• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Ziara ya Ruto Nyanza yatia Kalonzo presha

Ziara ya Ruto Nyanza yatia Kalonzo presha

VIONGOZI kutoka eneo la Ukambani wameanzisha kampeni ya kumshiniza kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kutengana na kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga.

Vigogo wa UDA wa Ukambani na baadhi ya viongozi wa Wiper, wanataka Bw Musyoka kukubali kushirikiana na Rais William Ruto ili kuletea eneo hilo maendeleo.

Shinikizo za kutaka ashirikiane na Rais Ruto zimekuwa zikitolewa na wandani wake waliochaguliwa kupitia chama cha Wiper pamoja na mahasimu wake wa kisiasa.

Hatua ya Bw Odinga kuruhusu viongozi wa ODM kumpokea Rais Ruto alipozuru kaunti za Luo Nyanza wiki mbili zilizopita, imezidisha presha ya kumtaka Bw Musyoka akumbatie serikali ya Kenya Kwanza.

Wandani wa Rais Ruto wanatarajiwa kufungua afisi ya UDA ambayo itakuwa makao makuu ya eneo la Ukambani mjini Wote, Kaunti ya Makueni.

Viongozi wa UDA waliohojiwa na Taifa Leo walisema kuwa, afisi hiyo inalenga kutoa ushindani mkali kwa chama cha Wiper ambacho kimekuwa kikidhibiti siasa za eneo la Ukambani.

Wandani wa Rais Ruto pia wamekuwa wakiandaa msururu wa mikutano inayohusisha viongozi wa kidini katika juhudi za kushinikiza Bw Musyoka kukumbatia serikali ya Kenya Kwanza.

“Tunakualika kuhudhuria mkutano wa kutoa shukrani kwa Mungu kutokana na maajabu ambayo ametendea watu wa Ukambani,” ikasema barua ya mwaliko ambayo imetumiwa viongozi mbalimbali wa eneo hilo.

Mkutano huo ambao mmoja wa waandalizi wake ni mwenyekiti wa UDA, Johnson Muthama, utafanyika katika eneo la Migwani, Kaunti ya Kitui.

Huo utakuwa mkutano wa tatu baada ya mingine miwili iliyofanyika katika Kaunti za Machakos na Kitui ambapo wamekuwa wakishukuru Rais Ruto kwa kuteua mawaziri wanne na makatibu wa wizara watatu kutoka eneo la Ukambani.

Wamekuwa wakitumia mikutano hiyo pia kuhimiza wakazi wa Ukambani kuunga mkono Rais Ruto.Aliyekuwa Seneta wa Kitui David Musila ni miongoni mwa wandani wa karibu wa Bw Musyoka ambao wamemtoroka na kuunga mkono Rais Ruto.

Kwa mujibu wa Bw Musila, jamii ya Wakamba imekuwa katika ‘baridi ya kisiasa’ kwa muda mrefu na wakati wa Bw Musyoka kuwaongoza kuelekea serikalini umewadia.

Bw Musila pia anashikilia kuwa, hakuna uwezekano wa Bw Musyoka kumshinda Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Minong’ono kwamba Bw Odinga huenda anajiandaa kushirikiana na Rais Ruto, imezidisha shinikizo za kumtaka kulegeza msimamo wake na kukubali kufanya kazi na serikali.

Bw Musyoka ambaye ametangaza kuwania urais 2027, anahofia kuwa akikubali kushirikiana na Rais Ruto, huenda akapoteza ushawishi wa kisiasa nchini.

“Ukizingatia mapokezi mazuri aliyopata Rais Ruto alipozuru Nyanza, hata sisi wakazi wa Ukambani hatuna budi kukumbatia serikali. Jamii ya Wakamba inafaa kufanya hima na kuingia serikalini ili tusije tukaachwa nyuma,” akasema Dkt Maurice Wambua, mdadisi wa masuala ya kisiasa katika eneo la Ukambani.

Msimamo wa Bw Musyoka kwamba ataendelea kusalia katika upinzani, umegawanya wandani wake.

Baadhi ya viongozi wa Wiper ambao wamekuwa wakishinikiza Bw Musyoka kukumbatia Rais Ruto ni Magavana Julius Malombe (Kitui), Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na Wavinya Ndeti (Machakos), na wabunge Patrick Makau (Mavoko) na Jessica Mbalu (Kibwezi Mashariki).

Bw Makau hivi majuzi alionya kuwa itakuwa vigumu kwa Bw Musyoka kushinda Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

“Mheshimiwa Rais (Ruto), nimesoma manifesto yako na nimebaini kuwa hakuna atakayekushinda 2027. Ni Mungu tu atakusimamisha. Katika uchaguzi wa 2022 tulipigia Raila kura lakini nakuhakikishia kuwa vindu vichenjaga (mambo yamebadilika),” akasema Bw Makau.

Kauli hiyo ilifasiriwa kuwa uasi wa wazi dhidi ya Kalonzo.Katika juhudi za kumpiku Kalonzo, Rais Ruto amekuwa akionekana kuwa ‘mwokozi’ wa wakazi wa eneo la Ukambani kutokana na tatizo sugu la ukosefu wa maji.

Rais Ruto amekuwa akituma wakuu wa Wizara ya Maji kukagua miradi mbalimbali ya maji katika kaunti tatu za Ukambani.

Mapema mwezi huu Januari, Waziri wa Maji Alice Wahome alizuru Bwawa la Thwake linalojengwa kwa Sh64 bilioni katika mpaka wa Kaunti za Kitui na Makueni.

Katibu wa Wizara ya Maji Kiprono Ronoh wiki iliyopita ailizuru Kaunti za Kitui na Machakos kukagua miradi ya maji.

Bw Ronoh aliandamana na Dkt Malombe na Bi Ndeti alipokuwa akikagua miradi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Saba wafariki kwenye ajali barabarani

Kipusa atimua malofa kupanga njama ya kumtongoza wakidai...

T L