• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Weta sasa kuvumisha Ruto kikamilifu akisubiri kutetea kiti Bungoma

Weta sasa kuvumisha Ruto kikamilifu akisubiri kutetea kiti Bungoma

NA BRIAN OJAMAA

KIONGOZI wa Ford Kenya, Jumapili aliidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutetea kiti chake cha Useneta wa Bungoma katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Bw Wetang’ula alisema hatua hiyo sasa itamwezesha kuelekeza juhudi zake katika kampeni za kitaifa za kupigia debe mgombea urais wa muungano wa Kenya Kwanza William Ruto.

“Tumepita hatua hii na sasa nitajitosa mzima mzima katika kampeni za kumtafutia kura mgombea wetu wa urais Dkt Ruto. Kampeni zetu hapa Bungoma sasa zitasimamiwa na Spika wa Seneti Ken Lusaka na maafisa wengine wa Ford Kenya,” Bw Wetang’ula akasema.

“Wajibu wetu mkubwa kama kaunti ni kuungana na kaunti nyinginezo kutoka eneo hilo na taifa kwa ujumla kuunda serikali ijayo kwa manufaa ya watu wetu,” akaongeza.

IEBC ilitoa wito kwa Bw Wetang’ula kuendesha kampeni ya amani, ikionya kumchukulia hatua za kisheria endapo wafuasi wake watachochea fujo.

“Kama tume, tunakutakia kila la kheri huku tukikuhimiza kuendesha kampeni za amani ambazo zitadumisha utulivu nchini,” akasema afisa msimamizi wa uchaguzi katika kaunti ya Bungoma, Bi Gladys Rono.

Akiongea na wanahabari baadaye, Seneta huyo wa Bungoma, alielezea imani kuwa atahifadhi kiti kwa kupata ushindi mkubwa.

Alitetea uamuzi wake wa kutetea kiti hicho akisema haukuongozwa na maslahi ya kibinafsi.

“Watu wengi, haswa katika mrengo wa Azimio wameuliza ni kwa nini ninatetea kiti changu ilhali tumetengewa viti katika serikali ya kitaifa endapo Kenya Kwanza itashinda. Ningetaka kurudia hapa kwamba siwanii kwa sababu ya manufaa yangu kama mtu binafsi bali manufaa ya watu wetu,” Bw Wetangúla akasema.

“Asilimia 30 ya serikali ambayo tumetengewa katika serikali ya Kenya Kwanza iko imara. Chama cha Ford Kenya kitapata mawaziri watatu, ANC kitatunukiwa mawaziri wengine watatu. Hii ni kando na nafasi za makatibu wa wizara na mabalozi,” akaeleza.

Bw Wetang’ula alisema hizo nyadhifa sio zake bali yeye ameridhika na cheo chake cha sasa kama seneta na “baba wa kaunti ya Bungoma na kama kiongozi wa kitaifa kutoka eneo hili.”

Pia alielezea imani kuwa muungano wa Kenya Kwanza utashinda na kuunda serikali ijayo, akisema kuwa wapinzani wao wa Azimio hawana ufuasi Bungoma na maeneo mengine ya Magharibi mwa Kenya.

You can share this post!

Maskini Homeboyz wajikwaa Ligi Kuu

Karan Patel ndiye mfalme wa Eldoret Rally

T L