• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Wazee wakemea mzozo wa ugavana Wajir

Wazee wakemea mzozo wa ugavana Wajir

Na FARHIYA HUSSEIN

WAZEE kutoka Kaunti ya Wajir wamemtaka aliyekuwa gavana wa Kaunti hiyo, Mohamed Abdi na mwenzake Ahmed Muktar kuzingatia uamuzi uliotolewa na korti na kusitisha vita vyao vya kisiasa.

Wakiwaonya viongozi hao wawili, wazee hao walitaja vitendo vyao kuwa aibu kubwa katika jamii ya Wajir.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Wajir, Sheikh Noor Ahmed alisema wazee wanazungumza kwa sauti moja na wametoa onyo kwa viongozi hao wawili.

“Hatutaki kujua kama wewe ni Ajuran, Degodia, Kamba au Kikuyu. Ikiwa wewe ni mkazi wa Wajir, hatutaki aibu,” akasema Bw Ahmed.

Wazee walionya kuwa ikiwa jambo hilo halitatatuliwa kwa haraka, wakazi wataathiriwa pakubwa.

Bw Mohammed Dahiye, mzee mwingine, alisema viongozi hao hawajali jamii na wanaweza kuchangia chuki kati ya wenyeji.

Akizungumzia tukio la Jumatano ambapo Bw Abdi alishambulia ofisi za kaunti na kuingia kwa nguvu, Mzee Dahiye alitaja kitendo hicho kama kinyume na sheria za nchi.

“Kuna njia ya utulivu na amani ya kusuluhisha maswala yanayoendelea ila si kuingia majengo ya kaunti kwa nguvu. Tunalaani kitendo hicho. Viongozi wa bunge la kitaifa ambao walionekana wakiunga mkono kitendo hicho wametuaibisha. Wasihusishe wakazi wa Wajir katika ugomvi wao,” akasema Bw Dahiye.

“Kutumia maafisa wa polisi kukusindikiza ili kuingia katika ofisi za kaunti kwa nguvu si suluhisho. Hatutaki wakazi wa Wajir kujulikana kwa njia kama hizo,” akasema Bw Osman Madope.

Wazee hao wamewahimiza viongozi hao wawili wa kisiasa kutafuta njia mbadala za kutatua mizozo yao.

You can share this post!

Makala ya spoti- Bandari FC

KIKOLEZO: Wa-totos na pesa