• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
Washirika wa Ruto wadai Obado avuruga chama cha Naibu Rais

Washirika wa Ruto wadai Obado avuruga chama cha Naibu Rais

Na IAN BYRON

HATUA ya Gavana Okoth Obado kujihusisha na siasa za chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais, Dkt William Ruto imezua mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wa chama hicho katika Kaunti ya Migori.

Baadhi ya wanasiasa wa UDA sasa wanamshuku Bw Obado, wakisema huenda anatumia chama chake cha PDP kusimamia kampeni za Dkt Ruto huku wanachama halisi wa UDA wakipigwa kumbo.Mbunge wa Kuria Magharibi, Mathias Robi amekashifu Bw Obado akisema kuwa anavumisha PDP badala ya UDA na kuna wawaniaji ambao anawadhamini ili kuvuruga umaarufu wa UDA.

“PDP si maarufu hapa na juhudi za kumfanya ajiunge na UDA zimegonga mwamba. UDA ina sura ya kitaifa na ujio wa Obado kwenye mrengo wa Dkt Ruto umeibua taharuki miongoni mwa wawaniaji na wajumbe wetu,” akasema Bw Robi.

“Tuna wawaniaji wengi wa UDA eneo la Luo Nyanza na tunakabiliana na kibarua kigumu katika kutayarisha uteuzi wetu kutokana na siasa zetu kuingiliwa na PDP,” akaongeza. Mwaniaji wa kiti cha ugavana katika Kaunti ya Migori, Bi Jane Moronge alidai kuwa wakati wa ziara ya Naibu Rais katika eneo hilo hivi majuzi, Bw Obado alidhibiti shughuli zote na hata wao kama wanachama wa UDA hawakuhusishwa.

Huku uhasama wa kisiasa ukiendelea kutokota kati ya UDA na PDP, Naibu Gavana wa Migori, Mwita Mahanga naye amewataka wakazi wa kaunti hiyo waendelee kuunga mkono chama cha ODM na siasa za kiongozi wake Raila Odinga.

You can share this post!

Arati akana dai la kuzua fujo kanisani

Mwendwa atupwa seli tena baada ya kukana mashtaka

T L