• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Wetang’ula asuta Azimio

Wetang’ula asuta Azimio

NA BENSON MATHEKA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amesuta muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya unaongozwa na Raila Odinga kwa kutishia kufanya maandamano kushinikiza serikali kushughulikia matakwa ya muungano huo.

Bw Wetang’ula amemtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani kukumbatia mifumo ya amani kushughulikia matakwa yao kwa ustawi wa nchi.

“Ikiwa Raila na timu yake wana masilahi ya kaunti hizi moyoni, anapaswa kuhakikisha kuwa amani inakuwepo hata katika hali ambapo anakosoa serikali kama Kiongozi wa Upinzani,” amesema spika Wetang’ula.

Wetang’ula amesema hayo Ijumaa alipojumuika na familia, marafiki na jamaa katika kumuaga marehemu chifu mstaafu Mzee Julius Macheso Masibo katika kijiji cha Milo, wadi ya Sitikho katika eneobunge la Webuye Magharibi.

Amesema kuwa Kenya inahitaji amani kuendelea kuvutia wawekezaji wa kigeni na wale wanaopanga kuvuruga utulivu wa nchi wanapaswa kujua kwamba “hatuna nchi nyingine.”

Kulingana na Bw Wetang’ula, hakuna nchi inayoweza kuimarika kiuchumi bila uthabiti huku akiwataka Wakenya kuendelea kuliombea taifa pamoja na utawala wa Kenya Kwanza.

“Tuendelee kushirikiana, tupendane ili nchi yetu iwe na amani. Hatuna nchi nyingine na hata watu hawa wanaostawi katika machafuko, tunataka kuwaambia kwamba kuna njia nyingi lakini msiharibu nchi yetu. Tunataka amani kwa sababu bila amani hatuwezi kujiendeleza na bila maendeleo, hatuwezi kusonga mbele,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

‘Nabii Yohana wa Tano’ ahojiwa na maafisa wa...

Polisi wawili wauawa na Al-Shabaab katika Kaunti ya Mandera

T L