Makala

Sifa za ‘Lumumba’, fahali mpya wa kivita aliyeteuliwa na Khalwale

February 10th, 2024 1 min read

Na CHARLES WASONGA

FAHALI aliyeteuliwa na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale kujaza pengo lililoachwa wazi na ‘Inasio’ anasheheni sifa za kumwezesha kuwa shujaa wa mashindano ya vita vya mafahali Ikolomani, kiongozi huyo amesema.

Akitangaza uteuzi wa fahali huyo kuchukua mahala pa mwezake aliyemuua mtunzaji wake, Kizito Amukune, mnamo Januari 28, Dkt Khalwale alimpa jina, ‘Lumumba’ na kumtaja kama fahali wa kivita mwenye uzani mkubwa na “mkali” zaidi, licha ya umri wake mdogo.

Hata hivyo, kwenye ujumbe wake kupitia akaunti ya mtandao wa X (zamani twitter), Dk Khalwale hakuelezea sababu za kuteua jina hilo.

“Viatu vikubwa vya mwendazake fahali wa kivita, ‘Inasio’, sasa vimevaliwa na fahali mdogo lakini stadi katika vita, Lumumba,” akasema.

“Mila ya tamaduni za Abaluhya hairuhusu uwepo wa pengo lolote. Kuna ukuruba mkubwa kati ya watu wetu na tamaduni zao,” Dkt Khalwale akaongeza huku akiandamanisha ujumbe huo na picha pamoja na video ya fahali Lumumba.

Uteuzi wa Lumumba sasa ni kiashirio cha umuhimu za kudumisha matendo ya kitamaduni na imani za jamii hiyo.

Kabla ya kumuua mtunzaji na mkufunzi wake wa miaka mingi, Amukune, ‘Inasio’ alikuwa bingwa wa mashindano ya vita vya mafahali katika eneo la Ikolomani.

Fahali huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitano na uzani wa kilo 120 alitawazwa bingwa katika mashindo ya kukaribisha mwaka Januari 1, 2024.

Kulingana na mila na desturi mafahali wa wa kutumiwa katika mashindano kama hayo hupewa majina ya kuwatambua.

Wao hupewa majina ya wanasiasa mashuhuri, wanaspoti, matukio ya kimaumbile au misimu.

Siku chache kabla ya mashindano hayo, mafahali hao huandaliwa vizuri kupewa lishe yenye madini ya kuwapa nguvu. Aidha, huzuiwa kukaribiana na ng’ombe jike wasije wakajamiiana nao na “kupoteza nguvu”.

Siku yenyewe ya mashindano, mafahali hao hunyweshwa pombe ya kitamaduni iliyochangwa na viungo vya kuwapa “ukali”.