenyeji wa Mlima Kenya.

Sisi tushaamua kwa pamoja tutamuunga mkono Dkt Ruto kuwania urais 2022. Hivyo, hatuhitaji kualikwa katika vikao vingine vya kuamua ‘mwelekeo wa Mlima’,” akasema mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu), ambaye ni miongoni mwa wafuasi sugu wa Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema dalili za mafanikio kutopatikana zi wazi, kwani mazingira ya kisiasa kwa sasa hayajabadilika.“Hali ya kisiasa iliyopo ni sawa na ilivyokuwa wakati vikao vya awali kama Limuru I na Limuru II vilifanyika.

Waandalizi waliviendesha kwa kutoshirikisha mirengo yote ya kisiasa. Hilo ndilo lililoongeza migawanyiko ambayo imekuwepo,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Makongamano

Anasema itabidi waandalizi kubuni mkakati mpya, ikizingatiwa migawanyiko hiyo imekuwepo licha ya Rais Uhuru Kenyatta kushiriki katika makongamano ya Sagana I na II, ambayo pia yalilenga kubuni umoja wa kisiasa katika eneo hilo.

Sababu nyingine inayotajwa kuwa kizingiti ni uwezekano wa wanasiasa wengi kutohudhuria, kwani watakuwa mashinani wakifanya kampeni za kutetea viti vyao.Wadadisi wanasema ingekuwa vizuri ikiwa kikao hicho kingeandaliwa mapema, wakati harakati za kampeni hazijaanza kushika kasi.

“Kwa maoni yangu, kikao hicho kimepelekwa mbali sana. Kingeandaliwa mwezi ujao (Novemba) ama Desemba wakati mazingira ya kisiasa bado yametulia ili kumpa Rais Kenyatta nafasi ya kuwakusanya wanasiasa wote ambao wamegawanyika katika mirengo tofauti,” asema mchanganuzi wa siasa Wathige Mwangi.

‘Kosa’ jingine linalohofiwa kuchangia kikao hicho kutofaulu ni hatua ya Rais Kenyatta kuonyesha wazi anamuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kuwa mrithi wake.Wadadisi wanasema ikiwa lengo kuu la kikao hicho ni kubuni mwelekeo wa pamoja wa Mlima Kenya, basi ingekuwa vizuri ikiwa Rais Kenyatta hangeonyesha mrengo wa kisiasa ama mgombea urais anayeunga mkono.

“Kutokana na msimamo wa wazi ambao Rais Kenyatta ameonyesha, hisia zilizopo miongoni mwa viongozi wengi ni kuwa lengo la kikao hicho ni kuwashinikiza kuchukua mwelekeo uo huo. Hivyo, ili kikao hicho kufaulu, lazima waandalizi waondoe dhana hiyo,” akasema Bw Mwangi.

Licha ya hofu hizo, waandalizi wanashikilia kikao hicho ki wazi na hakilengi kuwashinikiza washiriki kuunga mkono mrengo wowote wa kisiasa.Wanasema lengo lao ni kuhakikisha maslahi ya wenyeji yatazingatiwa kikamilifu na mrengo wa kisiasa watakaouunga mkono.

“Moja ya madhila eneo hili lilipitia ni kutengwa kisiasa na kiuchumi na utawala wa marehemu Daniel Moi kwa miaka 24 aliyoiongoza nchi. Wenyeji waliteseka sana baada ya serikali kutekeleza sekta muhimu kama kilimo, kwani walikuwa wakiunga mkono upinzani.

Tunataka kuhakikisha maslahi yetu yatazingatiwa na yeyote atakayekuwa mamlakani, hata ikiwa si mmoja wetu atakuwa uongozini,” akasema aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo.Hata hivyo, washirika wa Dkt Ruto wanasisitiza huenda kikao kikakosa kupata mafanikio yoyote, ikiwa Rais “ataanza kuwakemea watu kama ambavyo amekuwa akifanya awali.”

“Vikao hivvyo vinapaswa kuwapa nafasi watu kushauriana wala si kupewa mihadhara na washiriki wengine. Kama mrengo wa ‘Hustler Nation’, tushawasilisha matakwa ambayo tungemtaka Dkt Ruto ayashughulikie atakapotwaa uongozi.

Hivyo, hatuna haja kushiriki katika vikao vingine,” akasema mbunge Rigathi Gachagua (Mathira).

You can share this post!

Mwanamke ni shujaa

CECIL ODONGO: Raila akiacha dhana ya ‘mradi’ ishike...

T L