Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu zinazodhihirisha tofauti kati ya Isimu na Isimujamii

February 21st, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

TUNAENDELEA kuchambua isimu na isimujamii.

Tofauti nyingine inayojitokeza kati ya isimu na isimujamii ni kwamba, isimu inafuata mkabala wa ki-Chomsky wa kuchambua lugha kwa misingi ya kidhahania kuwa haina tofauti ndani yake wakati isimujamii hutambua kuwa lugha ina tofauti ndani yake, kwa maana kwamba ni mfumo wenye mifumo mingi ndani yake.

Hivyo basi  huona kuwa ni jukumu la isimujamii kuzitafiti na kuzifafanua tofauti hizo.

Tofauti nyingine inadhihirika katika vipengele. Hii ni kwa sababu vipengele vinavyoshughulikiwa na isimu ni tofauti na vile vinavyoshughulikiwa na isimujamii.

Kwa mfano, isimujamii hushughulikia vipengele kama vile, uhusiano kati ya lugha na utamaduni (elimu), matumizi ya lugha tofauti wakati mmoja, kama katika wingi lugha, ubadilishaji msimbo na diglosia. Matumizi ya aina tofauti za lugha na mazingira yake, kama lahaja, rejista na mtindo.

Pia hushughulikia vipengele mbalimbali vya mawasiliano kupitia maoni ya msemaji.

Tawi hilo pia huitwa isimu amali.

Matumizi ya lugha baina ya jamii za watu tofauti, kama lugha mawasiliano, pijini na kreoli, upangaji lugha na sera za lugha. Lakini isimu yenyewe hushughulikia vipengele kama fonolojia, fonetiki, mofolojia, sintaksia na semantiki.

Isitoshe, Florian Coulmas (1997), anadai kuwa tofauti kati ya isimu na isimujamii ni kwamba isimujamii ni taaluma ambayo hujihusisha tu na ufafanuzi wa lugha kama inavyoonekana ikitumika katika mazingira halisi.

Hivyo basi, kwa maoni yake, si jukumu la isimujamii kutafuta na kuchanganua data kuthibitisha au kukanusha nadharia yoyote kama ilivyo katika isimu.

Kwa sababu hiyo isimujamii ni “taaluma bila nadharia” kama anavyosema Mekacha (2000:31) akimnukuu Coulmas (1997).

Matawi

Vilevile, tofauti nyingine kati ya isimu na isimujamii ipo katika matawi au tanzu; kwa mujibu wa Mgullu (1990:4) isimu ni taaluma pana kuliko isimujamii.

Hii hujidhihirisha katika matawi yake ambayo mojawapo ni isimujamii yenyewe. Matawi mengine ni isimufafanuzi na isimu Kiafrika, isimuhistoria, isimulinganishi, isimutumizi, isimutiba, isimufalsafa.

Pamoja na kutofautiana kwa  taaluma hizi mbili ambazo ni isimu na isimujamii, bado taaluma hizi hukamilishana na vilevile hutegemeana hivi kwamba ili kimoja kiwepo ni lazima kingine kiwepo.

Mkamilishano wa taaluma hizi hudhihirika kwa njia mbalimbali ambazo tutajadili.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo:

   Msanjila, Y. P. (1990) “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili ni Teacher Training Colleges in Tanzania”.                  Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia”. Dar es Salaam: BAKITA.

Mulokozi, M. M. (1991) “English versus Kiswahili ni Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studies Ghent.