Sichukii wanaume, ninazingatia haki ninapotoa uamuzi – Koome

Sichukii wanaume, ninazingatia haki ninapotoa uamuzi – Koome

Na SAMMY WAWERU

JAJI Mkuu mteule Bi Martha Koome amejitetea vikali dhidi ya madai kuwa anachukia jinsia ya kiume kufuatia maamuzi yake kadha awali anaposikiliza kesi.

Akipigwa msasa Alhamisi na Kamati ya Masuala ya Sheria bungeni, CJ Koome aliambia wabunge kuwa huzingatia ukweli, sheria na haki anapotoa uamuzi baada ya kusikiliza kesi.

Hilo liliibuka baada ya kamati hiyo kutaka kujua endapo hubaguwa kwenye maamuzi yake, kufuatia malalamishi yaliyowasilishwa.

“Ninaposikiliza kesi, huzingatia ukweli. Huwa siangalii ikiwa mlalamishi ni mwanaume au mwanamke,” Jaji Koome akajitetea.

Jaji huyo alisema yeye ni mzazi, na “mama wa familia ambaye amekuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka 35”.

“Ninawahakikishia huwa sibagui jinsia yoyote, huzingatia ukweli, sheria na haki,” akaambia wabunge.

Kamati hiyo ya sheria ilimpiga msasa baada ya jopokazi la makamishna wa tume ya huduma za mahakama (JSC) kutangaza kumteua kama Jaji Mkuu, na majina yake kupokezwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliyawasilisha bungeni.

Endapo bunge itapitisha uteuzi wake, Rais Kenyatta atamuidhinisha rasmi ili aapishwe kuhudumu kama Rais wa Idara ya Mahakama kipindi cha muda wa miaka minne mfululizo.

Kiti hicho kilisalia wazi baada ya kustaafu kwa Jaji Mkuu David Maraga, mnamo Desemba 2020.

You can share this post!

Lukaku na Young watozwa faini kwa kukiuka kanuni za corona...

Mchuuzi wa ndizi taabani kwa kupatikana na Sh900,000 ndani...