Habari Mseto

Sielewi nilikuwa nafikiria nini nikianguka kwa eskaleta – Nyota Ndogo

May 29th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSANII kutoka Pwani, Nyota Ndogo alichekelewa na kutaniwa katika kituo cha treni la kisasa jijini Nairobi wikendi, baada ya kuanguka kutoka kwa eskaleta.

Akiwa ameandamana namumewe Henning Nilesen, Nyota Ndogo alielezea jinsi Wakenya walimchekelea kwa dhihaka huku akianguka licha ya wengine kumsaidia kusimama.

“Baada ya kuanguka pale SGR Nairobi na mabagi yangu nikachekwa mpaka nikaskia kulia. Yaani mashabiki walinicheka huku wakinipa pole. Yaani zile ngazi za umeme leo zimeniaibisha kishenzi. Lakini hata sijui nilikua nafikiria nini kusimama na mabagi mawili yani,’’ akasema.

Ingawa hakuumia, nyota huyo alifichua kuwa alikuwa maetoka likizoni kule bara Ulaya na mumewe raia wa Uholanzi.

“Naihitaji hii likizo kwa kweli. Kwa miezi sita nimekua nikisimamia nyumba, kimbia nunua hii, hoo sijui nini hakuna, kidogo nishikwe na wazimu. Nafikiri pia uchovu ulichangia ile aibu ya pale SGR.’’