Makala

Sifa teule za maafisa ‘wamalizaji’

February 29th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

HAKUNA polisi au afisa wa usalama aliyesajiliwa kikosini ili awe muuaji lakini katika hali ya kazi, baadhi yao huchukua jukumu la ‘kumaliza’ kwa niaba ya usalama wa kitaifa.

Ili uwe mfaafu kwa kazi hiyo ya ‘umalizaji’ ni lazima uwe na roho ngumu, mapenzi na utu kiasi kwamba walio na unyama, utawaona tu kama taka.

Vile vile unatakiwa uwe na ujasiri wa kukubali kwamba kazi yako ni mbaya kuliko ya wahudumu wa vichinjio vya mifugo wasiozingatia mafundisho ya Mungu.

Ingawa hivyo, wanaharakati hupinga hayo kwa sababu mara nyingi kazi hiyo inahusu umwagaji damu pasipo kupitia hukumu za mahakamani.

Aidha huna budi kuwa mtiifu kwa imani kwamba mambo yanaweza yakakuendea kombo na urukwe na akili, ufungwe jela endapo utashtakiwa kwa njia ya kawaida au kufuatia shinikizo za wanaharakati, au hata ulengwe na majambazi na mitandao yao ya ufadhili wa magenge.

Kwa mujibu wa mahojiano na baadhi ya maafisa wa usalama, ukweli ni kwamba kuna mikutano ambayo huandaliwa kuhusu usalama wa nchi ambapo watu ambao huwa wamemulikwa kuuawa, hujadiliwa na utekelezaji kukabidhiwa maafisa wenye sifa hizi.

“Sio tu nchini Kenya. Hili ni suala la ulimwengu ambapo yumkini vyombo vya dola huua raia wake na pia wa kigeni kwa mujibu wa sheria fiche za suala pana la usalama,” akasema mmoja wa wadokezi wetu.

Hapa nchini, washukiwa wa ujambazi sugu ukiwemo yule wa ugaidi, wamekuwa wakishukiwa kuuawa baada ya kujadiliwa na kutambuliwa kama wasio na manufaa yoyote kwa maslahi ya usalama.

“Mambo ni… Ama utii, uhame nchini au usafirishwe mbinguni,” akanukiliwa Rais William Ruto aliposema ni sharti raia, wakazi na wafanyabiashara watii uzingativu wa sheria.

Kauli ya kiongozi wa nchi iliungwa mkono na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome.

Lakini ieleweke kwamba Rais Ruto alielezea kujitolea kwake kuleta mageuzi katika idara ya polisi.

Alisema kwamba tawala zilizopita zilikuwa zinatumia polisi vibaya ambapo baadhi ya maafisa walikuwa wakitekeleza mauaji kiholela wakilenga raia wasiokuwa na hatia.

Dokezi zetu katika vitengo vya polisi zinafichua kwamba uongozi wa kiusalama mara kwa mara hupokezwa majina ya waliowekewa shabaha ya kuuawa.

“Kuna kamati za masuala ya usalama ambazo ni za kitaifa na huhusisha Rais mwenyewe akiwa na washauri wake na pia mawaziri kadha. Ukiona jina lako limefika katika kikao hicho, wewe ni jambazi wa hadhi… umeweza kweli. Ukijadiliwa na iamuliwe uuawe, basi elewa yako ya uhai yameisha,” akasema.

Hali hii ilikuwa imedokezewa Wakenya mwaka wa 2007 ambapo aliyekuwa Waziri wa Usalama John Michuki alitangaza kanisani Murang’a kwamba “hakuna serikali itakubali kutekwa nyara na majambazi sugu pasipo kughadhabika na kulipiza kisasi”.

Akiwa amesakamwa na kero ya kundi haramu la Mungiki ambalo lilikuwa limezindua misururu ya kuua raia wasio na hatia kiholela, kutoza Wakenya ushuru haramu na kukeketa wanawake, Bw Michuki alitangaza mwisho wa kunyonyeshana kidevu.

“Nataka kutangazia watu wote waziwazi kwamba sitakubali utundu wa watoto wachache ambao wazazi wao wameshindwa kuwadhibiti. Ikiwa mtoto wako hakusikii ukimshauri afuate sheria, ujue leo kwamba serikali haitalemewa naye na mtakuwa tu mnasikia kuhusu mazishi yao,” akatangaza.

Japo haijulikani kilichotokea, washukiwa wa ufuasi katika kundi la Mungiki walianguka kiasi kwamba mkubwa wao ambaye alikuwa ni Maina Njenga aliishia kulivunja, akaokoka na akajitosa kwa ulingo wa kisiasa.

Maafisa wa ngazi ya juu vitengo vya usalama wanadokeza kwamba ukitambuliwa kwamba uzalendo wako uko katika kiwango cha juu na hungependa kuona taifa lako likiangamizwa na mahangaiko yanayosababishwa na wahalifu, wakiwemo majambazi na majangili, unaweza ukaingizwa ndani ya vitengo spesheli uwe ‘mmalizaji’ kwa niaba ya Wakenya.

“Kuna vile utatambuliwa na utasajiliwa. Kazi yako itakuwa spesheli ambapo ukipewa majina ya kushughulikia, unayawinda na unawasafirisha wakahukumiwe,” asema afisa huyo.

Katika harakati zetu za kusaka ufahamu kuhusu suala hili, tulikumbana na mmoja wa maafisa aliyehudumu katika kikosi cha ‘umalizaji’ lakini anaifananisha na “kazi ya kishetani”.

“Ukiingia huwa na maono kwamba unasaidia nchi na watu wake. Ukiendelea kuhudumu unaanza kuona majina mengine yamechaguliwa yaangamizwe ili kusaidia baadhi ya wakubwa wasijulikane ni washirika katika mtandao wa ujambazi. Unafika wakati mwingine ambapo unatumwa kummaliza huyu lakini unachanganyikiwa na unaua mwingine asiye na makosa,” akasema.

Aliongeza kuwa “kwingine unapata tu umetumwa kumaliza ili kulinda masilahi ya kisiasa wala sio kukinga binadamu wenzako na hatimaye harakati hizo zinageuka kuwa mkorogo ambao haueleweki”.

Na kwa kuwa vitengo vya usalama huendeshwa na amri za wakubwa ambazo huwezi ukakaidi, anasema inabaki tu kuomba Mungu akupe amani ya ubongo.

“Wengi huingilia utumizi wa pombe na mihadarati kiholela ili kujipa amani wakijua kwamba kujitoa ni vigumu kwa sababu tayari huwa wana siri za mauaji hayo. Mwishowe unageuka kuwa kigae… Mimi nilinusurika kibahati nilipohamishiwa kitengo cha ujasusi nchini kwa kuwa niko na masomo,” akasema.

[email protected]